ads

SHAIRI: WARIDI


 
Shamba ni kubwa urefu, lenye miche maarufu
miti yapita maelfu, na tofauti harufu
haina ulinganifu, kwa mapana na marefu
yanipalia harufu, waridi lilonadhifu
 
ua lililotulia, waridi linavutia
wengi walikimbilia, wapate kulitumia
na kinachowavutia, ni rangi na shepu pia
waridi lanikusudi, waridi linanibidi 
 
mti wake ni wa ndani, muhali kuwa porini
ameupanda jirani, wapo wachupao ndani
pigi, mawe na majani, mti wakosa amani
waridi lanikusudi, waridi linanibidi
 
lengo lao maadui, waridi lishe harufu
mtaani wanadai, lajifanya ni nadhifu
mti eti hauzai, yanini umaarufu
waridi lanikusudi, waridi linanibidi
 
asubuhi na jioni, mti upo lawamani
wengine wanatamani, waridi liwe porini
kusaidia jirani, silaha iwe begani
waridi lanikusudi, waridi linanibidi
 
natwika shaba begani, mti kuupa amani
ukombozi wa jirani, kulipachua mtini
kutolitupa porini, ni ahadi kwa jirani
waridi lanikusudi, waridi linanibidi
 
kwangu sasa kubwa dhima, harufu ikome ndani
natena nifanye hima, isizagae njiani
kwa waridi nikowima, hata kukaa sitamani
waridi lanikusudi, waridi linanibidi
 
kwa waridi sina kosa, jirani ameridhia
waridi limeninasa, ni kosa kuliachia
waridi limeniasa, harufuye kuridhia
waridi wangu wa moyo, barafu langu la roho.
 
Mtunzi: Mwinyi Abdallah
Phone: 0655 895599
Email: mwinyiabdallah2012@gmail.com

Post a Comment

0 Comments