ads

SHAIRI: NIMEMPOSA JIRANI, TATIZO UMASIKINI

 

 Mwanzo ulioadhimu, napenda nikujuzeni
naanza kwa tabasamu, mawazo yatulizeni
lipo jambo maalumu, nataka nikwambieni
asalamu alaykumu, salamu yangu shikeni
 
leo tena sikieni, nilonalo pokeeni
musinichoke jamani, nateseka mawazoni
naumia akilini, ninaloswali moyoni
nimemposa jirani, tatizo umasikini
 
lipo jambo la muhimu, nimemposa jirani
kubwa lengo maalumu, tuwe pamoja mwandani
kwangu ni nyenzo adhimu, amefundisha manani
nimemposa jirani, tatizo umasikini
 
musinicheke wenzangu, yamenifika shingoni
mke kuwa mali yangu, wazazi hawatamani
nimetoa posa yangu, wameipiga pembeni
nimemposa jirani, tatizo umasikini
 
mawazo yangu mwanzoni, mganga kumuendea
sielewi na sioni, penzi limenikolea
najibu lake mwandani, subira kuendelea
nimemposa jirani, tatizo umasikini
 
tatizo umasikini, sina nyumba yenye bati
wazazi wake mwandani, wanataka nyingi noti
harusi ya ukumbini, vyombo meza na kabati
nimemposa jirani, tatizo umasikini
 
naumia akilini, mawazo yenu nipeni
nimemposa jirani, kwa uzuri pia dini
naumbo lake mwandani, limenikata maini
nimemposa jirani, tatizo umasikini
 
wazazi wao kauli, kipato changu kidogo
mtoto kenda skuli, pia bado dogodogo
mimi kunipa muhali, ameshakuja kigogo
nimemposa jirani, tatizo umasikini
 
wadau nimerejea, nahitaji ushauri
wengi katika dunia, ila yule ni mzuri
moyo umeweka doa, kwa vumba pia uturi
nimemposa jirani, wadau nifanye nini?

Post a Comment

0 Comments