ads

SHAIRI: CHUMVI

chumvi

Napatwa na mtihani, majibu sijui nini

Tafakari ya mwanzoni, chochote sijabaini

Moyoni ninayakini, jambo hili sio geni

Chumvi mimi masikini, sina thamani chunguni

Sina thamani chunguni, kwa chochote masikini

Nimekwepa mitihani, nafasi yangu mwishoni

Na kila ajae ndani, mimi nipo lawamani

Chumvi mimi masikini, sina thamani chunguni

Sendi mwenyewe chunguni, natupiwa lawamani

Nikizidi sana ndani, nazidishwa tafurani

Naambiwa hayawani, umezidi chakulani

Chumvi mimi masikini, sina thamani chunguni

Siku sawa sawiani, sitajwi hata kwanini

Akina giligilani, husifiwa kwa mizani

Na mimi sionekani, hata niwe mwema gani

Chumvi mimi masikini, sina thamani chunguni

Daima ni lawamani, sijulikani ni nani

Mpishi pia yundani, ninazidi matatani

Mpishi hana Imani, nitazidi muda gani

Chumvi mimi masikini, sina thamani chunguni

Ninafungiwa koponi, hata nje mi sioni

Nikitoka ni motoni, Maisha yangu chunguni

Nipatapo ahueni, natafunwa mdomoni

Chumvi mimi masikini, sina thamani chunguni

Naililia thamani, kamwe sina abadani

Daima nipo rehani, Maisha yangu chunguni

Nani anipe thamani, mpishi hama amani

Chumvi mimi masikini, sina thamani chunguni

Kaditama mtihani, swali bado li moyoni

Sijui yangu thamani, Maisha yangu chunguni

Sina hadhi duniani, kila siku mi mgeni

Chumvi mimi masikini, sina thamani chunguni

Mtunzi: Mwinyi Abdallah
Phone: 0655 895599
Email: mwinyiabdallah2012@gmail.com

Post a Comment

3 Comments

  1. Maashaa Allah shairbzuti.
    thamani ya chumvi ipo waaasp????

    ReplyDelete
    Replies
    1. Chumvi haionekani thamai yake

      Delete
    2. anaitafuta thamani yake haioni

      Delete