ads

UTENZI WA HARUSI -{FAUDHIA}

Bismillah Wadudi
Njema Sifa Maabudi
Kwa Mtume Ahmadi
Ujumbe Nawaletea.

Panasababu Adhimu
Kuitukuza Salamu
Mwanzo Wa Langu Jukumu
Asalamu Alaykumu.

Kikweli Imewadia
Siku Ilo Wavutia
Wengi Tulisubiria
Leo Imetufikia.

Siku Bora Kwa Manani
Kaisifu Rahmani
Wawili Kuwa Mwandani
Mwenendo Wake Nabia.

Karibuni Uwanjani
Karibuni Barazani
Karibuni Majirani
Pamoja Kusherekea.

Ninayo Mengi Moyoni
Nayasema Hadharani
Lengo Letu Uwanjani
Harusi Ya Faudhia.

Faudhia Katulia
Mtoto Hana Madoa
Tabasamu Lavutia
Ndoani Anaingia.

Vigelegele Kidogo
Tuifanye Haja Ndogo
Faudhia Si Mdogo
Mengi Ameyapitia.

Tumefurahi Nyoyoni
Furaha Iso Kifani
Leo Upo Darasani
Twakufunza Faudhia.

Ninalo Jambo Moyoni
Nalimwaga Uwanjani
Wageni Na Majirani
Sote Tupate Sikia.

Ndani Umeshaingia
Faudhia Zingatia
Ndoa Suna Ya Nabia
Leo Kwako Yatimia.

Faudhia Sikiliza
Si Kama Nakuchombeza
Ukweli Ninakufunza
Ndoa Ipate Tulia.

Mume Kwako Ni Mtoto
Ahitaji Lako Joto
Mpe Mapenzi Mazito
Kamwe Nje Kuwazia.

Mume Pia Umlishe
Bafuni Umuogeshe
Na Nguo Umvalishe
Kazini Akirejea.

Sifa Waridi Harufu
Waridi Pia Nadhifu
Faudhia Maradufu
Moyo Wake Umetua.

Mume Wako Mthamini
Mume Kwako Ndo Mwandani
Yanayojiri Chumbani
Kamwe Nje Kuyatoa.

Mume Ndio Bwana Wako
Paka Wanja Paka Piko
Mwili Wako Tikisiko
Nyumbani Atatulia.

Ukiadhimu Kutoka
Bora Ruhusa Kutaka
Ukiona Kaudhika
Rudi Na Kujikalia.

Mume Kwako Ndo Swahiba
Ndo Mpishi Wa Mahaba
Kwa Huzuni Pia Huba
Mume Kwake Vumilia.

Bashasha Kitu Kizuri
Chakuleta Kila Kheri
Ndio Sifa Ya Bashiri
Mtume Wetu Nabia.

Ndoa Dada Ni Matunzo
Ndio Twakupa Mafunzo
Wewe Kwako Ndio Mwanzo
Ndoa Wajibu Tulia.

Enyi Mulio Vijana
Waume Kwa Wasichana
Jamii Hushikamana
Wakioana Jamia.

Ndoa Funguo Ya Nyumba
Mke Pia Kujiremba
Mashairi Pia Imba
Mumeo Kumvutia.

Ung’arishe Uso Wako
Ung’arishe Mwili Wako
Ng’arisha Sauti Yako
Kamwe Mume Kukohoa.

Kila Ndege Mti Wake
Kakupenda Mwanamke
Zidisha Kwake Makeke
Moyoni Kujinasia.

Mume Jina Libadili
Kwako Awe Ni Khalili
Usimwite Kistuli
Moyoni Atachukia.

Mume Muite Mpenzi
Maridhia Laazizi
Mahabuba Kumuenzi
Wajibu Nakuambia.

Mume Muite Vizuri
Kwa Sauti Ya Hariri
Mambo Yaliyo Ya Siri
Subiri Akitulia.

Ataporudi Kazini
Msubiri Ukumbini
Mabusubusu Mwilini
Kabla Ya Kutulia.

Mume Ni Wako Muenzi
Kwa Kazi Mpe Pongezi
Zidisha Kwake Mapenzi
Nyumbani Akirejea.

Mpe Maneno Laini
Kwa Sauti Ilo Chini
Mkaribishe Chumbani
Chakula Kujipatia.

Da Fau Nakuambia
Da Fau Umesikia
Da Fau We Vumilia
Ndoani Umeingia.

Yako Mengine Ndoani
Da Fau Maliza Ndani
Usiende Kwa Jirani
Wivu Utakusumbua.

Cheko Lako Ni Mwanana
Usikae Kuuchuna
Mumeo Akikuona
Huzuni Utamtia.

Zungumza Kwa Kicheko
Uwapo Kwa Mume Wako
Lililo Moyoni Mwako
Bwana Hulisubiria.

Mengi Nimeyaongea
Ila Hapa Naishia
Hatari Inanijia
Musije Kuniachia.

Bibie Umesikia
Nasema Na Faudhia
Dada Ulietulia
Hongera Nakupatia.

Tunaagana Nyumbani
Tutakutana Mwakani
Apendapo Rahmani
Uzima Kutupatia.

Kwaherini Maharusi
Kwaheri Bibi Harusi
Kwaheri Wala Si Tusi
Moyoni Tumeridhia.

MTUNZI:     MWINYI ABDALLAH
              mwinyiabdallah2012@gmail.com
                         0655895599

Post a Comment

1 Comments