ads

UTENZI WA HARUSI: SADRA

 
 
UTENZI WA HARUSI: SADRA

Bismillah wadudi 
Mola wangu maabudi
Nashukuru sina budi 
Baraka kutujazia 

Neema pia baraka 
Kutoka kwako rabuka 
Twakuomba msifika 
Jambo letu kutimia 
 
Leo ni siku adhimu
Siku ya mashamshamu 
Nyoyo zina tele hamu
Sherehe twasherekea 

Karibuni uwanjani
Karibuni nyi wageni
Karibuni shughulini 
Sherehe imetimia 

Vigele gele kidogo 
Tuifanye haja ndogo 
Dada yetu si mdogo
Ndoani ameingia 

Ndoa ndio njema dira
Nakuasa dada sadra 
Ndoa ni njema bishara 
Maisha kuendelea 

Da sadra wangu mpenzi
Sikufundishi mapenzi 
Nakufundisha kuenzi 
Mume aweze tulia 

Mume kwako ndiye mwenza
Mume wako ni wakwanza 
Mume ukimchombeza
Ndoa yenu kutulia 

Ongeza tele makeke 
Mume wako umteke 
Thamani yako ya mke
Mume atakupatia

Kuna vitamu ndoani 
Ndoani sio ndotoni
Usicheke na jirani 
Usije ukajutia

Jipake poda uturi
Bashasha kitu kizuri
Sema na mume vizuri 
Itakuwa njema ndoa

Ataporudi kazini 
Mkaribishe chumbani 
Mpige busu laini 
Mume atakuridhia

Timiza wajibu wako 
Mume kwako ndiye wako
Usingoje ndugu zako
Mume atakukimbia 

Mume wako muogeshe 
Na nguo umvalishe 
Chakula pia mlishe 
Mahaba yatajazia

Ng'arisha sauti yako
Ung'arishe uso wako 
Paka wanja paka piko 
Da sadra ndani tulia

Mume ni wako da sadra
Yapunguze masihara
Ukali uwe wa nadra 
Ndoani utaenea 

Ndoa kamwe si ndoana 
Ndoa nikuelewana
Ndoa ni kushikamana 
Mapenzi yanaenea 

Tamati sijafikia 
Da sadra wetu tulia
Shukrani nazitoa 
Wote mupate sikia 

Nipo chini yako mama
Naogopa kusimama
Nisijevunja heshima 
Shukurani sana mama

Mama yangu shukurani 
Kwa mizani yangu duni 
Sinayo mengi kinywani 
Ninakupenda moyoni

Kando ya yote ni baba
Kwa mapenzi marhaba 
Nakushukuru si haba
Baba shukurani baba

Mapenzi niliyahisi 
Mama na baba kaisi 
Daima nitawamisi 
Maisha kuendelea

Niendelee kidogo 
Ni kwa mamie wadogo 
Hawa kwangu ni vigogo 
Makuzi walinilea 

Shukurani zilo aya
Mamie wangu jinaya 
Umepigania haya
Leo nami kutulia 

Mamie wangu bishara
Na khadija ndio dira 
Leo nimekuwa sadra
Shukurani nawambia

Bibi zangu wa daima
Wa kwanza bibi asma 
Bibi shungi hima hima
Nawapenda nyie sana

Nawashukuru kwa dhati 
Walioniweka kati 
Shukrani sio ati
Shukurani zilo dhati 

Shukurani dada nasra
Shukurani da munira
Nanyi kwa ndio dira 
Maisha kuyaendea 

Da bidawana salma 
Mmenifunza heshima
Kamwe sitokuwa nyuma
Shukurani nawambia

Dada mamu na bogozo 
Nyinyi kwangu muongozo
Pia ndio maliwazo
Ndoani nimeingia

Shukurani ka Hassani
Akhera na duniani
Nimefurahi moyoni 
Shukurani nakwambia

Shukurani  babu ally
Idirisa babu dully
Hekima zenu awali
Shukurani nawapeni 

Tamati nimefikia
Sina budi kuwambia
Kwaheri nawapatia 
Ndoani sasa nangia.


Mwinyi Abdallah 
O655895599

Post a Comment

0 Comments