ads

SHAIRI: USITUNASE URIMBO




Nataka kusema jambo. Naombeni umakini
Hatakama ni kwa wimbo, kuirudisha amani
Katu kuto kwenda kombo,tukaicha na dini
Usitunase urimbo, umoja wetu wa dini.

Kadhalika hili kadha, hasira ziko moyoni
Jambo dogo lenye adha, twashindwa kutua chini
Yapo tele mawaidha, naomba tushike dini
Tutaionja na ladha, akhera twende peponi.


Nani hapa asotaka, tuwe pamoja peponi 
Nyoyo ziso na mashaka, rasuli awe pembeni
Chochote unachotaka, anakupa rahmani
Dunia twahadaika, tutayakosa mageni.

Zuia chukizo lako, mbele yake ndugu yako
Hili leo pambazuko, musivifanye vituko
Tamati pumzi yako, ndipo tatizo liliko
Tamaa ziso mashiko, zinazima nuru yako.

Hii jamani ni dini,  wala sio kibatari
Ni nuru yake manani, haizimi kwa kiburi
Alipita firauni, mfano wetu misri
Na tusiivunje dini, mola wetu tusitiri.

Mazoea twazoea, utani sio wa dini
Na kama umekosea, basi omba samahani
Kwa mola wako tubia, asikutie motoni
Hasira zako zuia, hapa uwanja vitani.

Nyote nakupongezeni, munaounga amani
Anapenda rahmani, kuona hatukosani
Tusimfwate shetani, yeye kwanza maluuni
Mola akuongozeni, kwenye yenu mitihani.

Tamati nimefikia, ujumbe kuwapatia
Kila aliyesikia, ndiye mlengwa tambua
Ninamuomba jalia, na kazi kuyafanyia
Radhize kutupatia, na salama kuzidia.

MTUNZI:        Mwinyi abdallah
                         Mwinyiabdallah2012@gmail.com
                         0655895599


Post a Comment

0 Comments