ads

SHAIRI: NAZI

Hodi mbona siwaoni, Milango haipo wazi
Au mpo masokoni, Desturi ya Uswazi
Nabisha mpaka jikoni, Mada yangu leo nazi
Nazi kweli inapendwa, Kuikuna ina kazi

Ukitaka kutafuta, Sisumbuke nenda pwani
Kila kona tazikuta, Mjini na mashambani
Zilopangwa kwa matuta, Uchague hadharani
Nazi kweli inapendwa, Kuikuna ina kazi


Usiuziwe koroma, Ndani lenye ulaini
Linolia kama ngoma, Kiligonga kubaini
Iwe ngumu kama koma, Ndio nazi ya thamani
Nazi kweli inapendwa, Kuikuna ina kazi

Itikise usikize, Kama ndani ina maji
Ukishindwa uulize, Achague muuzaji
Mwambie akueleze, Mwenzio alokipaji
Nazi kweli inapendwa, Kuikuna ina kazi

Kifuo kiwe imara, Hakikisha hakiyumbi
Ukikite barabara, Nazi kuvua makumbi
Usije ukaparara, Kujipakaza mavumbi
Nazi kweli inapendwa, Kuikuna ina kazi

Utulie kwa makini, Kuivunja ni akili
Usiipige kwa chini, Kupasua kikatili
Itapoteza thamani, Sipogawa mara mbili
Nazi kweli inapendwa, Kuikuna ina kazi

Ina rangi ya nadhifu, Nyeupe iso na doa
Wala haina harufu, Ndani ukiitoboa
Imezungukwa na ndifu, Unopaswa kuzitoa
Nazi kweli inapendwa, Kuikuna ina kazi

Usidhani unaweza, Kuikuna ina kazi,
Makalini kuwekeza, Ukishaivunja nazi
Sikune kwa kulegeza, Vifuu vina uwazi
Nazi kweli inapendwa, Kuikuna ina kazi

Na iwapo wajaribu, Uliza wenye ujuzi
Ulekezwe taratibu, Ndipo usogeze mbuzi
Uikalie karibu, Usijiweke kipuzi
Nazi kweli inapendwa, Kuikuna ina kazi

Hakikisha sio mbata, Nazi ilo kuukuu
Kazana kuimata, Ukunapo chini-juu
Unaweza kujikata, Kikuponyoka kifuu
Nazi kweli inapendwa, Kuikuna ina kazi

Halafu kuna machicha, Uliyoyakusanyia
Kifumbuni kuyaficha, Lazima kushindilia
Kisha utayafikicha, Na tui kulikingia
Nazi kweli inapendwa, Kuikuna ina kazi

Kamua kikamavu, Kifumbu kuzungushia
Geuza kila ubavu, Tui kulikamulia
Yakeshakuwa makavu, Machicha yatupilia
Nazi kweli inapendwa, Kuikuna ina kazi

Nazi basi mkavune , Sikusudii kisomo
Burudika usinune, Siambe napiga domo
Kalia mbuzi ukune, Nimefikia kikomo
Nazi kweli inapendwa, Kuikuna ina kazi

Nimetunga kwa uchache,  Shairi laning’inia
Vina vyangu  ni vichache, Na beti zilofifia
Bora sasa niwaache, Nazi yanisubiria
Nazi kweli inapendwa, Kuikuna ina kazi

by: HAMZA A. MOHAMMED

Post a Comment

0 Comments