ads

SHAIRI: NASIKITIKA HADUMU, RAFIKI YANGU UJANA





Ujana kitu kitamu, tena ni azizi sana,
Maungoni mwangu humu, nilikuwa nao jana,
Kwa wingi katika damu, tahamaki leo sina!
Nasikitika hadumu, rafiki yangu ujana.

Kichwa kimejaa mvi, kinywani meno hamna,
Nikenda kama mlevi, miguu nguvu haina,
Kumbe ujana ni hivi, ukenda hauji tena!
Nasikitika hadumu, rafiki yangu ujana.

Jua langu limekuchwa, na nyota nilizoona,
Ukinitazama kichwa, nywele nyeusi hakina,
Kama zilizofikichwa, zikang’olewa mashina,
Nasikitika hadumu, rafiki yangu ujana.

Ntatizika kauli, midomo najitafuna,
Nimekusanya adili, walakini hali sina,
Dunia kitu bahili, hiki una kile huna!
Nasikitika hadumu, rafiki yangu ujana.

Nilikuwa ni waridi, furaha ya wasichana,
Neno hawakunirudi, wakati wa kukutana,
Sasa nanuka baridi, wanionapo waguna,
Nasikitika hadumu, rafiki yangu ujana.

Waliowakinibusu, walikuwa wengi sana,
Wanawake wenye busu, uzuri na usichana,
Sasa sina hata nusu, ya wanitajao jina,
Nasikitika hadumu, rafiki yangu ujana.

Wazuri wenye uturi, na mikono yenye hina,
Kila mtu mashuhuri, alipenda kuniona,
Nilifaa kwa shauri, na sasa suti sina!
Nasikitika hadumu, rafiki yangu ujana.

Dunia Bibi Arusi, kwa watu kila namna,
Inapendeza nafsi, wakati wa kuniona,
Na leo sina nafasi, kwa uzee kunibana,
Nasikitika hadumu, rafiki yangu ujana.

Kilichokuwa gizani, niliweza kukiona,
Nikakijua thamani, sura yake hata jina,
Sasa sijui ni nini, hata ikiwa mchana,
Nasikitika hudumu, rafiki yangu ujana.

Kilichotaka fikira, niliweza kukinena,
Kwa mfano na sura,. mpaka kikafanana,
Leo tazama hasara, nguvu hiyo sina tena!
Nasikitika hadumu, rafiki yangu ujana.

Kinachotaka mapimo, sikifahamu mapana,
Marefu yake na kimo, siifahamu bayana,
Nusu nimo nusu simo, duniani najiona,
Nasikitika hadumu, rafiki yangu ujana.

Hudum nasikitika, rafiki yangu ujana,
Machozi yamiminika, na la kutenda hapana,
Na wakati umefika, uzee dawa hauna,
Nasikitika hadumu, rafiki yangu ujana,

Hauna dawa uzee, mabega yamepetana.
Anionaye ni “Wee, ondoka hapa laana,”
Wanaposema na miye, niliyekuwa na jina!
Nasikitika hadumu, rafiki yangu ujana.

Wakatabahu shairi, uchungu wanitafuna,
Walakini nafikiri, twafuata subhana,
Katika ile amri, ya kuwa na kutengana,
Nasikitika hadumu, rafiki yangu ujana


©Shabaan Robert

Download here NASIKITIKAHADUMU, RAFIKI YANGU UJANA

Post a Comment

0 Comments