ads

SHAIRI: NIPENDE NIKUPENDAVYO





Sauti nainururi, swahibu nakuswabahi
Tabasamu desturi, kuchukia hujawahi
Mola wetu tusitiri, usiku na asubuhi
Utujazie mazuri, mapenzi tuyasabahi

Nakuita laazizi, itika kwa tabasamu
Hata kama unakazi, ishike yangu salamu
Mitihani kwetu ngazi, upoe na majukumu
Moyo wangu upo wazi, salamu yangu ni hamu

Maridhia samahani, uridhie moyo wangu
Nimekupenda zamani, ukawa jirani yangu
Kukutoa mawazoni, hilo jukumu ni langu
Kupenda boga mtini, maua wajibu wangu

Vumilia tabasamu, mimi ni wako swahibu
Ninakupenda hamumu, kama tunda ni zabibu
Salamu mashamshamu, mola atupe thawabu
Nakupenda mahamumu, kwako wangu sina tabu

Uzuri wa sura yako, mfanoe sijaona
Na umbo la mwili wako, atukuzwe maulana
Unipe na radhi zako, tukaishi wote janna
Niwapo karibu yako, nazidi furaha sana

Mpenzi nikupe siri, hujapata kuijua
Mume wangu we mzuri, idara zimetimia
Hakika wanisitiri, na madhila ya dunia
Nakupenda sio siri, sina budi kukwambia

Usichoke nihimize, niwe kwako mke bora
Haki kwako nitimize, kwa mola niwe mbora
Kwa marimba hata zeze, zikamilike ibara
Daima tutangulize, mazuri yetu akhera

Sina budi katamati, itue yangu salamu
Tuipange mikakati, tupate sote elimu
Mazuri tuweke kati, mapenzi yawe ya hamu
Mapenzi yangu ya dhati, nakupenda mahamumu

Mtunzi: Mwinyi Abdallah
Phone:  0655895599



Download here  SHAIRI: NIPENDE NIKUPENDAVYO

Post a Comment

7 Comments