ads

SHAIRI: MALENGO ENDELEVU


      Duru ninazialisha, hapa kule huku kile
Leo ninabainisha, mbeleni toka ya kale
Sera zilimakinisha, uhuru tujitawale
Kwa malengo endelevu, hayapati uchakavu

      Vyema tukaikalia, ardhi yenye rutuba
Uchafu tukiondoa, salama maji ni tiba
Jamii kuizindua, misitu kwetu haiba
Kwa malengo endelevu, hayapati uchakavu


     Uoto ukinawiri, ukijani ukatanda
Mbuga zetu mashuhuri, tutapata kuzilinda
Majanga yaso mazuri, daima kutotuwinda
Kwa malengo endelevu, hayapati uchakavu

      Maji safi na salama, nguvu kazi kutugea
Watoto baba na mama, daima kufurahia
Mashamba watayalima, mvua kujinyeshea
Kwa malengo endelevu, hayapati uchakavu

      Haki pia na amani, huleta uadilifu
Kwa watu pia kazini, nguvu kazi maradufu
Uhusiano jirani, viongozi wanadhifu
Kwa malengo endelevu, hayapati uchakavu

      Kipaumbele elimu, watu wapate elimu
Wapatikane walimu, wasimamie nidhamu
Wamsingi kwa awamu, yazidi mashamshamu
Kwa malengo endelevu, hayapati uchakavu

      Afya bora kila kona, vituo kote viwepo
Dawa pia ni amana, kila kituo ziwepo
Vijiji vingi hakuna, hima wahini walipo
Kwa malengo endelevu, hayapati uchakavu

      Viwanda tuvijengeni, tuvigawe kila kona
Mazingira boresheni, uoto kwetu dhamana
Na ajira zigaweni, wapate kazi vijana
Kwa malengo endelevu, hayapati uchakavu

      Malengo tumeyaweka, kwa malengo endelevu
Malenga nimeandika, hayapati uchakavu
Ardhi tukiishika, nishati kwetu angavu
Kwa malengo endelevu, hayapati uchakavu

          Tamati nimefikia, hima jama zingatia
Malengo yakitimia, tumepata bora njia
Vizazi vinofatia, vyema watayatumia
Kwa malengo endelevu, hayapati uchakavu


MTUNZI: MWINYI ABDALLAH
TEL: +255655895599
EMAIL: Mwinyiabdallah2012@gmail.com

Post a Comment

0 Comments