UTANGULIZI
Namshukuru m/mungu kwa kunineemesha neema
hii na kunipa umri hadi leo hii bado ninaendelea katika kuitetea dini ya Allah
(sw) ninamtakia ziada ya rehma mtume Muhammad (saw) na jamaa zake na waislam
wanaume na waislam wanawake
Baada ya kumshukuru Allah na kumtakia
ziada ya rehma mtume Muhammad (saw). Hakika Allah leo hii amenipa nguvu ya
kuwaelimisha waislam wenzangu juu ya suala zima la historia katika uislam na
pia leo hii nitaelezea juu ya vita vya kiislam alivyopingana mtume (saw) na
maswahaba zake na kuwapiga makuraishi ambavyo viliitwa vita vya badr
VITA
VYA BADR
Badr ni jina la mji uliopo kiasi cha
kilomita mia na hamsini(km150) mbali na mji wa madina na mahali hapo hapakuwa
na chochote isipokuwa bonde na kisima kilichokuwa milki ya mtu mmoja aitwae
Badr na kwa ajili hiyo mahala hapa pakaitwa badr, kwa vile vita hivyo
vilipiganwa mahali hapa ndiyo maana vikaitwa vita vya badr
Vita hivyo vilitokea asubuhi ya siku
ijumaa Ramadhani ya kumi na saba mwaka wa pili baada ya hijra (baada ya mtume
(saw) kuhamia madina)
SABABU
ZA VITA
Chanzo cha vita hivi kilikuwa ni msafara
wa biashara wa makafiri ukiongozwa na
abu sufyan uliokuwa ukitokea nchi ya sham (Syria) ukirudi makkah ukiwa
na watu wasiozidi Arobaini (40)
Msafara huu ulikuwa umebeba mali nyingi sana ya watu wa makkah na mtume
(saw) akaona hii ndiyo fursa nzuri ya kuipiga dola hiyo ya kikafiri kiuchumi,
kijeshi na kisiasa na pia kulipiza kisasi hasa kwa vile waislam walipohama
makkah kwenda madina makafiri waliwalazimisha kuziacha mali zao zote huko, na
kuondoka bila chochote isipokuwa nguo zao na wanyama wa kuwapanda hata hivyo
wengine walinyang’anywa wanyama wao na ikabidi kutembea kwa miguu mpaka madina
na wengine waliviziwa njiani na kuuliwa
Mtume(saw) pia akawaambia waislam”msafara huu wa
makurashi umejaa mali zao, uendeeni huenda Allah akatulipa haki zetu
walizotunyang’anya kwa kutuwezesha kuuteka”
Si watu wengi waliojitolea kwenda, na hii ni
kwa sababu mtume (saw) hakutia mkazo katika suala hili na akawaachia watu
wajitolee wenyewe bila ya kulazimishwa na kwa ajili hiyo maswahaba wachache tu
walimfuata
NGUVU YA JESHI LA KIISLAM
Mtume (saw) akaondoka na watu wapatao mia tatu na kigodo tu hivi,
inasemekana walikua mia tatu na kumi na tatu( 313) na riwaya nyengine zinasema
walikuwa mia tatu kumi na saba (317), themanini na sita (86) ni muhajirina na
mia mbili thelathini na moja (231) ni watu wa pale pale
Maswahaba hawakujuwa kuwa msafara huo utakuja kuwa ni moja ya mapambano
makubwa baina ya haki na batili walidhani kuwa yatakuwa yale mapambano ya
kawaida na wapiganaji wadogo wadogo tu na wala hawakujuwa kuwa Allah amekwisha
panga atimize jambo lililokuwa lazima litendeke, Waliondoka wakiwa na farasi
wawili tu, mmoja wa zubeir bin Awaam na mwengine wa mikidadi bin Al-Aswad
Al-kindly(ra) walikuwa pia na ngamia sabiini wakipokezana katika kuwapanda
Msafara wa Abu sufyan
Abu sufyan alikuwa kiongozi wa msafara wa biashara ya makafiri wa makkah
alikuwa ni mtu mwenye kuchukuwa tahadhari sana, alijuwa kuwa njia ya makkah ina
hatari nyingi na kwa ajili hiyo kila mara alikuwa akitanguliza wapelelezi ili
wamletee habari za mbele safari wakati huo huo alikuwa akimuuliza kila
anayekutana naye, iwapo huko alikotoka
ameona chochote kile kisichokuwa cha kawaida, katika kuuliza uliza
akamuuliza mtu mmoja aitwae Majdi bin Amru iwapo ameona jeshi kutoka mji wa
madina akasema “mimi sikuona majeshi lakini niliona kundi kubwa la watu
waliopumzisha ngamia wao mahali hapa”
Abu sufyan akaenda kupafanyia uchunguzi mahali pale alipoambiwa kuwa
watu walipumzisha ngamia wao, baada ya kuchambua kinyesi cha ngamia
waliopumzishwa mahali hapa na kuona kokwa za tende za ndani yake akasema”maadam
choo chao kimejaa kokwa za tende bila shaka yoyote kuwa hawa ni ngamia wa watu
madina“
Alipotambuwa hayo akajua kuwa anaviziwa na hapo hapo akageuza msafara na
kupita njia nyengine na akamtuma mtu mmoja aitwae Dhamdham bin Amru Al-Ghafariy
atngulie mbio sana aende akawazindue watu wa makkah juu ya hatari inayoukabili
msafara wao wenye vitu vya thamani kubwa sana, Watu wa makkah
walipoyasikia haya wakasema”Muhammad
anadhani kuwa atauteka msafara huu kwa urahisi kama alivyouteka msafara wa Amru
bin Al-hadhramy” akaendelea kusema “haitakuwa hivyo kabisa atakiona cha moto chake
Muhammad safari hii”
Jeshi la makafiri wa makkah
Makafiri mara baada ya kujulishwa juu ya hatari hiyo wakakusanya jeshi
la watu wapatao elfu moja na mia tatu (1300), farasi wapatao mia moja (100) na
ngamia wengi sana. Wakaondoka pamoja na vigogo vya makuraish na walisafiri kwa
kasi kubwa sana kuelekea kaskazini mahali ulipo mji wa badr,walipofika mji
uitwao Al-juhufa wakapata salamu kutoka kwa Abu sufyan kuwa umekwisha salimika
msafara wao na kuwataka warudi makkah
Abu jahal akasema haturudi mpaka tufike badr,
tukae hapo siku tatu tuchinje wanyama wetu, tunywe pombe zetu na waimbaji
waimbe mpaka habari zetu ziwafikie waarabu wote ili wapate kutujua ni nani sisi
na ili watuogope
Mtume (saw)ashauriana na sahaba zake
Kutokana na mabadiliko haya ya ghafla na ya hatari ilimbidi mtume(saw)
awaite wakuu wa jeshi la waislam ili
kuwajulisha juu ya hali ya mambo ilivyo na kutaka ushauri wao.
Ama wa kwanza wao ni Abu bakar (ra) akamuunga mkono mtume(saw) juu ya
kulazimika kwao kupigana na makafiri, kisha akasimama Umar (ra) naye akamuunga
mkono mtume kwa rai yake, kisha Amru (ra) akasema “Ewe mtume wa Allah nenda
kama alivyokuonyesha Allah na sisi tuko nyuma yako wallahi hatutakuambia kama
walivyo mwambia wana wa israili mtume wao Mussa(as); nenda wewe na mola wako
mkapigane nasisi tutakaa hapa tunawangojea; Bali tunakwambia nenda wewe na mola
wako na sisi pamoja nanyi tunapingana”. Baada ya maneno haya mtume (saw)
akasema”vyema”.
Kisha akawaombea dua wote watatu waliotoa rai zao kwa upande wa muhajirina na
kwa upande wa madina akasimama sa’ad bin mua’adh(ra) aliyekuwa mmoja wa
viongozi wa watu wa madina aksema “sisi tumekuamini na kukusadiki na
tukashuhudia kuwa uliyokuja nayo ndiyo ya haki na tukakupa ahadi zetu na neno
letu kuwa tutakusikiliza na kukutii kwa hiyo endelea tu kama unavyotaka kwani
wallahi kama utatutaka tuivuke bahari hii,ukaivuka basi tutaivuka pamoja nawe
na hapana hata mmoja kati yetu atakaebaki nyuma sisi hatuogopi kupambana na
adui kesho, sisi ni watu wenye kusubiri katika vita na wakweli katika mapambano
na inshaallah Allah atkuonyesha ndani yetu yale yatakayo kufurahisha macho
yako, kwa hiyo tuongoze kwa baraka za Allah”
Mtume (saw) akafurahishwa na maneno ya sa’ad (ra) akasema “nendeni na
nakupeni bishara njema, Allah ameniahidi moja wapo ya makundi mawili wallahi
kama kwamba ninaona wapi wataanguka kila mmoja kati ya maadui”
Majeshi ya kiislam yanafanya upelelezi
Walipowasili mahali panapoitwa
Addiya karibu na badr, mtume (saw) pamoja na swahiba yake wa pangoni Abu bakar
As-swidiq (ra) wakatoka na kuanza kufanya upelelezi nje ya kambi yao na katika
kutembea kwao, wakakutana na mzee mmoja wa kiarabu na kumuuliza juu ya habari
za jeshi la makuraishi na juu ya habari za jeshi la Muhammad (saw), ili asiweze
kumtambua ni katika kundi gani wao, Yule akamwabia”kabla sijakujibu niambieni
kwanza nyinyi mnatokea wapi?”. Mtume (saw) akamwabia “ukituambia nasi
tutakwambia” Yule
mtu akasema “nilisikia kuwa jeshi la Muhammad na swahiba zake lilitoka siku
kadhaa wa kadhaa, ikiwa habari hizi ni za kweli, basi leo watakuwa washafika
mahali kadhaa, akapataja mahali lilipojeshi la watu wa madina, na nimesikia
kuwa makuraysh wametoka siku kadhaa wa kadhaa na ikiwa maneno niliyoambiwa ni
kweli, basi leo watakuwa washafika mahali kadhaa wa kadhaa, akapataja mahali
lilipojeshi la watu wa makkah”
Baada ya kumaliza
maneno haya akawauliza “nyinyi mnatoka wapi?”. Mtume akamwambia “sisi tunatokana na
maji” kisha akaondoka. Yule mtu akawa anajiuliza “hawa wana
katika maji ya iraaq au maji gani?
Na ifahamike kuwa mtume hakusema uongo, kwani viumbe vyote vinatokana na
maji, Allah anasema “na tukafanya kwa maji kila kitu kilichohai”
(suratul anbiyaa aya 30)
Mchana wa siku
hiyo, mtume (saw) aliwatuma watu watatu kwenda kupeleleza juu ya habari za
jeshi la makuraishi nao ni Ally bin Abi Talib, Az-zuberybin Awaam na Sa’ad bin
Abi waqas(ra) walipokwenda penye visima vya badr wakawakuta watoto watatu
wanachota maji kwa ajili ya kuwapelekea jeshi la makuraishi, wakawateka na
kwenda nao kambini ili kuwauliza maswali, walipofika nao kambi, Mtume alikuwa
akiswali, kwa hiyo wao wakaanza kuwauliza mateka wao. Vijana hao wakasema
wametumwa na makuraishi ili kuwachotea maji, maswahaba walikasirishwa na jibu
hilo kwani wao walitamani wawe watu wa Abu sufyan. Wakawapiga wale vijana mpaka
wakasema kuwa wao ni watu wa Abu sufyan na si watu wa jeshi la makuraishi
Mtume baada ya kumaliza swala
akawaambia maswahaba”waliposema kweli mliwapiga na walipokudanganyeni mkawachilia,
walisema kweli wallahi kwani wao ni watu wa jeshi la makuraishi”.
Kisha mtume akawauliza wale vijana “nipeni habari za makuraishi ”, wakasema wapo katika ng’ambo ya bonde
lile la mbali, akawauliza “wako wangapi”. Wakasema” wengi”. Akawauliza mtume “idadi yao ngapi”,
wakasema hatujui. Akawauliza tena “wanachinja wanyama
wangapi kila siku”, wakasema wale vijana “siku nyingine
wanachinja ngamia tisa na siku nyingine kumi”. Mtume akasema kuwaambia maswahaba
(ra) ”idadi
yao ni baina ya watu mia tisa na elfu”
Mtume akawauliza tena wale vijana “nani katika vigogo vya makuraishi wamo miongoni mwao
”, wakasema “utbah na shaiba watoto wa Rabia, Abu Al-bakhtari bin hishaam,
Hakiym bin Hizaam, Naufil bin Khuwaliid, Al-Haarith Taimah, An-nadhar bin
haarith, Zaamah bin Aswad, Abu jahal bin hishaam na Umayyah bin khalaf”. Mtume
akasema kuwaambia maswahaba zake (ra) “makkah imekutupieni (imekuleteeni) vipande vya maini yao (vigogo
vyao na vipenzi vyao)”
KUTEREMKA KWA MVUA
Waislam wakasogea
mpaka wakakaribia bonde la karibu na mahali yalipopiga kambi makuraisha na
majeshi yao
Allah aliwateremshia waislam utulivu wakalala vizuri hata wengine
wakaota na kuamka wa kiwa na janaba, lakini mahali hapo hapakuwa na maji ya
kogea ili wapate kujitwaharisha na wala ya kunywa na shaitwani akaanza kuwatiya
wasiwasi “vipi mtapigana kesho wakati miili yenu haina twahara, vipi mtapigana
kesho wakati mna kiu……?”
Allah (sw) akawateremshia mvua iliyo wasaidia sana kwasababu kutokana na
mvua hiyo waliweza kujitwaharisha na kuondoa uchafu wa sheitwani na kuzipa
nguvu nyoyo zao na pia na pia yakawasaidia kuufanya mchanga chini yao uwe mgumu
ili waweze kutembea vizuri bila ya kuteleza wakati wa mapambano.Allah anasema “alipokufunikeni kwa
usingizi uwe ni uaminisho kutoka kwake na akakuteremshieni maji kutoka mbinguni
ili kukusafisheni kwayo na kukuondoleeni uchafu wa sheitwani na kuzipa nguvu
nyoyo zenu na kuitia imara miguu yenu” (suratul Anfaal:11)
Mtume (saw) akaliamrisha jeshi lake liondoke pale walipo haraka sana ili
wawahi kusogea mbele karibu na mahali yalipo maji ya mji wa badr, wakasogea
mpaka wakafika mwanzo wa visima vya maji ya badr na mtume (saw) akawamrisha
kupiga kambi hapo. Mmoja katika maswahaba aitwaye Al-khabaab bin Mundhir
akamuuliza mtume(saw) “Ewe mtume wa Allah mahala hapa tulipo simama Allah
amekuamrisha na hatuna haki ya kusonga mbele zaidi au katika hila za kivita tu
na rai yako mwenyewe?” Mtume (saw) akamwambia “Bali ni hila za kivita na rai yangu
mwenyewe” akasema Al-khabaab “Ewe mtume wa Allah mimi naona kuwa
hapa si makazi mazuri bora tusogee mbele mpaka mwisho wa visima vya badr
tuvizunguke kisha tujenge mahodhi tuyajaze maji kisha tupambane nao sisi tutakuwa
tunakunywa na wao wasipate kunywa”. Mtume (saw) akasema “rai uliotoa ni
nzuri”. Wakaondoka hapo na kusogea sehemu ya juu ya mahali
yalipo maji na usiku wakaanza kutengeneza mahodhi na kuyajaza maji
MAKAO MAKUU YA JESHI LA WAISLAM
Baada ya kumaliza kazi yao hiyo sa’ad bin
Mu’aadh (ra) akatoa rai nyengine pajengwe mahali patakapo kuwa makao makuu ya
jeshi lao ili waweze kujitayarisha na kuikabili hali ya hatari yoyote itakayo
tokea iwapo jeshi lao litashindwa katika vita hivyo akasema “Ewe mtume wa Allah unonaje kukujengea kipaa
mfano wa hema (Arshii), kisha tukakuwekea tayari wanyama wa kupanda kisha sisi
tutapambana na adui ikiwa Allah atatujaalia kuwashinda hayo ndiyo
tunayoyapenda, ama ikiwa kinyume na hivyo basi wewe utapanda wanyama wako na
utakwenda kujiunga na wenzetu tuliowaacha nyuma kwani hao tuliowaacha nyuma
mapenzi yao juu yako ni makubwa pia kama sisi wangelijuwa kuwa tunapambana na
adui basi wasingelirudi nyuma kabisa na wangelipigana jihadi pamoja nawe”. Mtume (saw) akamuombea kila la kheri kwa rai
yake hiyo, na waislam wakajenga mfano wa hema juu ya kilima sehemu ya kaskazini
ya uwanja wa mapambano, sehemu ambayo mtu anaweza kuviona vita bila tabu huku
vikipiganwa.
Usiku kabla ya mapambano, mtume (saw) alilipanga jeshi lake kisha akawa
anawaonesha maswahaba(ra) mahali watakapo kufa maadui mbali mbali kabla hata
vita havijaanza alikuwa akisema “hapa ataanguka Fulani, hapa atauliwa Fulani……”
Alipokuwa
akiwapanga watu wake, mtume (saw) alipita mbele ya Sawaad bin Aziya (ra)
akamgonga kwa nguvu tumboni kwake kwa bapa la mkuki na kumwambia “simama vizuri ewe
Sawad”. sawad(ra) akamwambia mtume “umeniumiza ewe mtume wa
Allah, na mola wako amekuleta kwa ajili ya kusimamisha haki na uadilifu, kwa
hiyo uniache na mimi nikulipizie katika mwili wako”. Mtume (saw) akalifunuwa
tumbo lake na kumwambia “ewe sawad jilipie kisasi chako”. Sawad
akalikumbatia tumbo la mtume huku akilibusu, mtume (saw) akamwambia “kipi
kilichokupeleka ukafanya hivi?”. Akasema sawad “Ewe mtume wa Allah mambo
ndivyo kama unavyo yaona na mimi nilipenda tendo langu la mwisho kabla sijafa
liwe ni kuugusa mwili wako”. Mtume (saw) akamuombea dua nzuri.
Baada ya kuwapanga watu wake sawa na kuwataka wasianze kupigana mpaka
atoe amri yake, akawaambia maswahaba “wakianza kuja anzeni kuwarushia mishale na msitoe panga zenu
mpaka wawe karibu nanyi kabisa”
JESHI LA WATU WA MAKKAH
Usiku ule baadhi ya makuraishi waijaribu kutaka kunywa maji penye
mahodhi wliyoyajenga waislam kalini kila aliyejaribu kuyasogelea aliuliwa
isipokuwa mtu mmoja aitwae Haakim bin Hizaam huyu aliachwa na alisilimu na
baadaye akawa muislam mwema
Makuraysh waimtuma Umair bin Wahaab Al-jahamiy aende kuchunguza nguvu za
jeshi la waislam, akawa anazunguka jeshi hilo akiwa juu ya farasi wake, huku na
kule kisha akarudi kwa wenzake na kuwaambia “jeshi lao ni kiasi cha watu mia
tatu na zaidi kidogo, lakini naona kesho balaa litakuwa kubwa sana, kwani watu
hawa hawana pakukimbilia na hawana cha kupoteza, wanajuwa kuwa wao watauliwa
tu, hawana isipokuwa panga zao tu, na nyuma yao jangwa tupu kwa hiyo inaelekea
watapigana kwa ushujaa zaidi na hawatokubali mmoja wao auliwe bila ya yeye naye
kuuwa mtu mmoja kati yenu, kwa hiyo tizameni wenyewe”. Pakatokea mzozo mkubwa
baina ya makuraysh, wengi wao wakamtaka Abu jahal arudi na jeshi lake makkah na
kwamba hapakuwa na haja ya kupigana na jeshi la Muhammad (saw), lakini Abu
jahal kwa haraka akafanikiwa kuuzima moto huo na kumlaumu Umair kwa kumwambia
“umeingiwa na khofu wewe ulipouona uso wa Muhammad, pale ulipokuwa ukichunguza
majeshi yake ndiyo sababu ukaja na uwoga na unataka kututia na sisi uwoga huo”.
Akaweza kuwaingiza watu wake mori wa vita kwa kuwa kumbusha kuuliwa kwa Amru
bin Al-hadhramy na kwamba lazima walipize kisasi
MAJESHI YANAPAMBANA
Asubuhi ya siku ijumaa tarehe kumi na saba
mwezi wa ramadhani, mwaka wa pili baada ya hijrah, majeshi hayo mawili
yakapambana. Allah (sw) aliwafanya waislam walione jeshi la makafiri kuwa ni
wachache ili wasiogope na akawafanya makafiri wawaone waislam pia kuwa ni
wachache ili wasiwaogope na kurudi nyuma, yote haya ili kutendeke kile
anachokitaka Allah (sw)
Kwa kawaida kabla ya kuanza mapambano, waarabu walikuwa na tabia ya
kuanzisha mubaraza, na maana yake ni mtu mmoja au wawili au watatu hutoka
kutoka katika kila upande na kuanza kupambana wao kwanza, kila mmoja na
mwenzake mpaka wauwane, kisha vita ndiyo vinaanza. Mapigano haya kwa kawaida
ndiyo yanayotoa picha ndogo ya mwisho wa vita
Katika mapigano haya mtume (saw) aliwatoa upande wa waislam Ali bin Abi
Talib, Ubaidah bin Haarith na Hamza (ra). Kwa upande wa makafiri wakatoka Utbah
na ndugu yake Shaibah na Al-waliid motto wa Utbah. Wote wakiwa watu wa aina
mmoja katika mapigano haya, Hamza alimuuwa mpinzani wake Shaibah na Ali (ra)
alimuuwa mpinzani wake Al-waliid bila tabu na bila ya kuchukuwa muda mrefu, ama
Ubaidah (ra) yeye na mpinzani wake wote waliumizana wakaanguka chini lakini Ali
na Hamza wakawahi kumrukia Utbah na kumuuwa kisha wakamuokowa mwenzao na
kumvuta nyuma na kumrudisha katika kambi ya waislam. Lakini hatimaye kutokana
na damu nyingi iliyomwagika alifariki dunia siku nne baada ya tukio la badr kwa
homa ya manjano.
MASHAMBULIO
Majeshi yalipoanza
kupambana mtume(saw) akaingia ndani ya lile hema yeye na Abu bakar (ra) peke
yao na hapana mwengine aliyeingia humo, Mtume(saw) akaanza kuomba dua huku akisema “mola wangu
hawa makuraishi wamekuja kwa jeuri na kiburi chao, wakikupinga na kumkadhibisha
mtume wako, mola wangu nitimizie yale uliyoniahidi, mola wangu watu hawa
wakishindwa leo, basi hautaabudiwa tena……” kila vita vikipamba moto, naye huongeza
kuomba dua, akawa anaendelea kuomba mpaka nguo yake ya begani ikamwanguka na
Abu bakar (ra) akaiokota na kumvisha tena huku akimwambia “inatosha ewe mtume
wa Allah ushamuomba vya kutosha mola wako”. Kisha mtume(saw) akasimama penye
mlango wa hema aliyojengewa akawa anaisoma aya ya 45 ya suratul Qamar “Wingi wao huo
karibuni watashindwa na wataendeshwa mbio na watageuza migongo”
Mapigano haya yalimaanisha mwisho mbaya wa jeshi la washirikina kwa
sababu wamepoteza watatu katika wapiganaji wao wakubwa kwa mpigo mmoja, kwa
ajili hiyo wakawavamia waislam kwa ghadhabu na kwa nguvu zao zote na waislam
wakapambana nao kwa ujasiri mkubwa kabisa.
Wakati huo mtume (saw) akawatokea waislam na kuwaambia “Naapa kwa
Yule ambaye nafsi ya Muhammad (saw) ipo
mikononi pake, yeyote atakayepigana nao leo, kisha akauliwa akiwa katika hali
ya kusubiri (subra) bila ya kurudi nyuma basi Allah atamuingiza peponi”.
Umair bin Al-hamaam (ra) aliyekuwa akila tende, mara baada ya kusikia maneno
hayo akasema “Hivyo baina yangu na baina ya kuingia peponi ni kupigana na
kuuliwa na watu hawa na tende hii ndiyo inayonicherewasha” akazitupa tende zake
akaingia vitani akapigana mpaka akauliwa
Mtume (saw) akasogea mbele akachota gao la mchango, akawakabili
makuraishi kisha akasema “zimeangamia nyuso zao”. Allah anasema “hamkuuwa nyinyi Allah ndiye aliyewauwa na wewe hukutupa
pale ulipatupa, walakini Allah ndiye aliyetupa ili awajaribu waumini majaribio
mema yatokayo kwake hakika Allah ndiye
msikizi na mjuzi ndiyo hivyo na hakika Allah ni mwenye kudhoofisha vitimbi vya
makafiri” (suratul Anfaal:17-18).
Kisha mtume (saw) akawaambia swahaba zake (ra) “wakazieni vizuri,
inukeni muifuate pepo ambayo upana wake tu ni sawa na mbingu na ardhi”
kisha akaondoka na kurudi katika hema lile alilojengewa. Mapambano makali
yakaanza baina ya makundi mawili hayo, na ushindi ukawa wa waislam, wakauliwa
waliouliwa katika vigogo vya makuraishi na wakatekwa waliotekwa, haya ni
mapambano ya pekee ambayo malaika walishiriki, akiwemo jibril(as). Baadhi ya
maswahaba walisema “siku hiyo tulikuwa tunaona vichwa tu na kuruka huku na
kule, hatujuwi nani anayevikata”
KIFO CHA ABU JAHAL
Abu jahal alipoona majeshi yake yanaanza kurudi nyuma akawa anapiga
kelele huku akisema “wasikutisheni hao,msiogope kwa kuwa Utbah na Al-waliid
wameuliwa, leo hatuondoki hapa mpaka turudi nao makkah tukiwa tumewafunga kamba
wote hawa”
Anasema Abdulrahman bin Auf kuwa
“nilipokuwa nimesimama vitani nikageuka kutizama kuliani kwangu na kushotoni
nikidhani watakuwepo watu wazima ili tusaidiane vita vikipamba moto, lakini
nikavunjika moyo nilipowaona watoto wawili wadogo wamesimama mmoja kushotoni
pangu na mwengine kuliani pangu, nikasema moyoni mwangu “leo sina pakuegemea”,
Yule mtoto aliye kuliani pangu akaiomba niiname apate kuniuliza ili yule
mwenzake asisikie. Akaniuliza “Ami! Yupi kati yao Abu jahal?” nikamuuliza “Ewe mwana wa ndugu yangu
unamtakia nini Abu jahal?” Akanijibu “nimemsikia kuwa anamtukana mtume wa
Allah, wallahi nikimuona basi sitomwacha, lazima nitamuuwa”, Yule mtoto aliye
kushotoni pangu akaniuliza vilevile kama mwenzake na nikamjibu kama mwenzake na
akasema yale yale aliyosema mwenzake; nilipomuona Abu jahal nikawaambia “Yule
rafiki yenu mnayemtafuta”, Wakamkimbilia na panga zao wakamvamia na kumpiga kwa
mapanga mpaka wakamuuwa
Mara baada ya kumuuwa wakakimbia mpaka kwa mtume (saw) na kumpa habari
njema hizo, mtume (saw) akawauliza “yupi kati yenu aliyemuuwa”. Kila mmoja akasema “mimi ndiye
niliyemuuwa”. Mtume (saw) akawaambia “hebu nione panga zenu”. Baada ya kuzitazama akasema “kweli, nyote
mmeshirikiana katika kumuuwa”. Kisha akasema “Allahu laailaaha illa huwa”
mara tatu, kisha akasema “Allhamdu lillahi lladhiy swadaq wa’adah wa naswara
abdahu,wahazamal-ahazaba wah-dahu”
Katikavita hivi waliuliwa makuraishi sabiin (70) na wengine sabiin(70)
walitekwa, na katika waliouliwa alikuwemo firauni wa umma huu; Abu jahal na
utbah bin Rabia na mwanawe Al-waliid na nduguye Shaiba na wengine wengi, na
miongoni mwa mateka alikuwemo; Abbas (ami yake mtume {saw}) na Aqiyl bin Abi
Talib na Nawfal bin Al-Haarith na Umayya bin khalaf na wengine wengi, hawa wote
walikuwa upande wa makuraishi
MIZOGA YA MAKAFIRI
Baada ya vita
kumalizika, waislam wakawazika wenzao waliokufa mashahidi na idadi yao walikuwa
kumi na nne {14}, kisha wakaichukuwa mizoga ya mushirikina na kuitupa katika
kisima kisichokuwa na maji kilicho karibu na mahali palipotokea mapambano hayo.
Usiku wa manane waislam walimsikia mtume(saw) akiwa amesimama penye kile
kisima walichotupa mizoga ya mushirikina akiwafokea huku akisema “Enyi mlio
kisimani, ubaya ulioje mliokuwa nao jamaa zangu nyinyi kwa mtume wenu!,
mlinikadhibisha wakanisadiki watu (wakweli), mkanitoa katika mji wangu,
wakanipokea watu (wakweli), mkanipiga vita wakanisaidia watu (wakweli), je!
Sasa nyinyi mmekwisha pata kweli yale aliyo kuahidini mola wenu? Ama mimi
nimepata yale aliyoniahidi mola wangu”
Maswahaba wakamuuliza mtume(saw) “Ewe mtume wa Allah unazugumza na watu
washakuwa mizoga”, mtume (saw) akasema “Wao wanasikia kuliko nyinyi haya niliyowaambia isipokuwa hawawezi
kujibu”
BISHARA NJEMA
Mtume (saw) aliwatuma watu kwa haraka sana waende madiynah ili kuwapa
habari njema hizo za ushindi wao juuu ya makafiri, Usamah bin zayd (ra) anasema
“zilitufika habari tulipokuwa tukimzika bibi Ruqayya (ra) bint wa mtume (saw),
mke wa Uthamin bin Affan (ra); Zayd bin harithah (ra) alipoingia msikitini watu
walimzunguka huku akisema kwa furaha “Amekwisha uliwa Utbah bin Rabia na
shaibah bin Rabia na Abu jahal…..” akawa anawataja mmoja mmoja katika vigogo
vya makuraishi waliouliwa Badr
Zayd bin Harithah (ra) anasema “nikamuuliza babangu unasema kweli?”
akanijibu “Naam, kweli mwanangu”
KUONDOKA MJI WA BADR
Mtume (saw)
akaondoka hapo badr pamoja na mateka wao na ngawira zao na alipofika karibu na
madinah alisimamisha msafara katika bonde la safra akawagawia waislam ngawira
yao sawa sawa na kila anapoukaribia mji wa madinah, alikuta makundi kwa makundi
ya watu waliosimama pembezoni mwa njia wakimpongeza.
Allah anasema “kumbukeni pale mlipokuwa nyinyi kwenye ng’ambo ya karibu ya
bonde,na wao wakawa ng’ambo ya mbali, na msafara ulipokuwa chini yenu. Na
ingeli kuwa mmeagana mngeli khitalifiana katika miadi. Lakini (mkakutana) ili
Allah atimize jambo liliokuwa lazima litendeke kwa sababu, aangamie wa
kuangamia kwa dalili zilizo dhahiri, na asalimike wa kusalimika kwa dalili
zilizo dhahiri, na Allah ni mwenye kusikia mwenye kujua, kumbuka alipo
kuonyesha usingizini mwako kwamba wao ni wachache na lau angeli kuonyesha kuwa
ni wengi, mngeli ingiwa na woga, na mngeli zozana katika jambo hilo, lakini
Allah kakuvueni, hakika yeye ni mwenye kuyajua yalio vifuani”
HITIMISHO
Ama tumshukuru Allah kwa kutujaalia sisi na mtume wetu kupata ushindi
dhidi ya makafiri na hii ndiyo ilikuwa vita ya kwanza kupigana na makafiri,
Allah awalipe kila la kheri wote wanao isimamisha dini yake katika njia ya
haki, na pia mshairi anasema juu ya neema za Allah (sw)
Umeniumba insani, mwanadamu alo huru
Ukanipa Qur-an, ili iwe yangu nuru
Sasa nina kheri gani, kama sijakushukuru
Kwa nini nisikupende, nawe umenikirimu
Ama mpaka kufikia hapa hatuna budi kumshukura
Allah kwa kutujaalia kuliendeleza jahazi hili la uislam kwa kujulishana habari
zilizopita za uislam kuhusiana na historia ya vita vya kiislam ambavyo ni vita
vya badr . pia endelea kusoma vitini hivi na hiki kikiwa ni sehemu ya kwanza na
sehemu ya pili inafuata ambayo
itahusu historia ya vita vya Uhud , INSHAALLAH.
Wabillah tawfiq
0 Comments