Yasita sita salamu,
Yasita sita kwa zamu,
Ninaitoa kwa hamu,
Salamu alaykumu.
Kikubwa nina wajuzaa,
Siko radhi kunyamaza,
Kipi kinachotukwaza,
Nakuomba sikiliza.
Mengi tunajifanyia,
Mabaya yamezagaa,
Kikomo kinafikia,
Dunia kuendelea.
Sasa nakukumbusheni,
Chamsingi duniani,
Dunia ni gerezani,
Toba toa kwa manani.
Toba toa kwa manani,
Makosani tumo ndani,
Toba ni kwa rahmani,
Mabaya tuepukeni.
Toba tuikumbukeni,
Na swala tuzidisheni,
Na aibu tuoneni,
Twapotea duniani.
Giza tumeliingia,
Giza linatuzidia,
Nuru inatukimbia,
Dunia kuangazia,
Katuahidi manani,
Mengi yaso na kifani,
Twamwabudu duniani,
Akhera sote peponi.
Sharti lake jalia,
Binadamu katugea,
Kosa tukilikosea,
Toba vema kuitoa
Toba bora kutubia,
Madhambi kujifutia,
Adhabu hutapitia
Toba akiiridhia.
Toba itoe moyoni,
Usitangaze jirani,
Sio tu msikitini,
Hata ukiwa njiani.
Tubia mapema sasa,
Nyoyo ipige msasa,
Nafsi kuitakasa,
Jiepushe na anasa.
Toba msingi jamani,
Toba bora duniani,
Toba haina kifani,
Toba msingi moyoni.
Machozi yanakutoka,
Machozi yabubujika,
Na sisi tumeumbika,
Neema zimekatika.
Maasi yamesambaa,
Vimini dada wavaa,
Kusengenya kumejaa,
Kila kona ya mtaa.
Mauti twachekelea,
Huzuni twaziondoa,
Stori twasimulia,
Bila woga twaongea.
Yakumbukeni moyoni,
Nayasema si utani,
Tukumbukeni manani,
Akhera iko mbeleni.
Toba ndo itatufaa,
Dunia yatuhadaa,
Toba hebu kimbilia,
Lilia kwake jalia.
Yote ninawakumbusha,
Kiama jama chatisha,
Mola ataturudisha,
Malipo kuthibitisha.
Ndugu ninawaombeni,
Mikono tuinueni,
Dua tuitikieni,
AMINI na tusemeni.
Rahmani ya rahimu,
Ya lainishe magumu,
Na yote yaso muhimu,
Tuepushe na haramu.
Iondoe migongano,
Udumishe muungano,
Uislamu pambano,
Pamoja mshikamano.
Tusamehe yarahimu,
Tukirimu ya karimu,
Tuzidishie elimu,
Manufaa toa humu.
Tamati salamu zetu,
Juu ya mtume wetu,
Ni twaha kipenzi chetu,
Kiongozi juu yetu.
Jamii zingatieni,
Toba sio mtihani,
Nikuubia moyoni,
Turejee kwa manani.
Mtunzi: Mwinyi abdallah
(0655895599)
Email: mwinyiabdallah2012@gmail.com
0 Comments