ads

SHAIRI: AISHA HUYU AISHA GANI?




 1
Natuma zangu salamu, ndugu zangu islamu
Enyi ninyi wanadamu, poleni na majukumu
Asalamu alaykum, muitikie kwa hamu
Waalaykum salamu, muitiko wake salamu

2
Wote muno nisikia, ndugu yenu niswalini
Tena ninafikiria, jibu wala silioni
Bila shaka munajua, tafakari akilini
Jibu nalisubiria, naombeni nijibuni

 3
Utata nauanzisha, naombeni tulieni
Tuna wengi bi aisha, waumini siwaoni
Ndo mfumo wa maisha, jibu wala silioni
Mrithi wa bi aisha, mimi wala simuoni

4
Bi aisha alitisha, kwa sifa ziso kifani
Hekima namaanisha, nyote mwajua jamani
Alikuwa akikesha, anamuomba manani
Sasa ni wengi aisha, wanakesha ukumbini

5
Alijihifadhi ndani, tena alijaa wivu
Sasa wengi mitaani, tena wengi ni wavivu
Hawajitulizi ndani, watakosa toka shavu
Waume zao jamani, watapata utulivu

6
Kiukweli siamini, naumia akilini
Kuwa nasi waumini, aisha nguo kimini
ukweli tafakarini, najibu nipatieni
Aisha huyu jamani, yu sawa na wazamani

7
Bi aisha wa zamani, ni mama wa waumini
Naombeni tulieni, aisha sasa wahuni
Tena na tafakarini, napindisha kichwa chini
Aisha huyu aisha gani, majibu nipatieni

Mtunzi: Mwinyi Abdallah 
                (0655895599)
Email: mwinyiabdallah2012@gmail.com

Post a Comment

0 Comments