ads

SHAIRI: ALBINO



1.
Amkeni amkeni, mawio yametufika
Amkeni tambueni, nje kumepambazuka
Waungwana duniani, pamoja kuelimika
Albino ni jirani, sawia tumeumbika

2.
Sawia tumeumbika, dira ninaangazia
Ametuumba rabuka, umbile lilotulia
Sawa tumemithilika, kasoro amezitoa
Albino ni jirani, sawia tumeumbika
3.
Nani anaetambua, yeye amekamilika
Kiumbo pia tabia, wenziwe kukasoreka
Simama tupatejua, tuanze na kukucheka
Albino ni jirani, sawia tumeumbika

 4.
Maji chura ayataka, ya moto sio sawia
Njia fupi mwaitaka, mali kujimilikia
Dunia inakucheka. Haya kutojionea
Albino ni jirani, sawia tumeumbika

5.
Wazee wale wa kale, machache waliyanena
Zitafika zama zile, kutokuwa waungwana
Kelele hapa na pale, watu kutwa kuuwana
Albino ni jirani, sawia tumeumbika

6.
Albino tu sawia, sijaona tofauti
Imani zilizodoa, wanahaha kwa mauti
Jamii yawazuia, kupaza zao sauti
Albino ni jirani, sawia tumeumbika

7.
Ninakupeni ujumbe, vyema kuuzingatia
Tuwalindeni viumbe, kwa huruma na sawia
Hata shairi tuimbe, jamii kuizindua
Albino ni jirani, sawia tumeumbika

MTUNZI: Mwinyi Abdallah
                    0655895599
Email: mwinyiabdallah2012@gmail.com

Post a Comment

0 Comments