Bismillahir-Rahmaanir-Raheem.Alhamdulillah
Rabbil'alamiin. Subhana Allaahi rabbil'arshil adheem. Hakika sifa njema zote ni za Allaah سبحانه وتعالى
tunamsifu na tunamuomba msaada na tuna muomba maghfira. Na tunamuomba
atuhifadhi na shari za nafsi zetu, na maovu ya matendo yetu.
Anaemuongoza Allaah سبحانه وتعالى hapana wakumpoteza na Anaempoteza hapana wa kumuongoza. Nakiri kwamba hapana apasae kuabudiwa illa Allaah سبحانه وتعالى,
hali ya kuwa peke yake, hana mshirika, na ninakiri kwamba Muhammad ni
mja wake na ni Mtume wake. Mwenyeezi Mungu amrehemu na awarehemu jamaa
zake na masahaba zake na wanaofuata hao kwa wema mpaka siku ya malipo
na amsalimishe kwa amani nyingi.
Napenda nishirikiane nanyinyi kisa cha safari yangu kufikia Uislamu dini ya asili iliyo safi na ya haki kabisa Aliyotuletea Mola wetu kutuongoza katika njia iliyonyooka kufuata kitabu chake na Mtume wake wa mwisho.
KABLA YA UISILAMU
Jamii, malezi na dini yangu
Nimezaliwa India
katika jamii ya Sikh (Singa Singa). Nimekulia katika malezi ya mzazi
mmoja tu ambaye ni mama yangu, baba yangu alitangulia zamani kuja Canada
akituacha mimi na mama yangu na mdogo wangu wa kike. Watu katika
mujtamaa wangu ni watu washupavu, tabia zao nyingi ni mbaya na za
uwongo, za kuhadaiana. Na matajiri ndio zaidi wenye tabia hizo, maskini
ni mtu wa kupuuzwa na kudharauliwa, na hakuna kuwaonea huruma wala
kuwasaidia, bali wanazidi kuwa katika hali hiyo.
Mama yangu alikuwa mkali sana
na mshupavu. Alipata tabu kutulea kuhakikisha tunapata elimu nzuri
pamoja na mafunzo mazito ya dini yetu ya Ki Singa Singa. Mzunguko wa
maisha yangu yalikuwa ya kidhiki kwa kukosa mapenzi ya wazazi wawili,
kwa hiyo sikuwa katika hali nzuri ya kisiha ya akili, kimwili hata
ikawa imeniathiri hisia zangu.
Nimesomeshwa
katika shule bora kabisa ya dini yetu na mafundisho niliyopewa kuhusu
mungu ni kuwa tuamini kwamba haifai kumuwaza mungu kwa kufuata akili za
binaadamu, yaani hakuna nafasi ya hoja au busara katika jambo hilo. Nakumbuka nilivyokuwa nikiwaza kuhusu mbingu na ardhi na nilivyozaliwa na kuwaza moyoni, "kama
vyote hivyo vimeumbwa, bila ya shaka kuna muumbaji wa hivi vyote.”
Nikimuuliza mama yangu, hakuwa ananipa jibu lolote bali kuniambia
niamini tu na kukubali mafunzo ya dini yetu. Nikifundishwa kuwa
kuwasiliana na mungu ni kuepukana na njia za kutafakari sana huku nikiamini kuwa mungu mmoja hasa yupo na ninaweza kuzungumza nae na kwamba ananisikia.
Fikra zangu zilivyopanuka
Nilipotimia miaka 13 familia yangu ikaja kuishi Canada
kuwa pamoja na baba yangu. Ghafula nikajikuta kwenye mawingu ya
mabadiliko ya maadili . Ikanichukua muda kujisawazisha. Maisha
yangu nyumbani yalikuwa ya kubanwa kabisa wakikhofu wazazi wangu
nisibadilike kuingia katika maadili na kuathirika na tamaduni za nchi
hii. Nilipoingia chuo kikuu nikajihisi huru kidogo na ndipo nikaanza
kuwaza vile nilivyo kuwa nahisi undani mwangu. Nilisoma masomo ya
Biology, Chemistry na Physics nikitaka niwe Engineer, ili tu
niwafurahishe wazazi wangu waliokosa mtoto wa kiume, kwani hiyo ilikuwa
ni tamanio lao kubwa na baba yangu hakunipa mapenzi yale anayostahiki
baba kumpa mwanawe. Na tamanio hili lilikuwa likiwavunja moyo katika
mujtamaa wetu kuwa hawana mtoto wa kiume bila ya kufikiri kuwa hayo ni
makadirio ya Mungu.
Nilipokuwa
naingia ndani kabisa katika masomo ya Biology na kuelimika elimu ya
mwili wa binaadamu, nilikuwa nikiwaza uzuri, ufundi, ustadi na uhodari
wa maumbile haya, kwamba kila sehemu ya mwili ina kazi yake maalumu na
zote zinafanya kazi barabara kabisa kumuezesha binaadamu aishi. Je!
Ni nani huyo aliyetengeneza mjengo huu wa mwili? Yuko wapi? Akili
yangu ikawa inanizunguka sana!!
Nikitazama mbingu na ardhi, jua, mwezi, mimea, wanyama na bahari,
almuradi nilitembea mbali kwa mawazo na kuwaza mjenzi wa hayo yote bila
ya kumjua ni nani, huku sina raha kabisa na hamu kubwa imenishika
nimtambue.
Ibada
na ada yangu zikaanza kuwa hazina muhimu akilini mwangu, nikaanza
kuzikataa ndani ya moyo wangu kwanza. Nikaanza kuwaza sababu ya maisha
yetu binaadamu. Nikahisi kuwa kuna kitu kilichopunguka katika kufahamu
kwangu kuhusu maisha. Vipi Muumba wa binaadamu na dunia yote
hakujijulisha kwetu?
Kuumwa kwangu
Ikaendelea hivyo mpaka siku za Spring 2002, nikaanza kuumwa. Sikuwa na wasiwasi sana nikajua kuwa nitapona tu na kila kitu kitarudi kama
mwanzo. Lakini haikuwa hivyo, nilizidi kuumwa mpaka nikafikia katika
hali ya kukata tamaa ya maisha, niliona ndio basi nakufa, hakuna wa
kunisaidia, sio daktari wala mama, wala ndugu wala rafiki, wote
hawakuweza kunifaa hata mimi mwenyewe sikuweza kujisadia lolote.
Niliyatamani hayo mauti na kupendelea bora nife kuliko kuadhibika na
mateso hayo ya maumivu. Nikawa najiuliza, "Kama mungu anadhibiti mambo yote ya watu vipi ananitesa hivi? Kama kweli yupo mbona haniponyeshi na wazee wangu wanamuomba?
Nikatambua
kuwa uzuri wangu, uhodari wangu, ujeuri na kiburi changu, vyote
nilokuwa navyo vikawa vinayayuka, sina tena hayo, kwani faida gani kuwa
nayo hayo na hayanifai kitu katika hali hii? Maumivu makali, mateso,
dhiki ya roho, kuchanganyikwa akili kulinipeleka kuwa katika kiza,
nikawa sioni sisikii, nimo matesoni tu na tamaa ya kuishi inazidi
kupotea.
Kuzungmza na Mungu na kusikia kuhusu Uislamu
Kwa
mara ya kwanza nikaanza kuzungumza na Mungu na kumuomba, bali kumuomba
msamaha na kusema, "Ewe Mungu kama kweli upo, na nafikiri kweli upo,
basi nisamehe, nisaidie na nionyeshe njia, na nijulishe sababu ya maisha
na ukweli wake”. Baada ya haya, kidogo nikahisi raha fulani imepenya
katika moyo wangu.
Siku
ya pili yake nilikuwa natizama T.V., walikuwa wakionyesha kisa cha mtu
aliyesilimu. Nilipendezewa na mabadiliko aliyopata huyo mtu baada ya
kuingia katika Uislamu, zaidi katika utakaso, ukweli, uaminifu,
udhalilifu wake yalikuwa ni mambo ya tunu kabisa. Alikiri huyo mtu
kuwa Uislamu ndio uliomfanya kupata sifa hizo. Nikasema moyoni "Lazima
niitafute hii dini ya Kiislamu niisome niijue ikoje? Waislamu
wanaamini nini kuhusu Mungu? Hili ni wazo kubwa muhimu nililotaka kujua
jibu lake.
Nikaanza
kutafuta katika internet kuhusu Uislamu nikasoma Tauhiid na iliniingia
moja kwa moja akilini na kuikubali, maana niliona yote yaliosemwa
yalikuwa ya hikma na yenye kuleta maana kabisa. Zaidi kilichonivutia ni
kukazaniwa neno la " Laa Ilaaha Illa Allaah” nikawa nawaza haya sana
bila ya kiasi. Nikaanza kujifundisha tabia za Kiislamu nikapendezewa
kuona sifa nzuri nzuri na mafundisho yake. Nikawaza sasa, "Je vipi
kuamini kwao kuhusu akhera? Wanaamini nini baada ya mtu kufa?”
Nikaanza kusoma tafsiir ya Qur’an nikatambua kuwa kweli haya ni maneno
ya Mungu hasa niliyekuwa namtafuta. Ni kitabu cha mwisho,
kilichokamilika na risala na uongofu wa Muumba uliomo humo, haukuwa na
shaka ulikuwa wa wazi kabisa na wa kuridhisha. Huku nikipata nafuu ya
maumivu.
Mama
yangu akawa anaona tofauti yangu ya siha na pia akaona mabadiliko ya
tamaa yangu, na kuwa ipo furaha fulani inayoonekana katika uso wangu.
Nikawa namuonyesha maneno ya Allaah akawa anayapokea vizuri na
kukubaliana na mimi (huku sijui matokeo yake yatakuwa nini baada kuingia
Uislamu). Qur'an ikanizidisha kuwaza dalili za Mungu zikawa
zinakubaliana kabisa na mawazo yangu ya mwanzo hasa nikipitia katika aya
kama hizi:
إِنَّ
فِي خَلْقِ السَّمَاوَاتِ وَالأَرْضِ وَاخْتِلاَفِ اللَّيْلِ وَالنَّهَارِ
وَالْفُلْكِ الَّتِي تَجْرِي فِي الْبَحْرِ بِمَا يَنفَعُ النَّاسَ وَمَا
أَنزَلَ اللّهُ مِنَ السَّمَاءِ مِن مَّاء فَأَحْيَا بِهِ الأرْضَ بَعْدَ
مَوْتِهَا وَبَثَّ فِيهَا مِن كُلِّ دَآبَّةٍ وَتَصْرِيفِ الرِّيَاحِ
وَالسَّحَابِ الْمُسَخِّرِ بَيْنَ السَّمَاء وَالأَرْضِ لآيَاتٍ لِّقَوْمٍ
يَعْقِلُونَ
{Hakika
katika kuumbwa kwa mbingu na ardhi, na kukhitalifiana usiku na mchana,
na marikebu ambazo hupita baharini kwa viwafaavyo watu, na maji anayo
yateremsha Mwenyezi Mungu kutoka mbinguni, na kwa hayo akaihuisha ardhi
baada ya kufa kwake, na akaeneza humo kila aina ya wanyama; na katika
mabadiliko ya pepo, na mawingu yanayo amrishwa kupita baina ya mbingu na
ardhi, bila shaka zimo Ishara kwa watu wanao zingatia} Al Baqara 2.164
Nikazidi
kujua aya zinazoelezea maumbile ya ulimwengu na binaadamu, elimu ambayo
imejulikana na binaadamu baada ya miaka ya utafiti wa elimu ya sayansi.
أَوَلَمْ
يَرَ الَّذِينَ كَفَرُوا أَنَّ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ كَانَتَا
رَتْقاً فَفَتَقْنَاهُمَا وَجَعَلْنَا مِنَ الْمَاء كُلَّ شَيْءٍ حَيٍّ
أَفَلَا يُؤْمِنُونَ
{Je!
Hao walio kufuru hawakuona kwamba mbingu na ardhi zilikuwa
zimeambatana, kisha Sisi tukazibabandua? Na tukajaalia kwa maji kila
kilicho hai? Basi je, hawaamini?} Anbiyaa 21:30
ثُمَّ
اسْتَوَى إِلَى السَّمَاء وَهِيَ دُخَانٌ فَقَالَ لَهَا وَلِلْأَرْضِ
اِئْتِيَا طَوْعاً أَوْ كَرْهاً قَالَتَا أَتَيْنَا طَائِعِينَ
{Kisha
akazielekea mbingu, na zilikuwa moshi, akaziambia hizo na ardhi:
Njooni, kwa khiari au kwa nguvu! Vyote viwili vikasema: Tumekuja nasi ni
wat'iifu} Ha Meem Fussilaat 41:11
وَالسَّمَاء بَنَيْنَاهَا بِأَيْدٍ وَإِنَّا لَمُوسِعُونَ
{Na mbingu tumezifanya kwa nguvu na uwezo na hakika Sisi bila ya shaka ndio twenye uwezo wa kuzitanua} Adhariyaat 51:47
وَاللَّهُ
خَلَقَ كُلَّ دَابَّةٍ مِن مَّاء فَمِنْهُم مَّن يَمْشِي عَلَى بَطْنِهِ
وَمِنْهُم مَّن يَمْشِي عَلَى رِجْلَيْنِ وَمِنْهُم مَّن يَمْشِي عَلَى
أَرْبَعٍ يَخْلُقُ اللَّهُ مَا يَشَاءُ إِنَّ اللَّهَ عَلَى كُلِّ شَيْءٍ
قَدِيرٌ
{Na Mwenyezi Mungu ameumba kila kinyama kutokana na maji. Wengine katika wao huenda kwa matumbo yao,
na wengine huenda kwa miguu miwili, na wengine huenda kwa miguu mine.
Mwenyezi Mungu huumba ayatakayo. Hakika Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kila
kitu.} An-Nuur 24:45
Haya hayawezi kuwa ni maneno ya binaadamu. Nikaamini
kabisa maneno haya kuwa hakika ni maneno ya pekee ya Muumba. Sasa
vipi basi binaadamu wote hawatambui haya? Vipi hawamtambui Mungu wao
Aliyewaumba? Nikazidi kupitia aya kama hizi zinazotaja kuhusu Mungu Muumba, na kuzidi kutumainika na dini ya Kiislamu.
قُلْ
مَن يَرْزُقُكُم مِّنَ السَّمَاءِ وَالأَرْضِ أَمَّن يَمْلِكُ السَّمْعَ
والأَبْصَارَ وَمَن يُخْرِجُ الْحَيَّ مِنَ الْمَيِّتِ وَيُخْرِجُ
الْمَيَّتَ مِنَ الْحَيِّ وَمَن يُدَبِّرُ الأَمْرَ فَسَيَقُولُونَ اللّهُ
فَقُلْ أَفَلاَ تَتَّقُونَ
{Sema:
Ni nani anaye kuruzukuni kutoka mbinguni na kwenye ardhi? Au ni nani
anaye miliki kusikia na kuona? Na nani amtoaye hai kutoka maiti, na
akamtoa maiti kutoka aliye hai? Na nani anaye yadabiri mambo yote?
Watasema: Allah, Mwenyezi Mungu. Basi sema: Je! Hamchi? }
فَذَلِكُمُ اللّهُ رَبُّكُمُ الْحَقُّ فَمَاذَا بَعْدَ الْحَقِّ إِلاَّ الضَّلاَلُ فَأَنَّى تُصْرَفُونَ
[Basi
huyo ndiye Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wenu wa haki. Na kipo kitu gani
baada ya haki, isipokuwa upotovu tu? Basi huwaje mkageuzwa?}
كَذَلِكَ حَقَّتْ كَلِمَتُ رَبِّكَ عَلَى الَّذِينَ فَسَقُواْ أَنَّهُمْ لاَ يُؤْمِنُونَ
{Ndio kama hivyo kauli ya Mola wako Mlezi itakavyo wathibitikia wale walio potoka, ya kwamba hawatoamini.}
قُلْ
هَلْ مِن شُرَكَآئِكُم مَّن يَبْدَأُ الْخَلْقَ ثُمَّ يُعِيدُهُ قُلِ
اللّهُ يَبْدَأُ الْخَلْقَ ثُمَّ يُعِيدُهُ فَأَنَّى تُؤْفَكُونَ
{Sema:
Je! Yupo katika miungu yenu ya ushirikina aliye anzisha kuumba viumbe,
na kisha akavirejesha? Huwaje, basi, mkadanganywa?]
قُلْ
هَلْ مِن شُرَكَآئِكُم مَّن يَهْدِي إِلَى الْحَقِّ قُلِ اللّهُ يَهْدِي
لِلْحَقِّ أَفَمَن يَهْدِي إِلَى الْحَقِّ أَحَقُّ أَن يُتَّبَعَ أَمَّن
لاَّ يَهِدِّيَ إِلاَّ أَن يُهْدَى فَمَا لَكُمْ كَيْفَ تَحْكُمُونَ
{Sema:
Je! Yupo katika miungu yenu ya ushirikina anaye ongoa kwendea Haki?
Sema: Mwenyezi Mungu anaongoa kwendea Haki. Basi, je, anaye stahiki
kufuatwa ni yule Mwenye kuongoa kwendea Haki au asiye ongoa ila aongozwe
yeye? Basi nyinyi mna nini? Mnahukumu namna gani?}Yunus 10: 31 – 35
Huu
ndio uongofu niliokuwa nautafuta! Furaha ikanizidi ya moyo na kujihisi
mwepesi kabisa. Qur'aan hii haikunionyesha uongofu tu, bali
imenionyesha uvumbuzi wa matatizo ya binaadamu akiwa pekee au akiwa
pamoja na familia yake au akiwa na mujtamaa wake (jamaa) .
Imemuonyesha wazi binaadamu wajibu wake, haki yake na jukumu lake katika
madaraka yake. Imempangia maisha katika mambo ya mahitajio yake, tabia
na matendo yake katika jamii kwa njia iliyo ya hikma na ya heshima
kabisa.
Qur'ani
imefundisha binaadamu vipi kujiepusha na matamanio ya nafsi yaliyo kuwa
ya mazowea katika nyoyo za binaadamu mwanamme na mwanamke.
وَقُل
لِّلْمُؤْمِنَاتِ يَغْضُضْنَ مِنْ أَبْصَارِهِنَّ وَيَحْفَظْنَ
فُرُوجَهُنَّ وَلَا يُبْدِينَ زِينَتَهُنَّ إِلَّا مَا ظَهَرَ مِنْهَا
وَلْيَضْرِبْنَ بِخُمُرِهِنَّ عَلَى جُيُوبِهِنَّ وَلَا يُبْدِينَ
زِينَتَهُنَّ إِلَّا لِبُعُولَتِهِنَّ أَوْ آبَائِهِنَّ أَوْ آبَاء
بُعُولَتِهِنَّ أَوْ أَبْنَائِهِنَّ أَوْ أَبْنَاء بُعُولَتِهِنَّ أَوْ
إِخْوَانِهِنَّ أَوْ بَنِي إِخْوَانِهِنَّ أَوْ بَنِي أَخَوَاتِهِنَّ أَوْ
نِسَائِهِنَّ أَوْ مَا مَلَكَتْ أَيْمَانُهُنَّ أَوِ التَّابِعِينَ غَيْرِ
أُوْلِي الْإِرْبَةِ مِنَ الرِّجَالِ أَوِ الطِّفْلِ الَّذِينَ لَمْ
يَظْهَرُوا عَلَى عَوْرَاتِ النِّسَاء وَلَا يَضْرِبْنَ بِأَرْجُلِهِنَّ
لِيُعْلَمَ مَا يُخْفِينَ مِن زِينَتِهِنَّ وَتُوبُوا إِلَى اللَّهِ
جَمِيعاً أَيُّهَا الْمُؤْمِنُونَ لَعَلَّكُمْ تُفْلِحُونَ
{Na waambie Waumini wanawake wainamishe macho yao,
na wazilinde tupu zao, wala wasionyeshe uzuri wao isipo kuwa unao
dhihirika. Na waangushe shungi zao juu ya vifua vyao, wala wasionyeshe
uzuri wao ila kwa waume zao, au baba zao, au baba wa waume zao, au
watoto wao, au watoto wa waume zao, au kaka zao, au wana wa kaka zao, au
wana wa dada zao, au wanawake wenzao, au iliyo wamiliki mikono yao ya
kuume, au wafwasi wanaume wasio na matamanio, au watoto ambao hawajajua
mambo yaliyo khusu uke. Wala wasipige chini miguu yao ili yajuulikane mapambo waliyo yaficha. Na tubuni nyote kwa Mwenyezi Mungu, enyi Waumini, ili mpate kufanikiwa} An Nuur 24: 31
يَا
أَيُّهَا النَّبِيُّ قُل لِّأَزْوَاجِكَ وَبَنَاتِكَ وَنِسَاء
الْمُؤْمِنِينَ يُدْنِينَ عَلَيْهِنَّ مِن جَلَابِيبِهِنَّ ذَلِكَ أَدْنَى
أَن يُعْرَفْنَ فَلَا يُؤْذَيْنَ وَكَانَ اللَّهُ غَفُوراً رَّحِيماً
{Ewe
Nabii! Waambie wake zako, na binti zako, na wake za Waumini
wajiteremshie nguo zao. Hivyo ni karibu zaidi kuweza kutambulikana
wasiudhiwe. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu.} Ahzaab 33:59
Qur'aan imempa haki mwanamke kwa kulinganisha na uumbile lake na
hali kadhalika mwanamme. Uislamu ni mpango mkamilifu na njia ya maisha
bora kabisa ya kumfaa binaadamu kumuongoza katika mwangaza,
kumtoharisha na maovu, na kumtoa katika kiza na kumuweka katika heshima
anayostahiki, nimetambua kuwa ni hiari yake mtu kufuata haki au
kuikanusha.
وَلَا
تَزِرُ وَازِرَةٌ وِزْرَ أُخْرَى وَإِن تَدْعُ مُثْقَلَةٌ إِلَى حِمْلِهَا
لَا يُحْمَلْ مِنْهُ شَيْءٌ وَلَوْ كَانَ ذَا قُرْبَى إِنَّمَا تُنذِرُ
الَّذِينَ يَخْشَوْنَ رَبَّهُم بِالغَيْبِ وَأَقَامُوا الصَّلَاةَ وَمَن
تَزَكَّى فَإِنَّمَا يَتَزَكَّى لِنَفْسِهِ وَإِلَى اللَّهِ الْمَصِيرُ
وَمَا يَسْتَوِي الْأَعْمَى وَالْبَصِيرُ
وَلَا الظُّلُمَاتُ وَلَا النُّورُ
وَلَا الظِّلُّ وَلَا الْحَرُورُ
وَمَا يَسْتَوِي الْأَحْيَاء وَلَا الْأَمْوَاتُ إِنَّ اللَّهَ يُسْمِعُ مَن يَشَاءُ وَمَا أَنتَ بِمُسْمِعٍ مَّن فِي الْقُبُورِ
{Na
mbebaji habebi mzigo wa mwingine. Na aliye topewa na mzigo wake akiomba
uchukuliwe hautachukuliwa hata kidogo, na angamwomba jamaa yake. Hakika
wewe unawaonya wale wanao mcha Mola wao Mlezi kwa ghaibu, na wanashika
Sala. Na anaye jitakasa, basi anajitakasa kwa ajili ya nafsi yake. Na
marejeo ni kwa Mwenyezi Mungu }
{Na kipofu na mwenye kuona hawalingani.}
{Wala giza na mwangaza}
{Wala kivuli na joto}
{Wala
hawalingani walio hai na maiti. Hakika Mwenyezi Mungu humsikilizisha
amtakaye. Wala wewe si wa kuwasikilizisha walio makaburini.} Fatir 35: 18 -22
أَوَ
مَن كَانَ مَيْتاً فَأَحْيَيْنَاهُ وَجَعَلْنَا لَهُ نُوراً يَمْشِي بِهِ
فِي النَّاسِ كَمَن مَّثَلُهُ فِي الظُّلُمَاتِ لَيْسَ بِخَارِجٍ مِّنْهَا
كَذَلِكَ زُيِّنَ لِلْكَافِرِينَ مَا كَانُواْ يَعْمَلُونَ
{Je, aliye kuwa maiti kisha tukamhuisha, na tukamjaalia nuru inakwenda naye mbele za watu, mfano wake ni kama aliyoko gizani akawa hata hawezi kutoka humo? Kama hivyo makafiri wamepambiwa waliyo kuwa wakiyafanya} An-Aam 6:122
Kuchukua Shahada (kuingia Uislamu)
Aya
zote hizo na nyingine nyingi zikanifanya nikubali Uislamu ndani ya moyo
wangu japokuwa sijakiri Shahada. Nikaamua sasa nikatafute Muislamu
anipe shahada. Nani atakaenipa? Wapi? Nikachukua kitabu cha simu
kutafuta duka la vitabu vya KiiIslamu. Nikapiga simu duka moja
nikafunga safari kulifuata, nalo ni mbali na kwetu. Kufika nikajidai
kwanza kutizama vitabu kisha kumuuliza mwenye duka kuhusu Uislamu na
vipi kuingia katika dini hii, akanifahamu kuwa nataka kuchukua shahada.
Akaniuliza, "Je ndugu unataka kuchukua shahada hivi sasa?" Machozi ya
furaha yakanitoka na kumuitikia, hapo hapo nikakiri shahada, "Ash-hadu An-Laa Ilaaha Illa Allaah Wa Ash-hadu Anna Muhammadan Rasulu Allaah.”
Furaha
ilioje moyoni mwangu, nilijihisi ni mtu mwingine kabisa. Nikarudi
nyumbani huku natabasamu, furaha ikidhihirika usoni mwangu. Zikapita
siku nikawa najifunza kuswali na kuibia kuswali kwani niliogopa wazazi
wasijue, ambao nimekuja kujua kuwa jamii yetu ni maadui wakubwa wa
Uislamu. Nikaendelea kuficha, lakini mama yangu alikuwa hana raha
kuniona kutwa niko kwenye internet nikisoma mambo ya Kiislamu, mwisho
ikabidi nimwambie. Kwa vile aliniona kuwa nimekuwa mtu mwenye furaha,
na bado sijapona vizuri, ikawa kama kuumwa kwangu ni usalama wa kuingia dini hii. Kama
kwamba nikimsoma mawazo yake mama yangu anasema, "Si kitu madamu
unapata nafuu ya maradhi yako na madamu una furaha basi, lakini
naichukia hiyo dini,” kwani alikwisha niambia kuwa utatutia aibu kubwa
katika jamii yetu, tutakuwa na uso gani mbele ya jamaa zetu?
Ikawa
kila siku ni masuali hayo hayo, na habari zikawafikia jamaa zangu wa ki
Singa Singa ambao hawakunyamaza, bali waliwaita wazazi wangu na
kuwataka watoke katika aibu hiyo. Wazee wangu hawakuweza kunilazimisha
kwani walihofu nisirudie hali yangu ya kuumwa. Subhana Allaah! Nikawa
nasema moyoni kila kitu kina kheri yake, kuumwa kwangu kumekuwa kheri
kwangu kwamba wazazi wangu wananistahmilia kubadili dini yangu ingawa
wanaichukia . Ukhasama ukawa baina ya jamii yangu na wazazi wangu.
Wakaukata uhusiano kabisa, na wachache tu ndio waliobakia kuwa na aila
yangu. Jeuri, kiburi na chuki ya dini ya Kiislamu ndio sababu ya ari yao hiyo.
Nikaanza
kwenda msikitini nikajuana na wanawake wengi walionipokea kwa mapenzi
na undugu wa dhati wa Kiislamu. Nikajulishwa na mwalimu wa Qur'ani
nikawa nakwenda kwake kusoma. Mwalimu huyo ni kama mama yangu, dada
yangu, rafiki yangu, nikashikana naye sana,
alikuwa akinisaidia kwa kila aina ya njia ya kuimarisha dini yangu.
Nikajifunza namna ya kusoma Qur'aani (Qaida) na Alhamdulillah nikaweza
kusoma na kuijua vizuri vile inavyopasa.
Baada
ya siku chache kuanza kujifunza Qur'ani, nilimuota bibi yangu mzaa mama
ambaye tokea kufariki kwake miaka mingi sikupata kumuota. Nilimuota
anafuraha na huku anamkumbatia mwalimu wangu. Ndoto ilikuwa ya wazi
kabisa hata niliamka usingizini na kupigwa na bumbuwazi! Ni ndoto au ni
kweli? Ni ndoto! Ndoto ya kweli! Bibi yangu amefurahi mimi kuingia
katika uislamu! Bibi yangu ananijulisha kuwa niko katika njia ya haki.
Jambo la mwanzo nilipoamka nikamuelezea mama yangu ambaye naye
alishangaa, lakini akanipuuza kwa vile hakutaka niiamini hii dini
yangu.
Wazee
wangu wakawa wanatia shaka na mimi kutoka kwangu kwingi kuhudhuria
darasa, mikutano ya dini, na hata mara nyingine wakinitumia mtu
kunifuata kuniona nakwenda wapi. Ajabu ni kwamba nilipokuwa natoka
kwenda disco, na sinema na kurudi usiku hapo mwanzoni walikuwa
hawaniambii kitu. Lakini nnapokwenda kusoma dini na kurudi mapema
nyumbani kuweko chumbani kwangu wakiniambia, "mbona kutwa uko chumbani
hutoki?” Maajabu!!
Nikaendelea hivyo hivyo na huku nikizidi kupata nafuu ingawa sikupona kabisa, lakini Alhamdulillah namshukuru Allaah سبحانه وتعالى
Kunifikisha hapa nilipofikia kwa Kuniongoza, Kunitoa katika kiza na
Kunitia katika mwangaza. Na ndio maana nimejibadilisha jina langu
kujiita 'Nuur' badili ya Rimmie. Alhamdulillah, neema zote ni Zake
Mola wa Mbingu na Ardhi namuomba Allaah سبحانه وتعالى Azidi Kuithibitisha imani yangu na Anijaaliye miongoni mwa watu wema mpaka nitakapokutana Naye.
Amiin.
Maelezo zaidi kutoka kwa mwalimu wake Nuur
Aliponipigia
simu Nuur kwa mara ya kwanza kutaka kusoma Qur'ani, na nilipojua kuwa
katoka katika jamii ya Singa Singa, kwanza mwili ulinisisimka, maana
niliona wengi wao wanaobadili ni kutoka dini ya Ukristo na kutoka jamii
nyingine lakini sijapatapo kuona kutoka jamii hii. Nilikuwa na hamu
kubwa ya siku tulioagana ifike. Nikachungulia dirishani kumsubiri
wakati anakuja na nilipomuona, Subhana Allaah, msichana mwenye uzuri wa
kupendeza kabisa, mpole, na juu ya hayo nimeona ajabu ya akili yake
aliyomjaalia Allaah سبحانه وتعال.
Alikuwa akihudhuria mara mbili tu kwa wiki, kila mara akitumia saa moja
na nusu, akisoma masomo mawili au matatu kwa mara moja, kisha baada
ya siku ya pili yake akirudi amekwishajifunza vizuri, hata ameweza
kumaliza kujifunza kusoma Qaida ya Qur'aan kwa muda wa miezi miwili na
nusu tu! Kisha akawa anaendelea kusoma sura mpaka akafikia karibu
kumaliza juzuu ya Amma nzima. Maajabu ni kwamba hata matamshi yake ya
kiarabu yalikuwa kama mtu aliyezaliwa nayo lugha ya Kiarabu. Na hawa ndio wale Allaah سبحانه وتعالى Kawataja kuwa 'Ulul-Al-baab" yaani "Watu wenye akili.” (Ya kutafakari )
Siku
ya harusi yake iliofanywa msikitini, alipendeza sana, na ajabu ni
kuwa hakujipamba mapambo yeyote, si wanja, wala podari wala si rangi ya
mdomo, lakini alikuwa ananġaa kwa uzuri na ucheshi, Nuru ya kweli
ilikuwa ikinġara usoni mwake. Mama yake alikuwa akilia sana. Nikamwambia "Nuur! mama yako analia sana"
Akanijibu "ewe dada yangu, huonii kuwa analia machozi ya kusikitika
kwamba siku ya leo hakutegemea kumuozesha mwanawe msikiti wa Waislamu?
na siyo machozi ya furaha wakati mimi nna furaha ya kupata dini ya
haki? Basi mwache alie tu, machozi hayo kwangu hayana thamani,
namuomba tu Allaah سبحانه وتعالى Amuongoze na yeye".
Hivi
sasa Nuru anasoma masomo ya Sheria ya Kiislamu, aliniambia kuwa anataka
kujua lugha ya Kiarabu vizuri ili aweze kufanya daawa katika jamii yake
ya Kipanjabi.
Kwa
vile ni nadra kuingia katika Uislamu mtu kutoka kwenye jamii hiyo na
kwa jinsi ilivyothibitika imani yake huyu msichana, nimependa kukiita
kisa chake "Wardi katika msitu" "A rose in the forest".
FROM: www.alhidaaya.com
0 Comments