ads

KUOSHA MAITI


KUOSHA MAITI



HUKMU YAKE:
Maulamaa wanasema kuwa hukmu ya kuosha maiti ni 'fardhi kifaya', na maana yake ni kuwa;
"ikiwa baadhi ya watu wataifanya kazi hiyo, basi waliobaki wale wanaolazimika watasameheka".

MAITI GANI WANAOWAJIBIKA KUOSHWA?
Ni wajibu kuosha maiti wote wa kiislam isipokuwa wale waliouliwa na makafiri katika vita vya Jihadi.

HUKMU YA KUOSHA SEHEMU YA MWILI WA MAITI
Maulamaa wamekhitalifiana juu ya hukmu ya kuosha sehemu za mwili wa maiti ikiwa haukupatikana mwili wote kamili.
Katika madhehebu ya Imam Shafi na Imam Ahmed bin Hanbal, wao wanaona kuwa sehemu hiyo ioshwe na kukafiniwa na kusaliwa.
Anasema Imam Shafi;
"Tumejulishwa kuwa ndege mmoja ulimwanguka mkono wa mtu mjini Maka wakati wa vita vya ngamia (Waqaat al jamal), wakaujuwa mkono wa nani kutokana na pete, wakauosha na kuusalia".
(Mkono huo ulikuwa wa Abdurahman bin Utaab bin Usayd(RA)).
Anasema Imam Ahmed;
"Abu Ayub (RA) aliwahi kuusalia mguu, na Omar bin Khatab (RA) aliwahi kuyasalia mafupa, na Ibni Hazam anasema kuwa; Ikipatikana sehemu yoyote ile ya maiti ya Muislam, basi inasaliwa na kukafiniwa isipokuwa kama sehemu hizo ni za maiti aliyekufa shahid katika vita vya Jihad. Na anayesali anatia nia sawa na nia ya kumsalia maiti aliyekamilika mwili wake.
Ama Maimam Abu Hanifa na Malik wao wanasema;
"Ukipatikana mwili zaidi ya nusu, hapo unakoshwa na kusaliwa, ama sivyo hapana haja ya kuoshwa wala kusaliwa".

ALIYEKUFA SHAHID HAOSHWI

Shahid aliyeuliwa vitani na makafiri, haoshwi hata kama alipokufa alikuwa na janaba, kama Mtume (SAW) alivyofanya juu ya Handhalah (RA) aliyeuliwa vitani akiwa na janaba, Mtume (SAW) alimzika bila kumuosha.
Anasema Sayed Sabeq, katika Fiqhi ssunah kuwa:
Shahidi anakafiniwa kwa ngou zake zile zile alozivaa ikiwa zitatosha kumkafinia, kama hazikumtosha, basi anakamilishiwa nguo nyengine, na zinapunguzwa zikizidi kupindukia, na anazikwa na damu yake bila kuoshwa.
Imepokelewa kuwa Mtume (SAW) amesema;
"Msiwakoshe, kwa sababu kila jeraha (au kila damu) litanukia harufu ya miski siku ya Kiama".
Ahmed
Anasema Imam Shafi;
"Huenda ikawa sababu ya kutooshwa maiti na kutosaliwa ni kwa ajili ya kukutana na Mola wao wakiwa na majeraha yao, kwani imepokelewa katika hadithi kuwa damu zao zitanukia harufu ya hal miski.

MASHAHIDI WANAOOSHWA NA KUKAFINIWA NA KUSALIWA

Ama wale waliouliwa nje ya uwanja wa vita, yote sawa ikiwa wameuliwa na kafiri au Muislam, hao kisheria pia wanaitwa mashahidi, isipokuwa wao wanaoshwa na kukafiniwa na kusaliwa.
Mtume (SAW) aliwaosha na kuwasalia watu wa aina hiyo waliouliwa wakati yeye Mtume (SAW) alipokuwa bado yu hai. Na Waislam waliwaosha Omar na Othman na Ali na wote hao waliuliwa, na kwa ajili hiyo walikufa mashahidi.
Kutoka kwa Abu Huraira alisema kuwa Mtume (SAW) aliuliza;
"Wepi mnaowahesabu kuwa ni mashahid?"
Masahaba (RA) wakasema;
"Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, aliyeuliwa katika vita vya Jihadi kwa ajili ya Mwenyezi Mungu huyo ni shahid".
Akasema;
"(Ikiwa ni hao tu) Basi mashahid katika umma wangu watakuwa wachache".
Wakamuuliza;
"Wepi wengine ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu?"
Akasema;
"Atakayeuliwa katika njia ya Mwenyezi Mungu huyo ni shahid, na atakayekufa akiwa katika njia ya Mwenyezi Mungu huyo ni shahid, na atakayekufa kwa (maradhi) ya tauni ni shahid, na atakayekufa kwa maradhi ya tumbo ni shahid na aliyezama (alyekufa kwa kuzama) ni shahid".
Muslim
Na kutoka kwa Said bin Zeid kuwa Mtume (SAW) amesema;
"Atakayeuliwa kwa kuilinda mali yake naye ni shahid, atakayeuliwa kwa kujihami nafsi yake naye ni shahid, na atakayeuliwa kwa kuilinda dini yake, naye ni shahid na atakayeuliwa akiwalinda ahli yake naye ni shahid".
Imam Ahmed na Attirmidhiy
KUMUOSHA MAITI
Si vizuri kuhudhuria watu wengi katika kuosha maiti isipokuwa wale wanaohitajika tu na walioruhusiwa na watu wa maiti, na muoshaji lazima awe mtu muaminifu ili awe anawaeleza watu yale ya kheri tu katika mambo atakayoona, na ayasitiri yale yenye shari.
Mtume (SAW) amesema;
"Waoshe maiti zenu wale wanaoaminika".
Ibni Majah
Maulamaa wamekhitalifiana juu ya maiti avuliwe nguo zake zote wakati wa kuoshwa au asivuliwe. Anasema Ibni Rushd al Qurtubiy katika 'Bidayatul mujitahid wa Nihayatul muqtasid';
"Imam Abu Hanifa anaona kuwa maiti avuliwe nguo zake na afunikwe tupu zake.
Ama Imam Shafi, yeye anaona kuwa maiti aoshwe akiwa amevalishwa sanda yake atakayobadilishwa baada ya kuoshwa.
Sababu ya kuhitalifiana kwao inatokana na kukoshwa kwa Mtume (SAW) akiwa na nguo zake. Wengine wakasema kuwa wamemuosha vile kwa sababu yule ni Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW). Wengine wakasema;'La, bali hivyo ndivyo inavyotakiwa". Wote wamekubaliana kuwa kilichoharamishwa kukitizama mtu anapokuwa hai, basi kwa maiti pia ni haramu kukitizama.
Anasema Sheikh Nasseriddin al Albani katika kitabu chake kitwacho; 'Ahkam al Janaiz wa Bidaiha';
"Katika kuosha maiti yazingatiwe yafuatayo;
  1. Aoshwe mara tatu au tano au saba au zaidi pakihitajika na hadithi ya Mtume (SAW) inayohusiana na haya itafuatilia.
  2. Uoshaji uwe kwa tarakimu witri.(yaani tatu au tano au saba au tisa nk.)
  3. Maji mengine yachanganywe na majani ya mkunazi au chochote kinachoweza kushika nafasi yake katika kusafisha kama vile sabuni nk.
  4. Muosho wa mwisho yachanganywe na kafur au kama haipatikani basi na manukato yoyote.
  5. Ifunguliwe mikia ya nywele kisha zioshwe vizuri,
  6. Zichanwe nywele
  7. Mwanamke asukwe maquruni matatu kisha ilazwe nyuma.
  8. Kuosha kuanzie sehemu za upande wa kulia na sehemu za udhu.
  9. Wanaume wawaoshe wanaume wenzao na wanawake wawaoshe wanawake wenzao isipokuwa penye udhuru (au rukhsa).
  10. Na dalili ya yote hayo inapatikana katika hadithi ya Mtume (SAW) ifuatayo;
    Anasema Ummu Atiya (RA);
    "Aliingia Mtume (SAW) wakati sisi tunamuosha binti yake (Zeinab) akasema;
    "Muosheni mara tatu au tano (au saba), au zaidi kuliko hapo mkiona panahitajika kwa maji na majani ya mkunazi".
    Anasema;
    "Nikamuuliza; 'witran'?" (kwa tarakimu za witri?)
    Akasema;
    "Ndiyo, na mnapotia maji mara ya mwisho changanyeni na kafur na mkeshamaliza niiteni".
    Tulipomaliza tukamuita, akatutupia saruni yake, kisha akasema;
    "Mvalisheni kwanza (igusane na ngozi yake)".
    Kisha tukamsuka mikia mitatu na kuitupa nyuma. Mtume (SAW) alituamiba (pia);
    "Anzeni upande wa kulia".
    Bukhari - Muslim - AbuDaud - Annasaiy - Attirmidhiy - Ibni Majah - Ibni l Jarudi - na Ahmed.
  11. Atakayemuosha avae kitambaa mkononi na kumsitiri maiti kwa kumfunika kitu kitachomsitiri mwili wake baada ya kuvuliwa nguo zake zote, kama ilivyokuwa wakati wa Mtume (SAW).
  12. Muhrim, (yule aliyefariki akiwa amevaa nguo za Ihram kwa ajili ya Hija) hayumo katika sharti (d) la kuyachanganya maji kwa kafur au kwa manukato mazuri, kwani yeye haijuzu kumpaka manukato kutokana na hadithi ya Mtume (SAW) aliposema;
  13. "Msimpake mafuta mazuri kwani anafufuliwa siku ya kiama akiwa anafanya talbiya (akiwa anasema 'Labbayka llahumma labbayka')".
  14. Katika shuruti (I) la mwanamume kuoshwa na mwanamume mwenzake na hali kadhalika mwanamke kuoshwa na mwanamke mwenzake, anatolewa mume na mke, kwani wao kutokana na dalili mbali mbali wanaruhusiwa kuoshana.
  15. Ni vizuri kazi ya kuosha maiti ifanywe na mtu anayeelewa vizuri mafundisho ya kuosha. Na ni bora zaidi ikiwa mtu huyo atakuwa katika watu wa nyumba yake maiti huyo, kwani Mtume (SAW) alioshwa na watu wa nyumba yake, na Ali (RA) alisema;
"Nilipokuwa nikimuosha Mtume (SAW) nilikuwa nikimtizama sana nikidhani kuwa kutakuwa na hitilafu yoyote ile, lakini sikuona kitu, na alikuwa akipendeza (sana) pale alipokuwa yuhai na hata baada ya kufa kwake".
Ibni Majah - Al Hakim na wengineo na akasema hadithi ni sahihi kwa masharti yaliyowekwa na Bukhari na Muslim.
Anasema Sh.Al Albani (Mwenyezi Mungu amrehemu) kuwa;
"Na muoshaji ana ujira mkubwa sana kwa Mwenyezi Mungu, lakini kwa masharti mawili yafuatayo;
  1. Amsitiri na asihadithie ikiwa ataona jambo lolote lile lisilo la kawaida, kwa sababu Mtume (SAW) amesema;
  2. "Atakayemuosha Muislam na asizungumze juu yake, Mwenyezi Mungu anamghufiria mara arubaini…."
    Al Hakim - Al Baihaqi na wengineo.
    Na katika riwaya iliyotolewa na Attabarani;
    "Anasamehewa madhambi makubwa arubaini (arbaina kabiyrah)".
  3. Aifanye kazi hiyo kwa ajili ya kutaka radhi za Mwenyezi Mungu na si kwa kutaka ujira kutoka kwa watu au kwa kutaka kushukuriwa kwa kupewa chochote kilekatika mamboya kidunia. Na hii inatokana na dalili mbali mbali kuwa Mwenyezi Mungu haikubali ibada yoyote isipokuwa ile iliyofanywa halisi kwa ajili ya kutaka radhi Zake".
Katika kuithibitisha hoja hii, Sheikh aliandika aya mbali mbali pamoja na hadithi ya Mtume (SAW) isemayo;
"Hakika ya amali (yoyote ile inakubaliwa) kwa nia zake, na kila mja anapata kutokana na nia yake…"
Bukhari na Muslim
NAMNA YA KUMUOSHA MAITI
Hapa nitanukuu moja kwa moja kutoka katika kitabu kidogo kiitwacho 'Huduma za kuosha Maiti', nilichopewa zawadi na Bwana Muhammed Humaid Al Khatry - mwandishi wa kitabu hicho, nilipokwenda kumtembelea nyumbani kwake.
Katika mlango wa 'Namna ya kumuosha maiti', Sheikh ameandika;
Ni vizuri huduma za Maiti zote zifanywe na jamaa zake au kwa ruhusa yao. Maiti huoshwa juu ya mnyanyuko kama kitanda au ubao au baraza ya saruji. Hulazwa chali. Na muoshaji huwa mmoja, wengine huwa watiliaji maji. Wote huitwa waoshaji. Ni uzuri wasiwe wengi. Na ni uzuri wale wasiohusika wasikaribie kama hawahitajiki. Wasijipeleke, wangoje wenyewe wawaombe kuosha na kuvika sanda. Ama kumsalia na kumchukua haihitaji ruhusa.
Muoshaji huvaa gloves. Hizi zinaweza kuwa za plastic au za kitambaa. Zinaweza kushonwa hapo hapo kutokana na sehemu ndogo ndogo za sanda.Hatua za kuosha ni hizi;
  1. Ni uzuri kufukiza ubani au udi wakati wa kuosha na kuvika sanda (hii si wajib wala si sunnah).
  2. Maiti asitiriwe kwa kufunikwa guo mwili mzima wakati anapokoshwa akoshe pahala stara kwa mapazia au hata uwa wa majani.
  3. Maji machafu na uchafu viwe na njia ya kwendea shimoni au uchimbwe ufuo. Ufuo ni shimo linalochimbwa kusudi kuingia huo uchafu na maji machafu.
  4. Ni vizuri miguu ya maiti kuelekekezwa Kibla ili uso wake nao uelekee Kibla pia.
  5. Muoshaji atie nia ya kumuosha mati. Sio lazima wala sio Sunnah kuitamka nia.
  6. Muoshaji huku amevaa gloves, amsafishe maiti kwa maji safi, yasiwe baridi sana wala ya moto sana.
  7. Muoshaji ataondoa juu ya mwili wa maiti, najsi ikiwapo kama damu, usaha, nk. Na akiwa na vidonda avioshe vyema kwa upole kabisa.
  8. Amnyanyue maiti sehemu ya juu kama anayemueka kitako na huku anambana tumbo kwa upole kabisa ili utoke uchafu tumboni. Wakati huu maiti huwa baina ya kuwa amelala na kukaa kitako. Muoshaji hodari humzuia kichwa kwa kidole gumba na mgongo kwa vidole vinne vengine na mkono mmoja akawa anambania tumbo. Wakati huu maiti akitoka uchafu humiminiwa maji kwa wingi.
  9. Kisha amlaze chali kama alivyokuwa. Amsafishe sehemu zote za siri kwa maji mengi. Hata katika hatua hii asisahau kumsitiri maiti kadiri ewezekanavyo.
  10. Maiti akiwa safi, muoshaji atavua gloves na atachukua kitambaa kidogo cha kumsafishia meno. Muoshaji, kwa kidole chake cha shahada alichokizungushia hicho kitambaa atamsuwaki maiti kwa kitambaa chengine kidogo atamsafisha pua na kuiosha pia kwa upole.
  11. Muoshaji atatia nia ya kumtia udhu maiti. Kisha atamtia udhu wa anayetaka kusali. Mpango ni ule ule wa udhu wa Sala.
  12. Maiti huoshwa mara tatu au tano au mpaka asafike. Mara ya mwanzo huoshwa kwa maji matupu. Mara ya pili ni pamoja na majani ya mkunazi au sabuni, na mara tatu ni maji yenye kutiwa kaafur. Na mara zote hizo aoshwe kwa mpangu huu ikiwezekana.
((Mtume (SAW) amesema;
"Waosheni 'witran', mara tatu au tano au saba au zaidi ya hapo mkiona inahitajika kwa majani ya mkunazi na mara ya mwisho kwa kafur".))
  1. Kichwa chote pamoja na ndevu na nywele mpaka ncha kabisa. Ihakikishwe kuwa mwanamke mwenye nywele refu zimepata maji zote mpaka ncha kabisa pamoja na ngozi ya kichwa.
  2. Mwili mbele sehemu yote ya upande wa kulia mpaka miguuni.
  3. Mwili mbele sehemu yote ya upande wa kushoto mpaka miguuni.
  4. Mwili nyuma sehemu yote ya upande wa kulia mpaka miguuni.
  5. Mwili nyuma sehemu yote ya upande wa kushoto mpaka miguuni.
((Mtume (SAW) amesema;
"Anzeni kuliani pao na sehemu za kutia udhu".))
  1. Muoshaji ampanguse maji maiti mwili wote kwa kitambaa kikavu au kwa taula.
  2. Ni uzuri kwa muoshaji kukoga baada ya kumaliza kuosha hasa ikiwa amerukiwa na maji yaliyotumika. Lakini kuoga si lazima. Maiti Muislamu sio najsi. Ama muoshji akiwa amegusa uchafu basi atie udhu.


TAYAMUM PAKIKOSEKANA MAJI\

Pakikosekana maji, maiti anafanyiwa tayamum kutokana na kauli ya Mwenyezi Mungu Subhanahu wa Taala aliposema;
"Na kama hamkupata maji basi tayamamuni"
Na kutokana na hadithi ya Mtume (SAW) aliposema;
"Imejaaliwa kwa ajili yangu ardhi yote (kuwa) msikiti na tahiri", na pia anaweza kutayamamishwa maiti ikiwa mwili utaharibika kwa kuoshwa na maji.
YASIYOFAA KUFANYIWA MAITI
Katika mambo yasiyofaa kufanyiwa matiti ni;
  1. Kumuacha wazi akaonekana mwili wake.
  2. Kumtesa kwa hali yoyote ile. Ikiwa wakati wa kumkosha au mwengineo. Kwa mfano, haifai mwoshaji anapomkosha kidonda akimkosha bila ya kumhurumia kwa kudhani kuwa maiti haumii. Wala haifai kumkosha kwa maji ya moto sana wala baridi sana.
  3. Kumnyoa chochote mwilini mwake.
  4. Kumpiga picha.
  5. Kumtoa kiungo chake kwa sababu yoyote ile.
  6. Kumsema vibaya (kumsengenya).
  7. Kumfanyia masikhara
  8. Kuchelewa kumhudumia maiti. Si vizuri kumchelewesha maiti.
  9. Kuomboleza. Si kosa kumlilia maiti, lakini haijuzu kuomboleza kwa kutaja mema yake au yale yatakayokosekana baada ya kufa kwake, kwa sababu Mtume (SAW) siku aliyokufa mwanawe, watu waliona macho yake yakitoka machozi, wakamuuliza;
"Hata wewe Mtume wa Mwenyezi Mungu?".
Mtume (SAW) akawajibu;
"Hakika jicho linatoka machozi na moyo unahuzunika, lakini hatusemi ila yale yanayomridhi Mola wetu".
Na katika hadithi nyingine akasema;
"Mwenyezi Mungu haadhibu kwa sababu ya kutoka machozi wala kwa huzuni ya moyo, lakini huadhibu au hurehemu kwa huu (ulimi)".

MUHAMMAD FARAJ SALEM AL SAIY

Post a Comment

1 Comments