Imekusanywa Na Muhammad Faraj Saalim As-Sa’iy
Badr
ni jina la mji ulio kiasi cha kilomita mia na hamsini mbali na mji wa
Madiynah, na mahali hapo hapakuwa na chochote isipokuwa bonde tu na
kisima kilichokuwa milki ya mtu mmoja aitwae Badr, na kwa ajili hiyo
mahala hapo pakaitwa ‘Badr’. Kwa vile vita hivyo vilipiganwa mahali
hapo, ndiyo maana vikaitwa vita vya Badr.
Vita
hivyo vilitokea asubuhi ya siku ya Ijumaa, Ramadhani ya kumi na saba
mwaka wa pili baada ya Hijra (baada ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa
aalihi wa sallam) kuhamia Madiynah).
Sababu Za Vita
Chanzo
cha vita hivi kilikuwa ni msafara wa biashara wa makafiri ukiongozwa na
Abu Sufyan uliokuwa ukitoka nchi ya Sham ukirudi Makkah ukiwa na watu
wasiozidi arobaini. Msafara huu ulikuwa umebeba mali nyingi sana
ya watu wa Makkah, na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa
sallam) akaona hii ni fursa nzuri ya kuipiga
dola hiyo ya kikafiri kiuchumi, kijeshi na kisiasa, na pia kulipiza kisasi. Hasa kwa vile Waislam walipohama Makkah kwenda Madiynah, Makafiri waliwalazimisha kuziacha mali zao zote huko, na kuondoka bila chochote isipokuwa nguo zao na mnyama wa kumpanda. Bali wengine walinyang’anywa hata wanyama wao, na ikawabidi kutembea kwa miguu mpaka Madiynah na wengine waliviziwa njiani na kuuliwa.
dola hiyo ya kikafiri kiuchumi, kijeshi na kisiasa, na pia kulipiza kisasi. Hasa kwa vile Waislam walipohama Makkah kwenda Madiynah, Makafiri waliwalazimisha kuziacha mali zao zote huko, na kuondoka bila chochote isipokuwa nguo zao na mnyama wa kumpanda. Bali wengine walinyang’anywa hata wanyama wao, na ikawabidi kutembea kwa miguu mpaka Madiynah na wengine waliviziwa njiani na kuuliwa.
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akawaambia Waislam:
((Msafara huu wa Makuraysh umejaa mali zao, uendeeni, huenda Allaah akatulipa (haki zetu walizotunyang’anya) kwa kutuwezesha kuuteka.))
Nguvu Za Jeshi La Waislam
Si watu wengi waliojitolea kwenda, na hii ni kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakutilia mkazo sana kutoka huko. Hakumlazimisha mtu kwenda naye na wala hakumlaumu yeyote yule asiyetoka pamoja naye. Bali alimwacha kila mmoja ajiamulie mwenyewe ikiwa anataka kwenda au hataki. Na kwa ajili hiyo Maswahaabah wachache tu walimfuata.
Mtume
(Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akaondoka akiwa na watu
wapatao mia tatu na kidogo tu hivi. Inasemekana walikuwa mia tatu na
kumi na tatu au kumi na nne na riwaya nyengine zinasema kuwa walikuwa
mia tatu na kumi na saba. Themanini na sita kati yao ni Muhajiriyn (watu wa Makkah waliohamia Madiynah) na mia mbili thelathini na moja ni watu wa pale pale Madiynah.
Maswahaabah
(Radhiya Allaahu ‘anhu) hawakujuwa kuwa msafara huu utakuja geuka kuwa
ni moja katika mapambano makubwa baina ya Haki na Baatwil. Walidhania
kuwa yatakuwa yale mapambano ya kawaida baina ya makundi ya wapiganaji
wa Kiislam na misafara midogo midogo ya makafiri. Hawakujua kuwa Allaah
amekwisha panga atimize jambo lililokuwa lazima litendeke.
Waliondoka
wakiwa na farasi wawili tu, mmoja wa Zubair bin Awaam na mwengine wa
Mikidaad bin Al-Aswad Al-Kindy (Radhiya Allaahu ‘anhu). Walikuwa pia na
ngamia sabiini wakipokezana katika kuwapanda.
Jeshi La Waislam Linaondoka Kuelekea Badr
Mtume
(Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akaondoka Madiynah pamoja
na Swahaabah zake hao (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuufuatia msafara huo wa
Abu Sufyan. Akamchaguwa Ibni Ummi Makhtuum (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa
ni mkuu wa Madiynah badala yake, lakini alipofika nje kidogo ya
Madiynah, mahali panapoitwa Ar-Rawha, akamrudisha Swahaabah mmoja
anayeitwa Aba Lubaba (Radhiya Allaahu ‘anhu), na kumtaka yeye awe
khalifa wake pale Madiynah badala ya Ibni Ummi Makhtuum (Radhiya Allaahu
‘anhu).
Katika
msafara huo, Mtume(Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)
akamchagua Mas-‘ab bin ‘Umair (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa ni mshika
bendera, na bendera yenyewe ilikuwa ya rangi nyeupe.
Akaligawa jeshi makundi mawili:
1. Kikosi cha Muhajiriyn (watu wa Makkah) na akampa bendera yao ‘Aliy bin Abi Twaalib (Radhiya Allaahu ‘anhu).
2. Kikosi cha watu wa Madiynah, na akampa bendera yao Sa’ad bin Mu’aadh (Radhiya Allaahu ‘anhu).
Mtume
(Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akaondoka na jeshi lake
hilo akiifuata njia ya Makkah, na alipofika mji uanoitwa Ar-Rawha
akapumzika, na baada ya kupumzika mahala hapo akaondoka kuelekea mji wa
Badr akiiacha njia ya Makkah kushotoni kwake na kuendelea na safari yake
mpaka akalifikia bonde la Rahiyqan na baada ya kuendelea mbele kidogo,
akawatuma Maswaahabah Basis bin ‘Umar na Uday bin Azzaghaabah (Radhiya
Allaahu ‘anhu) watangulie na kupeleleza habari za msafara waliokusudia
kuuteka.
Msafara Wa Abu Sufyan
Ama
Abu Sufyan aliyekuwa kiongozi wa msafara wa biashara ya makafiri wa
Makkah, alikuwa ni mtu mwenye kuchukua hadhari sana, alijuwa kuwa njia
ya Makkah ina hatari nyingi, na kwa ajili hiyo, kila mara alikuwa
akitanguliza wapelelezi ili wamletee habari za mbele ya safari, wakati
huo huo alikuwa akimuuliza kila anayekutana naye, iwapo huko alikotoka
ameona chochote kile kisichokuwa cha kawaida.
Katika kuuliza uliza kwake akamuuliza mtu mmoja anayeitwa Majdi bin ‘Amru iwapo ameona jeshi kutoka mji wa Madiynah, akasema:
“Mimi sikuona majeshi, lakini niliona kundi kubwa la watu waliopumzisha ngamia wao mahali hapa”.
Abu
Sufyan akaenda kupafanyia uchunguzi mahali pale alipoambiwa kuwa watu
walipumzisha ngamia wao. Baada ya kuchambua kinyesi cha ngamia
waliopumzishwa mahali hapo na kuona kokwa za tende ndani yake, akasema:
“Madamu choo chao kimejaa kokwa za tende, hapana shaka yoyote kuwa hawa ni ngamia wa watu wa Madiynah”.
Alipotambua
hayo, akajua kuwa anaviziwa, na hapo hapo akageuza njia yake na kumtuma
mtu mmoja aitwae Dhamdham bin ‘Amru Al-Ghafaariy atangulie mbio sana. Aende kuwazindua watu wa Makkah juu ya hatari inayoukabili msafara wao wenye vitu vya thamani kubwa sana.
Watu wa Makkah waliposikia hayo, wakasema:
“Muhammad anadhania kuwa atauteka msafara huu kwa urahisi kama
alivyouteka msafara wa ‘Amru bin Al-Hadhramiy?” (Kisa cha kutekwa kwa
msafara wa ‘Amru nimekielezea katika makala ya ‘Miezi Mitukufu’).
Makafiri wakaendela kusema:
“Haitokuwa hivyo kabisa! WaLlaah atakiona chake Muhammad safari hii”.
Jeshi La Makafiri Wa Makkah
Makuraysh
mara baada ya kujuulishwa juu ya hatari hiyo, wakakusanya jeshi la watu
wapatao alfu moja na mia tatu, farasi wapatao mia moja na ngamia wengi sana. Wakaondoka hapo wakiongozwa na Abu Jahal bin Hishaam pamoja na vigogo vya Makuraysh.
Walisafiri kwa kasi kubwa sana
kuelekea kaskazini mahali uliopo mji wa Badr. Walipoufikia mji uitwao
Al-Juhufa, wakapata salamu kutoka kwa Abu Sufyan kuwa; msafara wake
umekwishasalimika na hatari ya kutekwa, na akawataka warudi Makkah.
Kwa
sababu mara Abu Sufyan alipotambua kuwa anafuatwa, akabadilisha njia na
kupita njia ya pwani pwani badala ya kupitia njia ya mji wa Badr. Na
kwa ajili hiyo akaokoka na kuwapelekea habari hizo wenzake.
Abu Jahal akasema:
“Wallahi
haturudi, mpaka tufike Badr, tukae hapo siku tatu, tuchinje wanyama
wetu, tunywe pombe yetu na waimbaji waimbe mpaka habari zetu ziwafikie
Waarabu wote ili wapate kutujuwa ni nani sisi na ili watuogope”.
Tatizo La Jeshi La Waislam
Waislam
walipata habari za kuwaponyoka kwa msafara wa Abu Sufyan na wakati huo
huo wakapata habari za jeshi kubwa la watu wa Makkah lililowakabili
lililoazimia kwenda mji wa Badr, na kwa ajili hiyo wakaingia katika
tatizo kubwa sana.
Baadhi yao
wakaingiwa na hofu, na wengine wakatoa wazo la kurudi Madiynah, na hii
ni kwa sababu walikuwa wachache, hawana silaha za kutosha na hawakutoka
kivita. Lakini ikawabidi kulikabili tatizo hilo kwa ushujaa mkubwa
kabisa kwani iwapo watakimbia kupambana na jeshi la makafiri na kuliacha
litambe hapo Badr, mji ulio katika eneo la karibu na mji wa Madiynah,
huko kutawapa nguvu na kichwa kikubwa makafiri na watapata moyo zaidi,
jambo ambalo halitakuwa na mwisho mwema. Wakati huo huo haiba ya jeshi
la Waislam itaondoka.
Mwanachuoni mkubwa Al-Mubaarak Fury anasema katika kitabu chake Ar-Rahiyqul Makhtuum:
“Jeshi
la Waislam lingekuwa mfano wa mwili bila ya roho, na makafiri wangepata
moyo wa kujaribu kuushambulia mji wao wa Madiynah bila ya hofu yoyote
ile”.
Allaah Anasema:
{{(Atakunusuru) kama alivyokutoa Mola wako katika nyumba yako kwa haki, na kundi moja la walioamini halipendi (utoke).
Wakabishana nawe katika haki baada ya kubainika kwenda huko kama kwamba wanasukumwa katika mauti na huku wanaona.
Na
Allaah alipo kuahidini kuwa moja katika makundi mawili ni lenu. Nanyi
mkapenda lisilo na nguvu ndio liwe lenu; na Allaah anapenda ahakikishe
Haki kwa maneno yake, na aikate mizizi ya makafiri.
Ili ahakikishe Haki na auvunje upotovu na wangechukia wakosefu.}}
[Suuratul-Anfaal: 5-8]
Mtume (Swalla Allaahu ‘Alayhi Wa Aalihi Wa Sallam) Anashauriana Na Sahaba Zake (Radhiya Allaahu ‘Anhum)
Kutokana
na mabadiliko haya ya ghafla na ya hatari, ilimbidi Mtume (Swalla
Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aitishe mkutano wa mashauriano na
wakuu wa jeshi la Waislam ili kuwajuulisha juu ya hali ya mambo ilivyo
na kutaka ushauri wao.
Ama
wale aliowashauri katika wakubwa wa jeshi lake, kwanza aliinuka Abu
Bakar (Radhiya Allaahu ‘anhu) akatoa hutoba nzuri ya kumuunga mkono
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) juu kulazimika kwao
kupigana na makafiri.
Kisha akainuka ‘Umar bin Khatwaab (Radhiya Allaahu ‘anhu) na kutoa hotuba nzuri vile vile.
Kisha akainuka Al-Mikdaad bin ‘Amru (Radhiya Allaahu ‘anhu) akasema:
“Ewe Mtume wa Allaah, nenda kama atakavyokuonyesha Allaah, na sisi tuko nyuma yako. WaLlaah hatukuambii kama walivyomuambia wana wa Israili Mtume wao Muusa: {{Nenda wewe na Mola wako mkapigane vita sisi tutakaa hapa (tunangoja)}}. Bali tunakwambia: ‘Nenda wewe na Mola wako ukapigane na sisi pamoja nanyi tutapigana …”
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: ((Vyema)) Kisha akamuombea du’ah.
Hawa watatu wote walikuwa katika Muhajiriyn ‘Watu wa Makkah’, ambao ni wachache katika jeshi hilo,
na Mtume(Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akapenda kujua rai
ya viongozi wa watu wa Madiynah waliokuwa wengi katika jeshi hilo, akasema: ((Nipeni shauri lenu enyi watu))
Akikusudia
watu wa Madiynah. Sa’ad bin Mu’aadh (Radhiya Allaahu ‘anhu) aliyekuwa
mmoja wa viongozi wa watu wa Madiynah akatambua hayo, akasema: “WaLlaah kama kwamba unatukusudia sisi ewe Mtume wa Allaah?”
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: ((Ndiyo))
Sa’ad (Radhiya Allaahu ‘anhu) akasema:
“Sisi
tumekuamini na kukusadiki, na tukashuhudia kuwa uliyokuja nayo ndiyo
haki, na tukakupa ahadi zetu na neno letu kuwa tutakusikiliza na
kukutii, kwa hivyo endelea tu kama unavyotaka kwani WaLlaah kama
utatutaka tuivuke bahari hii, ukaivuka, basi tutaivuka pamoja nawe na
hapana hata mmoja kati yetu atakayebaki nyuma, sisi hatuogopi kupambana
na adui kesho, sisi ni watu wenye kusubiri katika vita na wakweli katika
mapambano na InshaAllaah Allaah atakuonyesha ndani yetu yale
yatakayokufurahisha macho yako, kwa hivyo tuongoze kwa baraka za
Allaah”.
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akafurahishwa sana na maneno ya Sa’ad (Radhiya Allaahu ‘anhu), akasema:
((Nendeni
na nakupeni bishara njema, Allaah ameniahidi moja wapo ya makundi
mawili. Wallahi kama kwamba ninaona wapi wataanguka kila mmoja kati ya
maadui.))
Majeshi Ya Kiislam Yanafanya Upelelezi
Walipowasili
mahali panapoitwa Addiya, karibu na Badr, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi
wa aalihi wa sallam) pamoja na Sahibu yake wa pangoni Abubakar
As-Swiddiiq (Radhiya Allaahu ‘anhu), wakatoka na kuanza kufanya
uchunguzi nje ya kambi yao, na katika kutembea kwao, wakakutana na mzee
mmoja wa Kiarabu na kumuuliza juu ya habari za jeshi la Makuraysh na juu
ya habari za jeshi la Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa
sallam), ili asiweze kutambua ni katika kundi gani wao.
Yule mtu akawaambia:
“Kabla sijakujibuni, nambieni kwanza nyinyi mnatokea wapi?”
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia:
((Ukituambia na sisi tutakuambia…?))
Yule mtu akasema:
“Nimesikia
kuwa jeshi la Muhammad na Sahibu zake lilitoka siku kadhaa wa kadhaa,
ikiwa habari hizo ni sahihi, basi leo watakuwa washafika mahali kadhaa.”
Akapataja mahali lilipo jeshi la watu wa Madiynah.
“Na
nimesikia kuwa Makuraysh wametoka siku kadhaa wa kadhaa, na ikiwa
maneno niliyoambiwa ni kweli, basi leo watakuwa washafika mahali kadhaa
wa kadhaa.”
Akapataja mahali lilipo jeshi la Makuraysh.
Baada ya kumaliza kusema, akawauliza:
“Nyinyi mnatokea wapi?”
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamuambia:
((Sisi tunatokana na maji.))
Kisha akaondoka.
Yule mtu akawa anajiuliza:
“Hawa wanatoka katika maji ya Iraaq au maji gani?”
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakusema uongo, kwani viumbe vyote vinatokana na maji. Allaah anasema:
{{Na tukafanya kwa maji kila kitu kilicho hai.}} [Suuratul-Anbiyaa:30]
Waislam Wanapata Habari Muhimu Kuhusu Jeshi La Makuraysh
Mchana
wake siku hiyo, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)
aliwatuma watu watatu kwenda kupeleleza juu ya habari za jeshi la
Makuraysh, nao ni: ‘Aliy bin Abi Twaalib, Az-Zubayr
bin ‘Awaam na Sa’ad bin Abi Waqaas (Radhiya Allaahu ‘anhu).
Walipokwenda penye kisima cha Badr wakawakuta watoto watatu wanachota
maji kwa ajili ya kuwapelekea jeshi la Makuraysh, wakawateka na kwenda
nao kambini ili kuwauliza masuali.
Walipofika
nao kambini Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa
akiswali, kwa hivyo wao wakaanza kuwauliza mateka wao.
Vijana hao wakasema kuwa wametumwa na Makuraysh ili kuwachotea maji. Maswaahabah walikasirishwa na jibu hilo, kwani walitamani wawe watu wa msafara wa Abu Sufyan. Wakawapiga sana mpaka wakasema kuwa wao ni watu wa Abu Sufyan na si watu wa jeshi la Makuraysh. Baada ya kutamka hayo, wakawaachilia.
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) baada ya kumaliza kusali akawaambia;
{{Waliposema
kweli mliwapiga, na walipokudanganyeni mkawachilia. Walisema kweli
WaLlaahi, kwani wao ni watu wa jeshi la Makuraysh.))
Kisha Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akawuliza wale vijana:
((Nipeni habari za Makureshi.))
Wakasema:
“Wapo katika ng’ambo ya bonde lile la mbali”.
Akawauliza:
((Wako wangapi?))
Wakasema:
“Wengi”
Akawauliza:
((Idadi yao ngapi?))
Wakasema:
“Hatujuwi”
Akawauliza:
((Wanachinja wanyama wangapi kila siku?))
Wakasema:
“Siku nyingine wanachinja ngamia tisa na siku nyingine kumi”.
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema kuwaambia Maswahaabah (Radhiya Allaahu ‘anhum):
((Idadi yao ni baina ya watu mia tisa na elfu.))
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akawauliza tena wale vijana:
((Nani katika vigogo vya Makuraysh wamo miongoni mwao?))
Wakasema:
“’Utbah
na Shaiba watoto wa Rabia, Abu Al-Bakhtari bin Hishaam, Hakiym bin
Hizaam, Naufil bin Khuwailid, Al-Haarith, Taimah, An-Nadhar bin Haarith,
Zaamah bin Aswad, Abu Jahal bin Hishaam, na Umayyah bin Khalaf”.
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema kuwaambia Swahaabah zake (Radhiya Allaahu ‘anhum):
((Makkah imekutupieni (imekuleteeni) vipande vya maini yao [vigogo vyao na vipenzi vyao].))
Kuteremka Kwa Mvua
Waislam wakasogea mbele kidogo mpaka wakakaribia bonde la karibu na mahali yalipopiga kambi majeshi ya Makuraysh.
Allaah
aliwateremshia Waislam utulivu wakalala vizuri, hata wengine wakaota na
kuamka wakiwa na janaba. Lakini mahali hapo hapakuwa na maji ya kuogea
ili wapate kujitahirisha na wala ya kunywa, na Shaytwaan akaanza kuwatia
wasi wasi:
“Vipi mtapigana kesho wakati miili yenu haina tohara, vipi mtapigana kesho mkiwa na kiu…?”
Allaah akawateremshia mvua iliyowasaidia sana. Kwa sababu kutokana na mvua hiyo waliweza:
· Kujitahirisha,
· Kuondoa uchafu wa shetani, na
· Kuzipa nguvu nyoyo zao.
Na maji ya mvua pia yakawasaidia kuufanya mchanga chini yao uwe mgumu ili waweze kutembea vizuri bila ya kuteleza wakati wa mapambano.
Allaah Anasema:
{{Alipo
kufunikeni kwa usingizi uwe ni uaminisho kutoka kwake, na
akakuteremshieni maji kutoka mbinguni ili kukusafisheni kwayo na
kukuondoleeni uchafu wa Shaytwaan, na kuzipa nguvu nyoyo zenu, na kuitia
imara miguu yenu.}} [Suuratul-Anfaal: 11]
Jeshi La Waislam Linatangulia Kukamata Sehemu Muhimu
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akaliamrisha jeshi lake liondoke pale walipo haraka sana
ili wawahi kusogea mbele karibu na mahali yalipo maji ya mji wa Badr.
Wakasogea mpaka wakafika mwanzo wa visima vya maji ya Badr na Mtume
(Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akawaamrisha kupiga kambi
hapo.
Mmoja
katika Maswaahabah aitwaye Al-Khabaab bin Mundhir (Radhiya Allaahu
‘anhu), akamuuliza Mtume(Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
“Ewe
Mtume wa Allaah, mahala hapa tuliposimama, Allaah amekuamrisha na
hatuna haki ya kusonga mbele zaidi au ni katika hila za kivita tu na rai
yako mwenyewe?”
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia:
((Bali ni hila za kivita na rai yangu mwenyewe.))
Akasema:
“Ewe
Mtume wa Allaah, mimi naona kuwa hapa si makaazi mazuri, bora tusogee
mbele mpaka mwisho wa visima vya maji ya Badr, tuvizunguke kisha tujenge
mahodhi, tuyajaze maji, kisha tupambane nao, sisi tutakuwa tunakunywa
na wao wasipate kunywa”.
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema:
((Rai uliyotowa ni nzuri.))
Wakaondoka hapo na kusogea sehemu ya juu ya mahali yalipo maji, na usiku wakaanza kutengeneza mahodhi na kuyajaza maji.
Makao Makuu Ya Jeshi
Baada ya kumaliza kazi yao
hiyo, Sa’ad bin Mu’aadh (Radhiya Allaahu ‘anhu) akatoa rai pajengwe
mahali patakapokuwa makao makuu ya jeshi lao, ili waweze kujitayarisha
na kuikabili hali ya hatari yoyote itakayotokea iwapo jeshi lao
litashindwa katika vita hivyo.
Akasema:
“Ewe
Mtume wa Allaah, unaonaje tukakujengea kipaa mfano wa hema (‘Ariish),
kisha tukakuwekea tayari wanyama wa kupanda, kisha sisi tutapambana na
adui, ikiwa Allaah atatujaalia tukawashinda, hayo ndiyo tunayoyapenda.
Ama ikiwa kinyume na hivyo, basi wewe utapanda wanyama wako na utakwenda
kujiunga na wenzetu tuliowaacha nyuma, kwani hao tuliowaacha nyuma
mapenzi yao juu yako ni makubwa pia kama sisi. Wangelijuwa kuwa utapambana na adui, basi wasingerudi nyuma kabisa na wangepigana jihadi pamoja nawe.”
Mtume
(Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamuombea kila la khayr
kwa rai yake hiyo, na Waislamu wakajenga mfano wa hema juu ya kilima,
sehemu ya Kaskazini ya uwanja wa mapambano, sehemu ambayo mtu anaweza
kuviona vita bila ya taabu huku vikipiganwa.
Usiku Kabla Ya Mapambano
Usiku
kabla ya mapambano, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)
alilipanga vizuri jeshi lake. Kisha akawa anatembea huku akiwaonyesha
Swahaabah (Radhiya Allaahu ‘anhum), mahali watakapokufa maadui mbali
mbali, kabla hata vita havijaanza. Alikuwa akisema:
((Hapa ataanguka fulani, hapa atauliwa fulani …))
Alipokuwa
akiwapanga watu wake, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa
sallam) alipita mbele ya Sawad bin Aziya (Radhiya Allaahu ‘anhu)
akamgonga kwa nguvu tumboni pake kwa bapa la mkuki na kumwambia:
((Simama vizuri ewe Sawaad.))
Sawad (Radhiya Allaahu ‘anhu) akamwambia:
“Umeniumiza
ewe Mtume wa Allaah na Mola wako amekuleta kwa ajili ya kusimamisha
haki na uadilifu, kwa hivyo uniache na mimi nikulipizie katika mwili
wako”.
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akalifunua tumbo lake na kumwambia:
((Jilipie kisasi chako.))
Sawad akalikumbatia tumbo la Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) huku akilibusu.
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia:
((Kipi kilichokupeleka ukafanya hivi?))
Akasema:
“Ewe Mtume wa Allaah, mambo ndiyo kama unavyoyaona na mimi nilipenda tendo langu la mwisho kabla sijafa liwe kuugusa mwili wako”.
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamuombea du’ah nzuri.
Baada ya kuwapanga watu wake sawa na kuwataka wasianze kupigana mpaka atowe amri yake, akawaambia:
((Wakianza kuja, anzeni kuwarushia mishale na msitoe panga zenu mpaka wawe karibu nanyi kabisa.))
Jeshi La Watu Wa Makkah
Usiku
ule baadhi ya Makuraysh walijaribu kutaka kunywa maji penye mahodhi
waliyoyajenga Waislam, lakini kila aliyejaribu kuyasogelea aliuliwa,
isipokuwa mtu mmoja aitwae, Haakim bin Hizaam, huyu aliachwa na
alisilimu baadaye na akawa Mwislam mwema.
Makuraysh walimtuma ‘Umair bin Wahaab Al-Jahamiy aende kuchunguza nguvu za jeshi la Waislam. Akawa anazunguka mbali na jeshi hilo akiwa juu ya farasi wake, huku na kule, kisha akarudi kwa wenzake na kuwaambia:
“Jeshi lao ni kiasi cha watu mia tatu na zaidi kidogo, lakini naona kesho balaa litakuwa kubwa sana,
maana watu hawa hawana pa kukimbilia, na hawana cha kupoteza, wanajuwa
kuwa wao watauliwa tu. Hawana isipokuwa panga zao tu, na nyuma yao
jangwa tupu, kwa hivyo inaelekea watapigana kwa ushujaa na hawatokubali
mmoja wao auliwe bila ya yeye naye kuuwa mtu mmoja kati yenu, kwa hivyo
tizameni wenyewe”.
Pakatokea mzozo mkubwa baina ya Makuraysh, wengi wao wakamtaka Abu Jahal arudi na jeshi lake Makkah,
na kwamba hapakuwa na haja ya kupigana na jeshi la Muhammad (Swalla
Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Lakini Abu Jahal kwa haraka
akafanikiwa kuuzima moto huo na kumlaumu ‘Umair kwa kumwambia:
“Umeingiwa
na hofu wewe ulipouona uso wa Muhammad, pale ulipokuwa ukiyachunguza
majeshi yake ndiyo sababu ukaja na uwoga na unataka kututia na sisi
uwoga huo.”
Akaweza
kuwaingiza watu wake mori wa vita, kwa kuwakumbusha kuuliwa kwa ‘Amru
bin Al-Hadhramiy na kwamba lazima walipe kisasi chake.
Majeshi Yanakabiliana
Asubuhi
ya siku ya Ijumaa, tarehe kumi na saba, mwezi wa Ramadhaan, mwaka wa
pili baada ya Hijrah, majeshi hayo mawili yakapambana. Allaah aliwafanya
Waislam walione jeshi la makafiri kuwa ni wachache ili wasiwaogope na
akawafanya makafiri wawaone Wasilam pia kuwa ni wachache ili wasiwaogope
na kurudi nyuma, yote haya ili kitendeke kile anachokitaka Subhaanahu
wa Taala.
Allaah anasema:
{{Na
mlipo kutana akakuonyesheni machoni mwenu kuwa wao ni wachache, na
akakufanyeni nyinyi ni wachache machoni mwao, ili Allaah atimize jambo
lilio kuwa liwe. Na mambo yote hurejezwa kwa Allaah. Enyi mlio amini!
Mkikutana na jeshi, basi kueni imara, na mkumbukeni Mwenyezi Mungu sana ili mpate kufanikiwa.}} [Suuratul-Anfaal: 44-45]
Majeshi
yalipoanza kupambana, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa
sallam) akaingia ndani ya lile hema, yeye na Abu Bakar (Radhiya Allaahu
‘anhu) peke yao, na hapana mwengine aliyeingia humo gheri yao, Mtume
(Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akaanza kuomba du’ah huku
akisema:
((Mola
wangu hawa Makureshi wamekuja kwa jeuri na kiburi chao, wakikupinga na
kumkadhibisha Mtume wako. Mola wangu nitimizie yale uliyoniahidi, Mola
wangu watu hawa wakishindwa leo, basi hutaabudiwa tena…))
Kila vita vikipamba moto, naye huongeza kuomba du’ah.
Akawa
anaendelea kuomba mpaka nguo yake ya begani ikamwanguka, na As-Swiddiik
(Radhiya Allaahu ‘anhu) akaiokota na kumvisha tena huku akimwambia:
((Inatosha ewe Mtume wa Allaah, ushamuomba vya kutosha Mola wako.))
Kisha
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasimama penye
mlango wa ‘Ariish aliyojengewa akawa anaisoma aayah ya 45 ya
Suuratul-Qamar:
“Sayuhzamu l jam-‘u wa yuwalluwna ddubur”
Na maana yake ni:
{{Wingi wao huo karibuni watashindwa na wataendeshwa mbio na watageuza migongo.}}
Mubaraza (Mapigano) Kabla Ya Mapambano
Kwa
kawaida kabla ya kuanza mapambano, Waarabu walikuwa na tabia ya
kuanzisha Mubaraza, na maana yake ni, mtu mmoja au wawili au watatu
hutoka kutoka kila upande na kuanza kupambana wao kwanza kila mmoja na
mwenzake mpaka wauwane, kisha vita ndiyo vinaanza. Mapigano haya kwa
kawaida ndiyo yanayotowa picha ndogo ya mwisho wa vita.
Katika
mapigano haya, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)
aliwatoa upande wa Waislam, ‘Aliy bin Abi Twaalib, Ubaidah bin Haarith
na Hamzah (Radhiya Allaahu ‘anhum). Kwa upande wa makafiri wakatoka,
Utbah na ndugu yake Shaibah, na Al-Waliid mtoto wa Utbah – wote wakiwa
watu wa aila moja. Katika mapigano hayo, Hamza (Radhiya Allaahu ‘anhu),
alimuuwa mpinzani wake Shaibah, na ‘Aliy (Radhiya Allaahu ‘anhu),
alimuuwa mpinzani wake Al-Waliid bila taabu na bila kuchukuwa muda
mferu. Ama Ubaidah (Radhiya Allaahu ‘anhu), yeye na mpinzani wake, wote
wawili waliumizana wakaanguka chini, lakini ‘Aliy na Hamzah (Radhiya
Allaahu ‘anhu) wakawahi kumrukia Al-Waliid na kumuuwa kisha wakamuokoa
mwenzao na kumvuta nyuma na kumrudisha katika kambi ya Waislam. Lakini
hatimaye kutokana na damu nyingi iliyomwagika alifariki dunia siku nne
baada ya tukio la Badr kwa homa ya manjano.
Mashambulio
Mapigano
haya yalimaanisha mwisho mbaya wa jeshi la washirikina. Kwa sababu
wamepoteza watatu katika wapiganaji wao wakubwa kwa mpigo mmoja, na kwa
kawaida Waarabu walikuwa na itikadi ya kuvipima vita kutokana na
mapigano ya mwanzo (Mubaraza). Kwa ajili hiyo wakawavamia Wasilam kwa
ghadhabu na kwa nguvu zao zote, na Waislam wakapambana nao kwa ujasiri
mkubwa kabisa.
Wakati huo Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akawatokea Waislam na kuwaambia:
((Naapa
kwa yule ambaye nafsi ya Muhammad ipo mikononi pake, yeyote
atakayepigana nao leo kisha akauliwa akiwa katika hali ya subra, bila ya
kurudi nyuma, basi Allaah atamuingiza Peponi.))
‘Umair bin Al-Hamaam (Radhiya Allaahu ‘anhu) aliyekuwa akila tende, mara baada ya kusikia maneno hayo akasema:
“Hivyo baina yangu na baina ya kuingia Peponi ni kupigana na kuuliwa na watu hawa na tende hii ndiyo inanichelewesha?”.
Akazitupa tende zake, akaingia vitani, akapigana mpaka akauliwa.
Mtume
(Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasogea mbele, akachota
gao la mchanga, akawakabili Makuraysh, kisha akasema:
((Zimeangamia nyuso zao.))
Kisha akawarushia nao.
Allaah Anasema:
{{Hamkuwauwa
nyinyi lakini Allaah ndiye aliye wauwa. Na wewe hukutupa, pale
ulipotupa, walakini Allaah ndiye aliye tupa, ili awajaribu Waumini
majaribio mema yatokayo kwake. Hakika Allaah ndiye Msikizi na Mjuzi.
Ndio hivyo! Na hakika Allaah ni Mwenye kudhoofisha vitimbi vya
makafiri.}} [Suuratul-Anfaal: 17 18]
Kisha Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akawaambia Swahaabah zake (Radhiya Allaahu ‘anhum):
((Wakazieni vizuri, inukeni muifuatilie Pepo ambayo upana wake tu ni sawa na mbingu na ardhi.))
Kisha akaondoka na kurudi penye ‘Ariish yake ile aliyojengewa.
Mapambano
makali yakaanza baina ya makundi mawili hayo, na ushindi ukawa wa
Waislam. Wakauliwa waliouliwa katika vigogo vya Makuraysh na wakatekwa
waliotekwa.
Haya ni mapambano ya pekee ambayo Malaika walishiriki, akiwemo Jibriyl ('Alayhis Salaam). Baadhi ya Maswaahabah walisema:
“Siku hiyo tulikuwa tukiona vichwa vikikatika tu na kuruka huku na kule, hatujuwi nani anayevikata”.
{{Mlipo
kuwa mkimuomba msaada Mola wenu Mlezi, naye akakujibuni kuwa: Kwa
yakini Mimi nitakusaidieni kwa Malaika alfu wanao fuatana mfululizo.
Na
Allaah hakufanya haya ila kuwa ni bishara na ili nyoyo zenu zituwe. Na
haupatikani ushindi ila kutoka kwa Allaah. Hakika Allaah ni Mwenye
nguvu, na Mwenye hikima.
Alipo
kufunikeni kwa usingizi uwe ni uaminisho kutoka kwake, na
akakuteremshieni maji kutoka mbinguni ili kukusafisheni kwayo na
kukuondoleeni uchafu wa Shaytwaan, na kuzipa nguvu nyoyo zenu, na kuitia
imara miguu yenu.
Mola
wako Mlezi alipo wafunulia Malaika: Hakika Mimi ni pamoja nanyi, basi
watieni nguvu walio amini. Nitatia woga katika nyoyo za walio kufuru.
Basi wapigeni juu ya shingo na wapigeni kwenye kila ncha za vidole.
Hayo ni kwa sababu wamemuasi Allaah na Mtume wake. Na mwenye kumuasi Allaah na Mtume wake basi Allaah ni Mkali wa kuadhibu.
Ndio hivyo! Basi ionjeni! Na bila ya shaka makafiri wana adhabu ya Moto.}}
[Suuratul-Al Anfaal: 9–14]
Kifo Cha Abu Jahal
Abu Jahal alipoona majeshi yake yanaanza kurudi nyuma akawa anapiga kelele huku akisema:
“Wasikutisheni
hao, msiogope kwa kuwa ‘Utbah na Al-Waliid wameuliwa, leo hatuondoki
hapa mpaka turudi nao Makkah tukiwa tumewafunga kamba wote hawa”.
Anasema
‘Abdur-Rahmaan bin Auf kuwa nilipokuwa nimesimama vitani nikageuka
kutizama kuliani kwangi na kushotoni kwangu nikidhania watakuwepo watu
wazima ili tusaidiane vita vikipamba moto. Lakini nikavunjika moyo
nilipowaona watoto wadogo wawili wamesimama mmoja kushotoni pangu na
mwengine kuliani pangu. Nikasema moyoni mwangu: “Leo sina pa kuegemea”.
Yule mtoto aliye kuliani pangu akaniomba niiname apate kuniuliza ili
yule mwenzake asisikie. Akaniuliza:
“Ami! Yupi kati yao Abu Jahal?”
Nikamuuliza:
“Ewe mwana wa ndugu yangu, unamtakia nini Abu Jahal?”
Akanijibu:
“Nimesikia kuwa anamtukana Mtume wa Allaah, WaLlaahi nikimuona basi sitomwacha, lazima nitamuuwa”
Yule mtoto aliye kushotoni pangu akaniuliza vile vile kama mwenzake, na nikamjibu kama mwenzake na akasema yale yale aliyosema mwenzake.
Nilipomuona Abu Jahal nikawaambia:
“Yule rafiki yenu mnayemtafuta”
Wakamkimbilia na panga zao, wakamvamia na kumpiga kwa mapanga mpaka wakamuuwa.
Mara
baada ya kumuuwa wakakimbia mpaka kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa
aalihi wa sallam) na kumpa habari njema hizo. Mtume (Swalla Allaahu
‘alayhi wa aalihi wa sallam) akawauliza:
((Yupi kati yenu aliyemuuwa?))
Kila mmoja akasema:
“Mimi ndiye niliyemuuwa”.
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akawaambia:
((Hebu nione panga zenu.))
Baada ya kuzitizama akasema:
((Kweli, nyote mmeshirikiana katika kumuuwa.))
Kisha akasema:
“Allaahu laa ilaaha illa huwa” mara tatu.
Kisha akasema:
“Alhamdu lillaahi lladhiy swadaka wa’adahu, wa naswara ‘abdahu, wa hazama l-ahazaaba wah–dahu”.
Katika
vita hivi waliuliwa Makuraysh sabiini, na wengine sabiini walitekwa, na
katika waliouliwa alikuwemo Firauni wa Umma huu – Abu Jahal na ‘Utbah
bin Rabia na mwanawe Al-Waliyd na nduguye Shaiba na wengi wengineo.
Na
miongoni mwa mateka alikuwemo Al-‘Abbaas – Ami yake Mtume (Swalla
Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na ‘Aqiyl bin Abi Twaalib, na
Nawfal bin Al-Haarith, na Umayya bin Khalaf na wengi wengineo.
Hawa wote walikuwa upande wa Makuraysh.
Mizoga Ya Makafiri
Baada ya vita kumalizika, Waislam wakawazika wenzao waliokufa Mashahid na idadi yao
walikuwa kumi na nne. Kisha wakaichukua mizoga ya Mushrikina na kuitupa
katika kisima kisichokuwa na maji kilicho karibu na mahali palipotokea
mapambano hayo.
Mtume (Swalla Allaahu ‘Alayhi Wa Aalihi Wa Sallam) Anawafokea Maadui Wake
Usiku
wa manane Waislam walimsikia Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa
sallam) akiwa amesimama penye kile kisima walichotupa mizoga ya
Mushrikina akiwafokea huku akisema:
((Enyi
mlio kisimani, ubaya ulioje mliokuwa nao jamaa zangu nyinyi kwa Mtume
wenu! Mlinikadhibisha wakanisadiki watu (kweli), mkanitoa katika mji
wangu, wakanipokea watu (kweli), mkanipiga vita wakanisaidia watu
(kweli). Je! Sasa nyinyi mmekwisha pata kweli yale aliyokuahidini Mola
wenu? Ama mimi nimepata kweli yale aliyoniahidi Mola wangu.))
Maswahaabah wakamuuliza:
“Ewe Mtume wa Mwenyei Mungu unazungumza na watu washakuwa mizoga?”
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema:
((Wao wanasikia kuliko nyinyi haya niliyowaambia isipokuwa hawawezi kujibu.))
Bishara Njema
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliwatuma watu kwa haraka sana waende Madiynah ili kuwapa habari njema hizo za ushindi wao juu ya Makafiri.
Usaamah bin Zayd (Radhiya Allaahu ‘anhu) anasema:
“Zilitufikia
habari tulipokuwa tukimzika Bibi Ruqayya (Radhiya Allaahu ‘anha) binti
wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), mke wa ‘Uthmaan
bin ‘Affaan (Radhiya Allaahu ‘anhu).
Zayd bin Harithah (Radhiya Allaahu ‘anhu) alipoingia msikitini, watu walimzunguka huku akisema kwa furaha:
“Amekwisha
uliwa ‘Utbah bin Rabia na Shaibah bin Rabia na Abu Jahal.” Akawa
anawataja mmoja mmoja katika vigogo vya Makuraysh waliouliwa Badr.
Zayd (Radhiya Allaahu ‘anhu) anasema:
“Nikamuuliza, Babangu unasema kweli?”
Akanijibu:
“Naam, kweli mwanangu”
Kuondoka Mji Wa Badr
Mtume
(Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), akaondoka hapo Badr
pamoja na mateka wao na ngawira zao na alipofika karibu na Madiynah
alisimamisha msafara katika bonde la Safra akawagawia Waislam ngawira yao
sawa sawa na kila anapoukaribia mji wa Madiynah, alikuta makundi kwa
makundi ya watu waliosimama pembezoni mwa njia wakimpongeza.
Allaah anasema:
{{Kumbukeni
pale mlipo kuwa nyinyi kwenye ng'ambo ya karibu ya bonde, na wao wakawa
ng'ambo ya mbali, na msafara ulipo kuwa chini yenu. Na ingeli kuwa
mmeagana mngeli khitalifiana katika miadi. Lakini (mkakutana) ili Allaah
atimize jambo lilio kuwa lazima litendeke, kwa sababu aangamie wa
kuangamia kwa dalili zilizo dhaahiri, na asalimike wa kusalimika kwa
dalili zilizo dhaahiri. Na Allaah ni Mwenye kusikia Mwenye kujua.
Kumbuka
alipo kuonyesha usingizini mwako kwamba wao ni wachache - na lau angeli
kuonyesha kuwa ni wengi, mngeli ingiwa na woga, na mngeli zozana katika
jambo hilo.
Lakini Allaah kakuvueni. Hakika Yeye ni Mwenye kuyajua yalio vifuani.}}
[Suuratul-Anfaal: 42–43]
Matukio Mbali Mbali
Baada
ya kumalizika vita, Masa-‘ab bin ‘Umair (Radhiya Allaahu ‘anhu)
alimuona ndugu yake Abu ‘Aziiz aliyekuwa upande wa makafiri akiwa
ametekwa na amefungwa kamba. Akamwambia yule aliyemfunga kamba:
“Mfunge vizuri huyo kwa sababu mamake ana mali nyingi, anaweza kumkomboa”
Ndugu yake akamwambia:
“Huko ndiko kuwapa usia mwema ndugu yangu?”
Mas-‘ab akamwambia:
“Huyu aliyekukamata ni ndugu yangu kuliko wewe”.
Baada ya kutupwa maiti za makafiri kisimani, Abu Hudhaifah (Radhiya Allaahu ‘anhu) mwana wa ‘Utbah bin Rabia alikuwa na huzuni sana. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamuuliza:
((Unaona vibaya juu ya babako, (kwa vile ni kafiri na ametupwa kisimani na wenzake)?))
Abu Hudhaifah akasema:
“Laa wallahi, ewe Mtume wa Allaah, isipokuwa babangu alinifanyia fadhila nyingi sana na alikuwa akinipenda, nikadhani kwa ajili hiyo naye atasilimu, na nilipomuona kuwa amekufa kafiri, ndio nikahuzunika”.
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamuombea du’ah kumtakia kila la khayr.
Wale
watoto wawili waliomuuwa Abu Jahal nao wana kisa chao. Walipokuja
kutaka kushiriki katika vita, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa
sallam) akamkubali ndugu mkubwa na akamkataa yule mdogo.
Yule mdogo akasema:
“Ewe Mtume wa Allaah, kwa nini umemkubali kaka yangu na mimi hukunikubali?”
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia:
((Kwa sababu umri wako ni mdogo.))
Akasema:
“Lakini sisi siku zote tukipigana mieleka, mimi namshinda kaka yangu.”
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema:
((Hebu piganeni mieleka nikuoneni.))
Wakapigana na yule mdogo akamshinda mkubwa wake, kisha Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamkubali.
‘Umar bin Khatwaab (Radhiya Allaahu ‘anhu) alimuuwa siku hiyo mjomba wake Al’Aas bin Hisham, aliyekuwa upande wa makafiri.
Hitimisho
Allaah anasema:
{{Na
Allaah alikunusuruni katika (vita vya) Badr. Hali nyinyi mlikuwa
dhaifu. Basi mcheni Allaah ili ili mpate kushukuru (kila wakati kwa
neema zinazokujieni).}} [Suuratul-‘Imraan: 123]
Allaah,
hapa anatujuulisha kuwa Yeye tu ndiye wa kutegemewa, na si viumbe vyake
dhaifu. Yeye tu ndiye mwenye kuleta ushindi, na anayestahiki
kukimbiliwa wakati wa dhiki, badala ya kuwakimbilia viumbe vyake dhaifu.
Na hili ni somo kwa wale ndugu zetu ambao mara wanapokumbwa na tatizo dogo, wanaikimbilia ile du’ah ya Hal Badiri (Ahlul-Badr) ambayo ndani yake mna majina ya Maswahaabah walioshiriki katika vita hivyo, na kuomba msaada kutoka kwao.
Allaah anasema:
{{Na Allaah alikunusuruni katika (vita vya) Badr. Hali nyinyi mlikuwa dhaifu.}}
Allaah
aliwapa ushindi Waislam katika vita hivi juu ya uchache wao, wakati
katika vita vya Hunain, kwa mara ya mwanzo Waislam walipigana vita idadi
yao
ikiwa kubwa zaidi kuliko ya makafiri lakini waliendeshwa mbio na
makafiri mpaka Allaah alipowateremshia utulivu wake. Hakupata Mtume
(Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kutoka na jeshi kubwa
kuliko la siku hiyo, alitoka na watu elfu kumi na mbili, hata Waislam
wakawa wanasema:
“Hatutoshindwa leo kwa sababu ya uchache wetu” [kwa vile tuko wengi leo hatutoshindwa]
Allaah anasema:
{{Bila
shaka Allaah amekunusuruni katika mapigano mengi, na siku ya Hunaiyn
(pia) ambapo wengi wenu ulikupandisheni kichwa, lakini haukukufaeni
chochote, na ardhi ikawa dhiki juu yenu ingawa ilikuwa yenye wasaa,
kisha mkageuka mkarudi nyuma.}} [Suuratut-Tawbah: 25]
Anasema Imaam Ahmad bin Hanbal (Rahimahu Allaah) kuwa:
“Katika vita vya Yarmuuk, ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu) aliwaambia Waislam:
“Mtakapotaka msaada katika vita hivi, basi muandikieni Abu ‘Ubaidah”.
Vita vilipoanza, wakamuandikia Abu ‘Ubaidah aje kuwasaidia, na kwamba wako katika hatari. Abu ‘Ubaidah akawaandikia hivi:
“Imenifikia
barua yenu ikitaka msaada kutoka kwangu, lakini mimi nitakujulisheni
yule atakayeweza kukusaidieni mkapata ushindi kuliko nitakavyoweza
kukusaidieni mimi; - Allaahu ‘Azza wa Jallah – ombeni msaada kutoka
kwake mkitaka kupata ushindi. Kwa sababu Muhammad (Swalla Allaahu
‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipewa ushindi na Allaah siku ya Badr
akiwa na watu wachache kuliko nyinyi. Itakapokufikieni barua yangu hii,
piganeni nao na wala msiniandikie mimi.”
Anasema Iyaadh Al-‘Ash-ary (Radhiya Allaahu ‘anhu), mwenye kuisimulia Hadiyth hii:
“Tukapambana nao na tukawashinda, na tukapata ngawira nyingi siku hiyo”.
0 Comments