BISMILLAH RAHMANI RAHIM
Abubakar (Radhiya Allaahu ‘anhu) alikua akimfahamu na akimuelewa vizuri sahibu yake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)kupita Masahaba wote (Radhiya Allaahu ‘anhu), na alikuwa na uhakika kuwa yote anayoyasema ni Wahyi utokao kwa Mola wake Subhanahu wa Taala.
Katika mwaka wa tano baada ya kuhamia
Madina, Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa
sallam)pamoja na Masahaba wake (Radhiya Allaahu ‘anhu) waliondoka Madina
kuelekea Makkah kwa nia ya kufanya Umra. Wakapiga kambi karibu na mji wa Makkah
mahali panapoitwa Al Hudaibiyya, kisha wakamtuma Othman bin Affan (Radhiya
Allaahu ‘anhum) ende Makkah kuwajulisha Makureshi juu ya nia yao hiyo na kwamba
hawakuja kwa nia ya kupigana vita.
Makureshi wakapeleka majeshi yao
kutaka kuwazuia, na baada ya majadiliano marefu yaliyopita baina yao, wakaamua
kumtuma mjumbe wao aitwaye Suhail bin Amr, aliyeweza kufikia makubaliano na
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), yaliyokuja kujulikana kwa
jina la Makubaliano ya Al Hudaibiyya.
Yafuatayo ni baadhi ya shuruti za makubaliano hayo;
· Waislamu warudi Madina mwaka huu na
wafanye Umra mwaka ufuatao.
· Waislamu wanalazimika kumrudisha kwa
Makureish yoyote atakayeingia katika dini yao na kukimbilia Madina, lakini
Makureshi hawalazimiki kumrudisha atakayetoka katika Uislamu na kukimbilia
Makkah.
· Wasipigane vita kwa muda wa miaka
kumi, na wawe wanaendeana watakavyo.
Kabla ya mkataba huo kutiwa sahihi
(saini), Waislamu walistukia kijana mmoja aitwae Aba Jandal aliyesilimu lakini
alikuwa akiishi Makkah akipitishwa mbele yao akiwa amefungwa minyororo shingoni
huku na kubebeshwa jiwe kubwa akipiga kelele akiwaomba Waislamu wenzake
wamuokoe kutokana na adhabu hiyo.
Kijana
huyu Aba Jandal ni mwana wa Suhail, mjumbe wa Makureish katika sulhu hiyo.
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa
aalihi wa sallam), alimuonea huruma kijana huyo, akamtaka Suhail amruhusu
wamchukuwe kwa sababu mkataba ulikuwa bado haukutiwa saini wala haukupigwa
mhuri, lakini baba yake alikataa na kutishia kuuvunja mkataba na kuanzisha vita
ikiwa watajaribu kumchukua kwa nguvu.
Abu
Jandal alikuwa akipiga kelele huku akisema;
"Enyi
Waislamu wenzangu! mnaniacha nirudi kwa washirikina hawa na mimi nataka himaya
yenu?"
Mtume(Swalla
Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia ;
"Kuwa
na subira, na Mwenyezi Mungu atakujaalia utoke katika janga hilo".
Omar
bin Khattab (Radhiya Allaahu ‘anhu) hakuweza kuyastahamilia haya, akamuendea
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)na kumuuliza;
"Ewe
Mtume wa Mwenyezi Mungu, wewe si Mtume wa Haki?"
Mtume
(Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)akamjibu;
"Ndiyo,
ewe Omar".
Akauliza
tena;
"
Kwa nini basi tunakubali kujidhalilisha?"
Mtume
(Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)akamwambia;
"Ewe
Omar, mimi ni Mtume wa Mwenyezi Mungu, siwezi kumuasi, na Yeye ndiye
atakayetunusuru".
Omar
(Radhiya Allaahu ‘anhu) akauliza;
"Si
ulituahidi kuwa tutakwenda Makkah na tutatufu katika nyumba kongwe?"
Mtume(Swalla
Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)akajibu;
"Nilikwambia
kuwa ni mwaka huu ewe Omar?"
Omar
akajibu;
"La
hukusema hivyo."
Mtume(Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)akasema;
"Utakwenda
Makkah ewe Omar na utatufu penye nyumba."
Omar
pamoja na baadhi ya Masahaba (Radhiya Allaahu 'anhum) hawakuridhika na baadhi
ya masharti yaliyokuwemo ndani ya mkataba ule, wao waliona kuwa Waislamu
wamekubali kujidhalilisha kwa kuyakubali masharti yote ya makafiri, na hii ni
kwa sababu dhahiri yake mkataba huo si mzuri juu ya Waislamu, lakini kwa anayeona
mbali mkataba huo ulikuwa ni ufunguzi mkubwa kwa Waislamu, kama alivyosema
Mwenyezi Mungu katika Suratul Fat-h aya ya mwanzo;
"Bila
shaka tumekwishakupa kushinda kuliko dhahiri"
Mwenyezi
Mungu katika aya hii anatujulisha kuwa kuukubali mkataba huo ni ushindi mkubwa
kwa Waislamu, juu ya kuwa dhahiri yake ni kukubali masharti yote ya makafiri,
na hii ni inatokana na sababu zifuatazo;
1) Kutokana na suluhu hiyo, makafiri
walifungika wasiweze kupigana vita dhidi ya Waislamu muda wa miaka Kumi.
2) Katika muda wote huo Waislmu wakawa
na uwezo wa kujishughulisha na kuieneza dini yao miongoni mwa makabila mengine
ya Bara arabu, pamoja na nchi za Sham.
3) Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla
Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)alituma ujumbe kwa wafalme mbali mbali
4) Wale waliosilimu wasioruhusiwa
kukimbilia Madina kwa ndugu zao Waislamu, ni bora kwao kubaki Makkah kwa ajili
ya kuwalingania watu katika dini ya Kiislam huko Makkah.
5) Makafiri watakaorudi Makkah iwapo
watatoka katika Uislam, hawataudhuru Uislam.
Sababu
hizi na nyinginezo ambazo si wasaa wake huu kuzitaja ni dalili kuwa mkataba huo
undani wake ulikuwa na manufaa makubwa kwa Waislamu, juu ya kuwa dhahiri yake
ni kusalimu amri na kukubali masharti yote ya Makureshi.
Na hii
ndiyo sababu iliyomfanya Omar (Radhiya Allaahu ‘anhu) asiridhike nao, wala
asisimame hapo. Kwani alimwendea pia Abubakar Al Siddiq (Radhiya Allaahu ‘anhu)
na kumuuliza tena masuali yale yale;
"Ewe
Abubakar, Muhammad si Mtume wa Haki?"
Abubakar
(Radhiya Allaahu ‘anhu); "Ndiyo"
Omar
(Radhiya Allaahu ‘anhu); "Tukipambana nao makafiri hawa, si atakayekufa
upande wetu ataingia Peponi na wao wanaingia Motoni?"
Abubakar
(Radhiya Allaahu ‘anhu); "Ndiyo".
Omar
(Radhiya Allaahu ‘anhu); "Kwa nini basi tunakubali kujidhalilisha?"
Abubakar
(Radhiya Allaahu ‘anhu);
"Ewe
Omar, yeye ni Mtume wa Mwenyezi Mungu na hawezi kumuasi, na Mwenyezi Mungu
ndiye atakayemnusuru, kamatana naye kwani Wallahi yupo katika Haki".
Majibu
yale yale ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)kayapata kwa
Abubakar (Radhiya Allaahu ‘anhu), na Mwenyezi Mungu akawateremshia Waislamu
utulivu nyoyoni mwao.
Mwenyezi
Mungu anasema;
"Yeye
ndiye aliyeteremsha utulivu katika nyoyo za Waislamu ili waongezeke imani juu
ya imani yao".
Suratul
Fat-h 4
Omar(Radhiya
Allaahu ‘anhu) alisema baadaye;
"Nikatambua
kuwa ile ndiyo Haki".
Mwaka wa tisa Hijri ndio mwaka ulioitwa
'Mwaka wa Wajumbe' na hii ni kutokana na wajumbe wa makabila mbali mbali ya
kiarabu waliokuja kusilimu mbele ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu
‘alayhi wa aalihi wa sallam).
WABILLAH TAUFIQ
2 Comments
ni notes safi
ReplyDeleteALI MAHMOUD ALI MAKUNDUCHI KUMBINI
shukrani sana, karibu
Delete