ads

KIBURI

                               1.
              Ikiwa umeumbika, kwa uzuri ulotimu,
              Au umetajirika, pesa nyingi tasilimu,
              Kiburi ukajivika. vazi lenye uhasimu,
              Kiburi kwa mwanadamu, Si kitu chema kiburi.

                               2.  
              Mola mwenye madaraka, ndiye mwenye kurehemu
              Kukupa na kukupoka, ndiyo kaziye Karimu.
              Humpa anayetaka, jamii ya wanadamu,
              Kiburi kwa mwandamu, Si kitu chema kiburi.

                                  3. 
              Waringa na hekaheka, wenzio kuwashutumu,
              Kwa kuziona fanaka, Mola alokukirimu,
              Wazimu ukakushika, ukawa huna fahamu,
              Kiburi kwa mwanadamu, Si kitu chema kiburi.

                                4. 
              Kwanza ziondowe taka, nduguzo kuwahasimu.
              Usiipige mipaka, wazazi kuwalaumu,
              Zinduka ndugu zinduka, wewe Sio marehemu,
              Kiburi kwa mwanadamu, Si kitu chema kiburi.

                               5.  
              Kiburi ni mbaya shuka, kuivaa ni haramu.
              Yapendeza kukumbuka, msemo wenye kudumu,
              Mpanda ngazi hushuka, alacho kikawa sumu.
              Kiburi kwa mwanadamu, Si kitu chema kiburi.

                               6. 
              Na mwanadamu yataka, bongo lake kuhitimu.
              Wazee walotamka, maneno yalo muhimu,
              Kulonama huinuka, laini huwa kigumu.
              Kiburi kwa mwanadamu, Si kitu chema kiburi.

                                7. 
              Kituoni nimefika, nazikomesha nudhumu,
              Yatosha naloandika, kiburi ni jahanamu,
              Ashikae atashika, asoshika Si lazimu,
              Kiburi kwa mwanadamu, Si kitu chema kiburi.
By - ABDALA KIZERE

Post a Comment

0 Comments