ads

SHAIRI: TOA KAMBA MGUUNI




1.         Naanza kwa rahmani, njema sifa za manani
Jambo lililo mwanzoni, salama yangu shikeni
Leo siku ya ugeni, moyoni hadi chuoni
Furaha iso kifani, wageni karibieni

2.         Karibu ukumbuni pamoja kufurahia
Karibu sana chuoni, pamoja kusherekea
Yamkini furahani, pamoja tumeridhia
Toa Kamba mguuni, wewe tena si mgeni

3.         Furaha yangu moyoni, japo najenga huzuni
Tunaagana chuoni, hali yangu sio duni
Nimejifunza mageni, wasia ninakupeni
Toa Kamba mguuni, wewe tena si mgeni

4.         Toa Kamba mguuni, zitoe nongo machoni
Mwalimu kwenda shuleni, taaluma iso duni
Kawafundisha mageni, injinia na rubani
Toa Kamba mguuni, wewe tena si mgeni

5.         Wasomi wetu wa sasa, mwalimu kafanya kazi
Tukawapige msasa, kwa nidhamu na malezi
Ubaguzi wenye visa, mwalimu ndie mkwezi
Toa Kamba mguuni, wewe tena si mgeni

6.         Wewe tena si mgeni, mazuri kuzingatia
Watoto walo shuleni, tamaa kutoitia
Wakinge kwa mitihani, uzinifu na udhia
Toa Kamba mguuni, wewe tena si mgeni

7.         Nadhani mmefahamu, hili pia ongezea
Taifa bila mwalimu, madhila yatatokea
Nenda ukawe hakimu, jamii kuizindua
Toa Kamba mguuni, wewe tena si mgeni

8.         Ualimu kwako nembo, popote kuangazia
Usije zidisha tambo, kumbuka kujitolea
Usikunase urimbo, pabaya kujinasua
Toa Kamba mguuni, wewe tena si mgeni

9.         Maisha yetu chuoni, changamoto si kadhia
Kuifeli mitihani, mazingira kuzowea
Chuoni si utumwani, wafalme tutakua
Toa Kamba mguuni, wewe tena si mgeni

10.       Ndugu zetu twawaaga, nyumbani twajirudia
Mazuri yetu kuiga, mabaya kutochukua
Nidhamu sio uoga, walimu kuwasikia
Toa Kamba mguuni, wewe tena si mgeni

11.       Sio mwisho wa kalmia, tamati nimefikia
Nina maliza kusema, ujumbe nimeutoa
Kaijengeni heshima, pamoja kuzingatia
Toa Kamba mguuni, wewe tena si mgeni


Mtunzi: Mwinyi Abdallah
Phone: 0655895599
Blog: maalimupacha.blogspot.com

download hapa Shairi: Toa kamba

Post a Comment

0 Comments