ads

SHAIRI: KWAHERINI TWAWAAGA





1.      Salamu na inudhumu, ujumbe nawaletea
Namshukuru rahimu, uzima kutupatia
Kwetu hili ni jukumu, uislamu kukua
Leo kwenu wahitimu, hongera nawapatia

2.      Karibuni barazani, karibuni ukumbini
Ninayo mengi moyoni, wahitimu sikieni
Hili lanipa huzuni, japo moyoni si geni
Ndugu zangu kwaherini, dunia bado chuoni

3.      Dua bado chuoni, dunia bibi harusi
Muloyapata chuoni, yatumieni kiasi
Dunia ni safarini, musipate ukakasi
Yatupasa jamiini, tukayatoe maasi

4.      Nawaasa ndugu zangu, acha kufuga mapenzi
Mila zile za kizungu, miaka tele mpenzi
Umewapanga mafungu, kwa enzi tangia enzi
Hautaki bwana mungu, uchumba huu wa enzi

5.      Ndoa weka msitari, kwako ni nguzo imara
Ndoa ndie mshauri, kupata kilichobora
Ndoa ninaihubiri, ndoa kwako ndio dira
Oeni mpate kheri, ndoa kwetu ni stara

6.      Vijana nawahusia, ishikeni sana dini
Vikaoni hudhuria, uisome qurani
Sunna za wetu nabia, zifwate bila mizani
Mola atajaalia, akhera wende peponi

7.      Daima shikamaneni, umoja ule wa safu
Musingoje mitihani, kusaka umaarufu
Wadada jihifadhini, daima muwe nadhifu
Sina budi kwaherini, safari yetu ni ndefu

8.      Anasa ndugu anasa, iepuke maishani
Anasa ndugu anasa, maishayo kuwa duni
Anasa ndugu anasa, kijana shikana dini
Anasa ndugu anasa, nawaaga kwaherini

9.      Tamati nimefikia, huzuni imenifika
Ujumbe nilokugea, ni vyema ukaushika
Dini mukizingatia, mengi yatawaepuka
Kwaheri nawapatia, kwaheri isiyoshaka

Mtunzi: MwinyiAbdallah
0657 895 599 
email: mwinyiabdallah2012@gmail.com 

Download shairi hapa shairi: Kwaherini Twawaaga

Post a Comment

0 Comments