ads

MUONGOZO KATIKA KUJIANDAA NA MAISHA YA NDOA



UTANGULIZI     
         Lengo na madhumuni ya mwongozo huu ni kujaribu kwa kiasi kidogo tu kutoa ufafanuzi wa jinsi ya kujiandaa na suala zima la ndoa na ikiwa kama ni mwongozo ambao utaangalia zaidi katika upande wa kidini wakati wa maandalizi ya kuchumbia pamoja na kugusia sehemu nyengine muhimu.

UMUHIMU WA NDOA

Moja katika alama zake Allah Subhaanahu Wata’ala ni kuisimamia ndoa na kuiwekea taratibu zake maalum katika sheria tokea nguzo, adabu, fadhila na hekima zake. Tukiangalia kitabu chake Allah Subhaanahu Wata’ala – Qur’aan tunaona jinsi ilivyotudhihirishia mambo haya katika sehemu tofauti
na kwa mfumo maalum ambayo ni Qur’aan pekee ingeliweza kuifafanua katika sura hii.
Miongoni mwa mambo ambayo Qur’aan inazungumzia juu ya ndoa ni 

1) Kuiamrisha
Kama anavyosema katika Suuratu Nnisaa/3
فَانكِحُواْ مَا طَابَ لَكُم مِّنَ النِّسَاء
Basi oeni mnao wapenda katika wanawake

Suratul Nnuur/32
وَأَنكِحُوا الْأَيَامَى مِنكُمْ وَالصَّالِحِينَ مِنْ عِبَادِكُمْ وَإِمَائِكُمْ 
Na waozeni wajane miongoni mwenu na wema katika watumwa wenu na wajakazi wenu

2 Kuihamasisha

Kama anavyosema Allah Subhaanahu Wata’ala katika Arra’ad/38
وَلَقَدْ أَرْسَلْنَا رُسُلاً مِّن قَبْلِكَ وَجَعَلْنَا لَهُمْ أَزْوَاجًا وَذُرِّيَّةً
Na hakika Sisi tulikwisha watuma Mitume kabla yako, na tukajaalia wawe na wake na dhuriya

3 Huleta utajiri na wepesi katika maisha kama anavyosema katika Annuur/32
إِن يَكُونُوا فُقَرَاء يُغْنِهِمُ اللَّهُ مِن فَضْلِهِ وَاللَّهُ وَاسِعٌ عَلِيمٌ
Wakiwa mafakiri Allah atawatajirisha kwa fadhila yake. Na Allah ni Mwenye wasaa Mwenye kujua

4 Ni njia ya kukiendeleza kizazi katika ardhi Annahl/72
وَاللّهُ جَعَلَ لَكُم مِّنْ أَنفُسِكُمْ أَزْوَاجًا وَجَعَلَ لَكُم مِّنْ أَزْوَاجِكُم بَنِينَ وَحَفَدَةً وَرَزَقَكُم مِّنَ الطَّيِّبَاتِ أَفَبِالْبَاطِلِ يُؤْمِنُونَ وَبِنِعْمَتِ اللّهِ هُمْ يَكْفُرُونَ
Na Allah amekuumbieni wake katika jinsi yenu, na akakujaalieni kutoka kwa wake zenu wana na wajukuu, na akakuruzukuni vitu vizuri vizuri.Basi je, wanaamini upotovu na wanazikataa neema za Allah?
5 Ni njia ya kupatikana utulivu, stara, mapenzi na kuoneana huruma. Arruum/21
وَمِنْ آيَاتِهِ أَنْ خَلَقَ لَكُم مِّنْ أَنفُسِكُمْ أَزْوَاجًا لِّتَسْكُنُوا إِلَيْهَا وَجَعَلَ بَيْنَكُم مَّوَدَّةً وَرَحْمَةً إِنَّ فِي ذَلِكَ لَآيَاتٍ لِّقَوْمٍ يَتَفَكَّرُونَ
Na katika Ishara zake ni kuwa amekuumbieni wake zenu kutokana na nafsi zenu ili mpate utulivu kwao. Naye amejaalia mapenzi na huruma baina yenu. Hakika katika haya bila ya shaka zipo Ishara kwa watu wanaofikiri.
6 Huunganisha koo kufikia kuweza kurithiana kati ya mume na mke. Annisaa/12
وَلَكُمْ نِصْفُ مَا تَرَكَ أَزْوَاجُكُمْ إِن لَّمْ يَكُن لَّهُنَّ وَلَدٌ فَإِن كَانَ لَهُنَّ وَلَدٌ فَلَكُمُ الرُّبُعُ مِمَّا تَرَكْنَ مِن بَعْدِ وَصِيَّةٍ يُوصِينَ بِهَا أَوْ دَيْنٍ
Na fungu lenu ni nusu walicho acha wake zenu ikiwa hawana mtoto. Wakiwa na mtoto basi fungu lenu ni robo ya walicho acha, baada ya wasia waliyo usia au kulipa deni. Na wake zenu watapata robo mlicho kiacha, ikiwa hamna mtoto. Mkiwa mna mtoto basi sehemu yao ni thumni ya mlicho kiacha, baada ya wasia mlio usia au kulipa deni
Ndoa, katika mtazamo wa kisheria, ni msingi wa kwanza katika kujenga jamii ya kiislamu iliyo safi na tohara ikipelekea kuwepo utulivu katika jamii hii na kuhakikishiwa malipo mema huko akhera kwani ni mojawapo katika mambo ambayo yataweza kutuingiza katika pepo ikiwa tutakamilisha na kutekeleza vizuri misingi na taratibu za ndoa.
Miongoni mwa Hadithi za Mtume Swalla Allahu ‘Alayhi Wasallam zinazozungumzia juu ya ndoa ni

1. Kuiamrisha
: يا معشر الشباب من استطاع منكم الباءة فليتزوج؛ فإنه أغض للبصر وأحصن للفرج، ومن لم يستطع فعليه بالصوم، فإنه له وجاء. متفق عليه.
Enyi vijana mwenye kuweza miongoni mwenu kuoa na aoe kwani (ndoa huleta) kuinamisha macho na kinga kwa utupu na asieweza basi na afunge kwani hiyo ndiyo kinga. Bukhaari na Muslim

2. Kuilinda
: ثلاثة حق على الله عونهم: المجاهد في سبيل الله، والمكاتب الذي يريد الأداء، والناكح الذي يريد العفاف
رواه الترمذي وغيره وحسنه الألباني
Watu watatu ni haki yake Allah kuwasaidia; mwenye kupigana jihadi kwa ajili ya Allah, mwenye kuandikiana na Mtumwa (Kwa ajili ya kuachiwa huru) huku akiwa na nia ya kulitekeleza hilo, na mwenye kutaka kuoa akitaka kupata sitara na kujizuia na maovu.”
Attirmdhiy na wengineo na Sh. Albaani anasema ni Hadithi Hasan

3. Hukamilisha nusu ya dini
: إذا تزوج العبد فقد استكمل نصف الدين فليتق الله فيما بقي. صححه الشيخ الألباني في السلسلة الصحيحة
"Mwenye kufunga ndoa (atakuwa) amekamilisha nusu ya Imani (dini yake) na amuogope Allah katika nusu itakayobakia" Ameisahihisha Sh. Albaani katika Silsila Sahiha

4. Kuiraghibisha
"إذا أتاكم من ترضون خلقه ودينه فزوجوه إن لا تفعلوا تكن فتنة في الأرض و فساد عريض
صحيح الجامع
Atakapokujieni mtakaemridhia kwa tabia zake na dini yake basi muozesheni na kama hamkufanya itakuwa fitna katika ardhi na ufisadi mkubwa. Sahihul Jaami’i

5. Ndiyo starehe ya dunia
"الدُّنْيَا مَتَاعٌ وَخَيْرُ مَتَاعِ الدُّنْيَا الْمَرْأَةُ الصَّالِحَةُ" مسلم
Dunia ni starehe. Na starehe iliyo bora kwa dunia ni mwanamke aliye mwema. Muslim
Pia ndoa ni muhimu kwa sababu
· Huitekeleza Sunna ya Mtume Swalla Allahu ‘Alayhi Wasallam.
· Hupata jamii iliyojengeka katika misingi sahihi.
· Huiepusha jamii na tabiya chafu ambazo wasiooa hupendelea kuzitekeleza.
· Huiepusha jamii na maradhi mengi.
· Kuwapa wanandoa hisia ya kwamba wao pia wanapendwa kama wanavyojipenda wao wenyewe.
· Hupatikana utajiri.
· Huifundisha jamii maana halisi ya kubeba majukumu  

YA KUZINGATIYA KABLA YA KUOA/KUOLEWA
· Ndoa ni moja katika alama na miujiza ya Allah Subhaanahu Wata’ala.
· Ndoa ni mojawapo ya rizki ambazo Allah Subhaanahu Wata’ala hugawa kwa waja wake.
· Ndoa ina haki, majukumu na uwajibikaji.
· Upungufu katika kutekeleza majukumu na kuwajibika ni mojawapo katika sifa za binadamu (aliyekamilika ni Allah Subhaanahu Wata’ala pekee).
· Ndoa ina mitihani na majaribu.

KWA NINI KUOA/KUOLEWA?
Jibu la suala hili ni muhimu. Ndiyo kitu cha kwanza kukiangalia kwa ukweli na moyo mkunjufu kwa kila anaejiandaa na ndoa. Kitu gani kinachotupelekeya kuoa/kuolewa? Hapa kuna mambo mengi kama:
· Kupata nafasi ya hadhi na heshima katika jamii
· Kupata watoto
· Kutafuta sitara
· Kujenga familiya bora
· Kuwaridhiya wazazi wawili
· Kukidhi hamu/shahawa za kijinsia
· Kufuata marafiki/mashoga na kadhalika
· Kupata mtu wa kupika na kuosha nguo na kadhalika
· Kupata mali na utajiri
· Kuepuka lawama na maudhi
Mifano hii inatupa picha kwamba kwa wanaoingia kwenye chuo cha ndoa huwa na malengo na sababu tofauti kulingana na hali na mazingira yao.
Tuangalie hadithi ya Mtume Swalla Allahu ‘Alayhi Wasallam ambayo pia inatufahamisha mambo ya kimsingi ambayo kwayo mwanamke huolewa.
Hakika Mtume Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam amesema:
تنكح المرأة لأربع: لمالها ولحسبها ولجمالها ولدينها، فاظفر بذات الدين تربت يداك. البخاري ومسلم
Mwanamke huolewa kwa mambo mane: Kwa (ajili ya) mali yake, kwa nasaba yake, kwa uzuri wake na kwa dini yake, basi mtafuteni mwenye dini (kwani) mikono yako itatakatika na michanga. Bukhaari na Muslim
Na pia Amesema:
: إذا تزوج العبد فقد استكمل نصف الدين فليتق الله فيما بقي. صححه الشيخ الألباني في السلسلة الصحيحة
"Mwenye kufunga ndoa (atakuwa) amekamilisha nusu ya Imani (dini yake) na amuogope Allah katika nusu itakayobakia” Ameisahihisha Sh. Albaani katika Silsila Sahiha.
Hapa ndipo umuhimu wa kujua lengo kabla ya tendo linapokuja. Kwani ndoa ni moja katika miundo mbinu ya jamii na hivyo ni vyema lengo likafahamika mapema na liwe katika sura na mtazamo sahihi kama tunavyosisitiziwa na Mtume wetu Swalla Allahu ‘Alayhi Wasallam.
HEKIMA YA KUWEPO NDOA
1 Kuitikiwa wito wa Allah Subhaanahu Wata’ala na Mtume wake Swalla Allahu ‘Alayhi Wasallam
2 Kupata ujira na thawabu
3
KWA NINI WENGINE HAWAFIKIRII NDOA?

Inawezekana kwa sababu tofauti kama
1 Sababu za kisaikolojiya
· Kuwa na khofu na wasiwasi
· Kuwa na udhaifu wa kudhani watashindwa kutimiza majukumu
2 Sababu za Kijamiii
· Ughali wa mahari
· Kusubiri mpaka mmojawapo awe tayari kwa ndoa
· Kusubiri kupata ajira, kazi au kibarua
· Kutofautiana kati ya wazazi na mtoto katika chaguo.
3 Sababu za kijinsia
· Kuweza kujitosheleza kijinsia kwa njia za haramu(zinaa)
4 Sababu za kielimu
· Kuendelea na masomo
Licha ya kuwepo sababu zote hizi turudi katika dini yetu na tuangalie kitu gani tunausiwa na Mtume wetu Swalla Allahu ‘Alayhi Wasallam katika suala zima la ndoa kwa mwenye uwezo wa kuhimili.


KWA NINI WENGINE HUCHUKIYA NDOA?

Ni kwa sababu tofauti kama
· Kulazimishwa kuolewa na mume asiyemtaka
· Kulazimishwa kuoa mke asiyemtaka
· Kuchelewa kuoa kwa kukosa uwezo
· Kutegemeya sifa za ujumla za familiya bila ya kufuatilia kwa undani
· Kumuandaa na kumwambia mtoto tokea utotoni kwake kwamba atamuoa/ataolewa na fulani
· Kutosimama kwa posa kwamba kila zikija huwa zinarudi.
· Kuzuiliwa mwanamke kuolewa kwa khofu na wasiwasi usiokuwa na msingi wa kidini

Post a Comment

0 Comments