ads

NDEGE NATUA MTINI


Nimeutua makini, mtini nimetulia
Miba iliyopo chini, nashindwa hata kutua
Natazama kuliani, jua linaniwakia
Hali yangu tafurani, mvua yaninyeshea

Na upepo kushotoni, vumbi lanizungukia
Nguvu zaisha mwilini, nashindwa kuendelea
Punde harufu mwilini, puani yanipitia
Ahueni ya moyoni, faraja umenitia

Nilikuwa mawazoni, nani kunisaidia
Furaha yangu moyoni, waridi umetokea
Harufu yako mtini, nguvu umenipatia
Nakuahidi moyoni, mapenzi kuendelea

Waridi lenye thamani, awali sikudhania
Mpera mwarubaini, nilikuwa nawazia
Kwa makazi ya ugeni, amani kujipatia
Thamani yangu moyoni, waridi nakuridhia

Safari yangu ni ndefu, maji nilihifadhia
Kwa uzima wa harufu, kiu kimeniishia
Waridi mimi dhaifu, maji ninakupatia
Kwa mola wangu raufu, baraka nakuombea

Mimi leo ni mgeni, nakuomba maridhia
wewe wanipa thamani, mji nipate ujua
Mbawa naziweka chini, heshima nakupatia
Njiwa natua mtini, mingi nimeikimbia

**************** TAMATI****************
Mtunzi: Mwinyi Abdallah
          0655895599
Email: mwinyiabdallah2012@gmail.com

Post a Comment

0 Comments