ads

UTENZI:JUMA NA SUBIRA

🌺🌺💐💐🌺🌺💐💐🌺💐💐 

salamu nainudhumu,
moyoni mwangu adhimu
salamu alaykumu
leo tunashangiria.

uwanja umesafika
lengo limekamilika
leo tunaburudika
wajibu kusherekea

karibuni nyi wageni
karibuni uwanjani
karibuni ukumbini
pamoja kusherekea


mulosimama tueni
wambali karibieni
jambo lipo uwanjani
nataka kuwaambia

kwanza wale wasotaka
mola kaweka baraka
ndoa imeshafungika
pole ninawaambia

kwasheria na ibara
juma wake ni subira
ametimia idara
ndoa imeshatimia

vigele gele kidogo
tuifanye haja ndogo
tuwajibu kwa mapigo
ndoa wakifurahia

ninaloswali moyoni
nalimwanga uwanjani
kifaa hiki jamani
wapi ulijionea?

ulimuona njiani
au ndo pale sokoni
mmependeza ndoani
umejua kuchagua

ujumbe ninautuma
mlengwa ni kaka juma
mkeo sio mlima
kupanda kujishukia

mke ana haki zake
subira kwake ndo mke
yaweke mbali makeke
mkeo kufurahia

subira kwako ndo ua
subira kuvumilia
wewe amekuridhia
mema tuombe jalia

mke kwako ni heshima
mtunze sana ka juma
mapenzi ni taaluma
wengi wameshapotea

mkeo kwako ndio cheo
mkeo kwako ni kioo
ukitaka ubishoo
kwako kujiangalia

bibi harusi subira
kwanza nakupa hongera
umepata mume bora
yule ulo mchagua

puuza maneno yao
juma sasa ndo mumeo
achana na vipepeo
ua kukuharibia

ukiadhimu kutoka
bora ruhusa kutaka
uonapo kaudhika
rudi upate tulia

mume pia umlishe
bafuni umuogeshe
nguo pia mvalishe
daima atatulia

subira uwepo ndani
atapo rudi kazini
mpokee mlangoni
busu zito ungezea

kwa mapana na marefu
amewaacha maelfu
wewe ndie mnadhifu
juma amejinasia

subira ninakuasa
kupata kuna kukosa
mikasa iko na visa
daima kupotezea

wazazi nguzo imara
juma pia na subira
yawakutapo madhara
kwao mbio kurejea

tamati nimefikia
ujumbe kuwapatia
kheri nina watakia
mola kuwaongozea

kwaherini maharusi
kwaheri bibi harusi
juma pia mahususi
baraka mawaombea

by: mwinyi abdallah
phone no: 0655895599
Email: mwinyiabdallah2012@gmail.com
💐💐💐💐💐💐💐💐💐💐💐💐💐💐💐💐💐💐💐💐💐💐💐💐

Post a Comment

0 Comments