Imetayarishwa na
Muhammad Faraj Salem Al Saiy
Mwenyezi Mungu Amemleta Mtume wake Muhammad (Swalla
Llaahu ‘alayhi wa sallam) akiwa kama ni mletaji habari
njema na muonyaji ambaye hakuacha jambo lolote la kheri isipokuwa ametujuulisha
nalo na kutuhimiza kulikimbilia, na hakuacha jambo lolote la shari isipokuwa
ametutahadharisha nalo.
Na kwa vile Ummah huu ni Ummah wa mwisho, basi
Mtume huyu mtukufu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) ametuletea kutoka kwa Mola
wake dalili za kutosha zilizo wazi, zenye kutujuulisha juu ya kukaribia kwa
Siku ya Qiyaamah. Akatubainishia kwa ulimi wake, tena
kwa ufasaha kabisa, juu ya baadhi ya yatakayotokea katika mwisho wa zama. Akatuhakikishia
kuwa yote hayo lazima yatatokea, haya yote yakiwa ni
dalili juu ya ukweli wa Utume wake (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam)
utakayowafanya watu wajitayarishe vizuri na Siku hiyo. Siku ambayo mtu hatovuna
isipokuwa kile alichochuma, na hatokuwa na wakumlaumu
isipokuwa nafsi yake.
Mwenyezi Mungu Anasema:
{{“Isije ikasema nafsi (asije akasema
mtu); “Eee majuto yangu kwa yale niliyopunguza upande
wa Mwenyezi Mungu, na hakika nilikuwa miongoni mwa wanaoyafanyia mzaha (mambo
ya diyn)”.
Au ikasema; “Kama
Mwenyezi Mungu angeniongoa bila shaka ningekuwa miongoni mwa wenye kumcha
Mwenyezi Mungu”.
Au ikasema ionapo adhabu; “Kama
ningepata marejeo (ya
kurejea tena duniani) ningekuwa miongoni mwa wafanyao mema”.
(Ataambiwa) “Kwa
yakini! Bila shaka zilikujia Aayah (dalili) zangu
ukazikadhibisha na ukajivuna na ukawa miongoni mwa wanaotakabari”.}}
[Az-Zumar: 56-59]
Katika kuzijua dalili hizo kisha kuziona
zikitendeka hapa duniani kunampatia mtu faida nyinigi sana
zikiwemo zifuatazo:
·
Kuwa na uhakika juu ya ukweli wa Utume wake Muhammad (Swalla
Llaahu ‘alayhi wa sallam).
·
Kujitayarisha
vizuri na Siku ya Qiyaamah. Kwani kwa
mfano mtu anapopewa habari juu ya meli
inayokaribia kuwasili bandarini, huingoja meli
hiyo huku akiwa na wasi wasi mwingi. Lakini anapoisika sauti ya selo ya meli hiyo, anakuwa na uhakika usio na shaka kuwa meli sasa imekaribia kweli kuwasili.
Mfano huu ni sawa na
mtu aliyejuulishwa juu ya dalili ya kukaribia kwa Siku ya Qiyaamah, kisha
akaziona dalili hizo zikitendeka mbele ya macho yake kama zilivyoelezwa na
Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam). Mtu huyo anakuwa na uhakika usio na shaka wa kuwepo kwa siku ya Qiyaamah.
·
Kwa
ajili hiyo, kuzijua na kuziona dalili za kukaribia kwa
Siku ya Qiyaamah kunaongeza pia yakini
juu ya ukweli wa kukaribia kwa Siku hiyo.
·
Kunamsaidia
mtu kutoyumbishwa na masaibu, mitihani na machafuko yanayotekea kila siku. Kwani akirudi katika
mafundisho ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) ataona kuwa
yote hayo yamekwishatajwa kuwa yatakuja kutokea.
·
Kunamsaidia
mtu aliyejisahau akawa anaikimbilia dunia, anapoziona dalili hizo zikitokea kikweli humkumbusha mtu huyo akawa
anaifanyia kazi Akhera yake
badala ya kuikimbilia dunia.
Kutokana na haya na
mengi mengineyo, Mwenyezi Mungu Akamfunulia Mtume wake (Swalla Llaahu ‘alayhi
wa sallam) baadhi ya dalili ya yale yatakayotokea kabla ya kuja kwa Siku ya Qiyaamah.
Mtume wa Mwenyezi Mungu
(Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) alikuwa anapozungumza juu ya dalili za
kukaribia kwa Siku ya Qiyaamah, mashavu yake yanageuka kuwa mekundu huku
akiipaza sauti yake juu kwa ghadhabu mfano wa Amiri Jeshi mwenye kulipa amri
jeshi lake.
Alikuwa pia akisema:
((“Nimeletwa baina yangu na Qiyaamah kiasi kama hiki”, huku akiashiria kwa kidole
chake cha shahada na cha pili yake.))
Zipo dalili zinazoitwa ‘dalili ndogo’ na zipo pia ‘dalili kubwa’ za Siku ya Qiyaamah. Nyingi
katika dalili ndogo zimekwisha tokea na kuonekana,
jambo lililowafanya Waislamu waongezeke imani na kumsadiki zaidi Mtume wao (Swalla
Llaahu ‘alayhi wa sallam). Wakati zitakapoanza kuonekana dalili kubwa, basi
zitatunga na kufuatana moja baada ya nyingine mpaka Qiyaamah
kitakaposimama. Lakini sisi tutazitaja hapa baadhi yake na
chache sana miongoni mwa ‘dalili ndogo’ tu.
Fitan
Neno ‘Fitan’ ambalo ni
wingi wa (plural ya) Fitnah; maana yake ni Mitihani. Lakini
neno hili linaongezeka maana yake kila linapozidi kutumika. Kwani neno hili linaweza kumaanisha misiba, madhambi, kufru,
mauaji, kuchomwa moto n.k.
Neno ‘Fitan’ pia linamaanisha vita vya wenyewe kwa wenyewe (civil wars). Mtume wa
Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) ametujuulisha juu ya Fitnah
nyingi sana zitakazotokea baada yake zikiwa kama ni dalili ya kukaribia kwa
Siku ya Qiyaamah. Fitnah zitakazomfanya mtu asiweze kutambua ipi haki na ipi baatwil. Fitnah zitakazozitetemesha nyoyo na kuiyumbisha imani, hadi kufikia kwamba mtu anaweza
akaamka asubuhi akiwa ni Muislamu na jioni yake akageuka kuwa kafiri, au
anaweza kuamka asubuhi akiwa kafiri na jioni yake akawa Muislamu.
Kila inapotokea fitnah, mtu hudhani kuwa hii
ndiyo itakayoangamiza, kisha humalizika na kutokea
nyingine kubwa kuliko ile. Na hali itaendelea hivyo mpaka
kitakaposimama Qiyaamah.
Anasema Abu Muusa Al-Ash’ary (Radhiya Allaahu
‘Anhu) kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu
‘alayhi wa sallam) amesema:
((Kinapokaribia Qiyaamah zitatokea
Fitnah nyingi mfano wa vipande vya usiku wenye kiza
kizito, mtu ataamka ndani yake akiwa Muislamu na jioni yake anakuwa kafiri, au
anakuwa wakati wa jioni Muislamu na asubuhi anakuwa kafiri. Aliyekaa katika
mtihani huo anakuwa bora kuliko aliyesimama, na
aliyesimama anakuwa bora kuliko mwenye kutembea taratibu, na mwenye kutembea
anakuwa bora kuliko anayekwenda mwendo wa kukazana.)) [Imepokewa na Imaam Ahmad,
Ibni Maajah, Al-Haakim na wengineo]
Imetolewa na Muslim pia kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya
Allaahu ‘Anhu) kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam)
amesema: ((Kimbilieni kufanya ‘amali njema kabla ya
kuja kwa Fitnah mfano wa vipande vya usiku wenye kiza kizito, mtu ndani yake
anaamka akiwa Muislamu na jioni yake anakuwa kafiri, au jioni anakuwa kafiri na
asubuhi anakuwa Muislamu. Mtu ndani ya Fitnah hizo anaiuza diyn yake kwa thamani ndogo ya dunia.)) [Imepokewa na Muslim]
Na maana ya neno ‘vipande vya usiku wenye kiza
kizito’, ni ule ubaya wa Fitnah hizo utakaomfanya mtu
achanganyikiwe asiweze kutambua baina ya haki na baatwil.
Kutoka kwa Ummu Salamah
(Radhiya Allaahu ‘Anha) amesema kuwa usiku mmoja Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla
Llaahu ‘alayhi wa sallam) aliamka akiwa na hofu nyingi huku akisema: ((Subhaana Llaah! Hazina ngapi alizoteremsha Mwenyezi Mungu,
na mitihani mingapi aliyoiteremsha Mwenyezi Mungu? Nani atakayewaamsha waliolala vyumbani mwao (akimaanisha wake zake),
huenda mtu akawa amevaa duniani akaenda uchi Akhera.))
Maulamaa wamelitafsiri neno ‘amevaa duniani akaenda
uchi Akhera’, tafsiri nyingi sana zikiwemo zifuatazo:
·
Mtu
tajiri mwenye nguo nyingi hapa duniani lakini hana ‘amali njema za kumsitiri huko Akhera.
·
Wengine
wakasema kuwa maana yake ni mtu mwenye kuvaa nguo
zisizomsitiri hapa duniani na huko Akhera hatokuwa na cha
kumsitiri.
Kuvunjwa
Kwa Mlango
Nitaanza kwa kutaja
baadhi ya Hadiyth alizozungumzia ndani yake Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla
Llaahu ‘alayhi wa sallam) Fitnah za mwanzo katika Uislamu, Fitnah zilizotokea
miaka michache baada ya kufariki kwake, mara baada ya kuuliwa kwa Khaliyfah wa
pili wa Waislamu ‘Umar bin Khatwaab (Radhiya Allaahu ‘Anhu).
Kutoka kwa Hudhayfah (Radhiya
Allaahu ‘Anhu) amesema kuwa:
‘Umar bin Al-Khattwaab (Radhiya Allaahu ‘Anhu)
aliuliza siku moja: “Yupi kati yenu aliyehifadhi
kauli ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) juu ya Fitnah?”.
Hudhayfah akasema: “Mimi
nimehifadhi kama alivyosema”.
‘Umar (Radhiya Allaahu ‘Anhu) akamwambia: “Tuhadithie, kwani wewe ni jasiri”.
Hudhaifah (Radhiya Allaahu ‘Anhu) akasema: “Fitnah ya mtu katika ahli yake (watu wa nyumba yake) na
mali yake na jirani zake zinaondoka kwa kuswali na kutoa Sadaka na kwa
kuamrisha mema na kukataza mabaya”.
‘Umar akasema: “La, mimi sikusudii (fitnah) hizi, bali zile zinazorusha mawimbi
(makubwa) kama mawimbi ya bahari”.
Akasema: “Ewe Amiri
wa Waislamu! Wewe umeepukana nazo Fitnah hizo, kwani baina
yako na baina yake (Fitnah hizo) upo mlango uliofungwa”.
‘Umar akauliza: “Mlango
huo utafunguliwa au utavunjwa?”
Akasema: “La, bali
utavunjwa”.
‘Umar (Radhiya Allaahu ‘Anhu) akasema: “Kwa hivyo hautofungika tena...” Na katika riwaya
nyingine akasema: “Kwa hivyo hautofungika mpaka
Siku ya Qiyaamah?”
Wakamuuliza (waliokuwa wakimsikiliza Hudhayfah baada
ya kufa kwa ‘Umar): “Aliujua?”
Na katika riwaya nyingine: “’Umar alikuwa akiujua
mlango huo?”.
Hudhayfah (Radhiya Allaahu ‘Anhu) akawaambia: “Naam kama (anavyojua kuwa)
usiku wa leo unakuja kabla ya usiku wa kesho)”.
Masruuq bin Al Ajda-a
alipomuuliza Hudhayfah (Radhiya Allaahu ‘Anhu): “Nani
mlango huo”.
Akasema: “(Mlango
huo ni) ‘Umar.”
Kisha Hudhayfah (Radhiya Allaahu ‘Anhu)
akawaambia: “Mimi nilimuhadithia ‘Umar Hadiyth
(hii) kama nilivyomsikia Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla
Llaahu ‘alayhi wa sallam) bila makosa.”
Ikawa kama alivyotujuulisha
Msemakweli Muhammad (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam), kwani mlango huo
ulivunjwa mara baada ya kuuliwa Khaliyfah wa pili wa Waislamu ‘Umar bin Al-Khattwaab
(Radhiya Allaahu ‘Anhu). Kuanzia hapo Fitnah zikafunguka na
kuenea na kukithiri, na Fitnah ya mwanzo ilikuwa kuuliwa kwa Khaliyfah wa tatu
wa Kiislamu- Mwenye Nuru mbili ‘Uthmaan bin ‘Affaan (Radhiya Allaahu ‘Anhu).
[Imepokewa na Al-Bukhaariy,
Muslim na At-Tirmidhiy]
Kuuliwa
Kwa ‘Uthmaan (Radhiya Allaahu ‘Anhu)
Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi
wa sallam) aliwahi kumbashiria ‘Uthmaan bin ‘Affaan (Radhiya Allaahu ‘Anhu)
kuwa atakumbwa na mtihani mkubwa.
Kisa chenyewe ni kama
ifuatavyo:
Anasema
Abu Muusa Al-Ash’ary (Radhiya Allaahu ‘Anhu) kuwa siku moja alimuona Mtume (Swalla
Llaahu ‘alayhi wa sallam) akielekea katika kisima kilichozungushiwa ukuta.
Abu
Musa Al-Ash’ary anasema: “Nikasema: Leo mimi nitakuwa mlinzi wa Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa
sallam).” Nikamuona Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa
sallam) akielekea kisimani, akakidhi haja yake kisha akakaa juu ya kisima huku
akining’iniza miguu yake.
Akaja
Abu Bakr akataka ruhusa ya kuingia ndani, nikamwambia: “Hapo
hapo ulipo, ngoja kwanza usiingie mpaka nikakuombee ruhusa kwa
Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam)”. Nikamwendea
Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) na kumwambia: “Abu Bakr anataka ruhusa ya kuingia”, Akanambia: ((Mruhusu aingie, na mbashirie Pepo)). Nikafanya
hivyo, akaingia na kukaa juu ya kisima kuliani kwa
Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) na kuining’iniza miguu yake kama
alivyofanya Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam).
Mlango ukagongwa tena.
Nikatamani mgongaji awe ndugu yangu. Nikauliza: “Nani?”,
“’Umar bin Al-Khattwaab”, Nikamwambia: “Hapo
hapo ulipo, usiingie mpaka kwanza nimjulishe Mtume wa
Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam)”. Mtume (Swalla Llaahu
‘alayhi wa sallam) akanambia: ((Mruhusu aingie, na mbashirie Pepo)). Nikafanya hivyo, na ‘Umar naye akaingia na kukaa juu ya kisima kushotoni kwa
Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) na kuining’iniza miguu yake kama
walivyofanya wenzake.
Haujapita
muda mlango ukagongwa tena: Nikatamani mgongaji awe ndugu yangu. “Nani?” “‘Uthmaan bin ‘Affaan”. Nikamwambia: “Hapo hapo ulipo, usiingie mpaka kwanza nimjulishe Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam)”. Nilipomjulisha,
Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) akanyamaza muda kidogo, kisha akanambia:
((Mruhusu aingie na mbashirie
Pepo baada ya kupambana na mtihani mkubwa)). Nilipomwambia hivyo, ‘Uthmaan
akasema: “Allaahul-Musta’an”, (na katika riwaya nyingine alisema: “Tutakuwa
na subira In shaa Allaah”). Kisha akaingia, lakini ‘Uthmaan
hakupata pa kukaa, akaenda upande wa pili akakaa akiwa amekabiliana nao.
Anasema
Abu Muusa (Radhiya Allaahu ‘Anhu): “Nikahisi kama
hivi ndivyo makaburi yao yatakavyokuwa, na nikatamani ndugu yangu naye aje”.
[Imepokewa
na Al-Bukhaariy]
Ingawaje ‘Umar bin Khattwaab (Radhiya Allaahu
‘Anhu) aliuliwa kama alivyouliwa ‘Uthmaan (Radhiya Allaahu
‘Anhu), lakini ‘Umar aliyeuliwa na kafiri anayeabudu moto wakati akiswalisha Swalah
ya Alfajiri hakupata misukosuko kama aliyopata ‘Uthmaan (Radhiya Allaahu ‘Anhu)
kabla ya kuuliwa kwake.
Baada ya kuuliwa ‘Uthmaan (Radhiya Allaahu
‘Anhu) Fitnah zikawa nyingi, khitilafu zikaongezeka, hata Maswahaabah (Radhiya
Allaahu ‘Anhu) walishiriki katika vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Mnayaona
Ninayoyaona Mimi?
Siku moja alipokuwa akisimamia ujenzi wa ngome katika mji wa Madiynah, Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla
Llaahu ‘alayhi wa sallam) aliyekuwa akiyajuwa yote hayo kuwa yatatokea,
aliwauliza Maswahaba wake: ((Mnaona ninayoyaona?))
Maswahaba (Radhiya Allaahu ‘Anhum) wakasema: “Hatuoni (kitu) ewe Mtume wa
Mwenyezi Mungu.”
Mtume wa Mwenyezi Mungu
(Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) akasema: ((Mimi
naona mapigano mengi yakitokea baina ya nyumba zenu, wingi wa nyumba kubwa
kubwa (zinazowakusanya watu wengi ndani yake).))
Fitnah nyingi zilizowakumba Waislamu zilitokea
upande wa Mashariki ya dunia, na Fitnah ya mwanzo
iliyoleta mfarakano baina ya Waislamu ilitokea upande huo wa Mashariki, jambo
ambalo bila shaka lilimfurahisha sana Shaytwaan. Na haya yanakubaliana na maneno ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi
wa sallam) aliyetujuulisha kuwa huko ndiko kwenye pembe ya Shaytwaan.
Kutoka kwa Ibn ‘Umar (Radhiya
Allaahu ‘Anhu) amesema kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa
sallam) amesema huku akiashiria upande wa Mashariki: ((Fitnah
ipo huku, Fitnah ipo huku, kutakapotokeza pembe ya Shaytwaan.))
[Imepokewa na Al-Bukhaariy na Muslim]
Habari hizi alizotujuulisha Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) zilianza
kuonekana tokea mwanzo wakati yalipotokea mapigano ya wenyewe kwa wenyewe, jambo
ambalo bila shaka yoyote lilimfurahisha sana Shaytwaan.
Anasema Shaykh Yuusuf bin ‘Abdillaah Al-Waabil
kuwa: “Kutoka upande wa mashariki Fitnah nyingi sana zilitokea. Kwani huko
ndiko yalipoanza mapigano ya wenyewe kwa wenyewe baina
ya Waislamu. Kutoka huko umekuja Ukadiani, Ukoministi.
Matartar pia wametokea huko katika karne ya saba ya
Hijriyyah, wakaangamiza na kueneza shari kubwa sana”.
“Hadi hii leo”,
anaendela kusema Shaykh Yuusuf: “Fitnah zinaendelea kutujia kutokea upande huo
wa Mashariki ya dunia na hata Yajuju na Majuju watatokea upande huo huo”.
Kupotea
Kwa Amaanah
Kutoka kwa Abu Hurayrah
(Radhiya Allaahu ‘Anhu) kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa
sallam) amesema: ((Uaminifu utakapoondoka basi
isubirini Sa’ah (kingojeeni Qiyaamah).)) Akaulizwa: “Vipi unapotea (uaminifu) ewe Mtume wa
Mwenyezi Mungu?”
Akasema: ((Mambo
yakiegemezwa kwa wasiostahiki, basi isubirini Sa’ah.))
[Imepokewa na Al-Bukhaariy, Kitaabur-Riqaaq]
Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam)
akatubainishia pia kuwa uaminifu utatoweka katika nyoyo na
kubaki athari yake tu.
Imepokewa kutoka kwa Hudhayfah
(Radhiya Allaahu ‘Anhu) kuwa amesema: “Mtume wa
Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) amenihadithia mambo mawili, na
mojawapo katika hayo nimekwishaliona likitokea na ninalisubiri la pili (nilione
pia). Amenihadithia kuwa uaminifu utatoweka.
Amenihadithia kuwa amaanah (ilipoteremshwa), iliteremshwa ndani ya mizizi ya
nyoyo za watu, kisha iilipoteremshwa Qur-aan wakaijua zaidi, kisha wakaijua
(vizuri zaidi) kupitia katika Sunnah (Mafundisho ya Mtume wa
Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam)).”
Kisha akatuhadithia juu ya kunyanyuliwa
(kupotea) kwa amaanah akasema: ((Mtu analala usingizi huku amaanah inafutwa moyoni mwake na kubaki
athari yake tu, mfano wa doa lisilokuwa na rangi. Kisha analala usingizi
(mwingine) na amaanah inafutwa (‘tena’ - yaani hilo
doa lililobaki). Kisha itabaki amaanah mfano wa alama
(ya ngozi iliyokunjika) inayobaki mkononi baada ya mtu kunyanyua kitu”,
(inayotoweka baada ya kupita muda mdogo) (au) maumivu yanayobaki mguuni baada
ya kukanyaga kijinga kidogo cha moto (pakafanya lenge lenge kisha likakauka).))
Kisha Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam)
akasema: ((Kisha watu watakuwa wanafanya biashara na hapana hata mmoja kati yao atakayekuwa muaminifu, itafika
hadi kusemwa; “Katika watu wa kabila Fulani yupo mtu mmoja muaminifu. Na hata
itafika hadi watu watakuwa wakimsifia mtu huku wakisema: ‘Mwanamume kweli huyu,
mkarimu kweli huyu, ana akili kweli huyu’, (atapewa sifa zote hizo) wakati mtu
huyo hana imani (wala uaminifu) hata yenye uzito wa
hardali.))
Hudhayfah (Radhiya Allaahu ‘Anhu) akaendela
kusema: “Nimekwishaiona zama
ambayo ndani yake uaminifu baina ya watu ulikuwepo. Na sikuwa nikijali
ninafanya biashara na nani (kwa sababu watu wote
waaminifu), akiwa mtu huyo ni Muislamu basi Uislamu wake utamfanya asiipoteze
amaanah yake. Na kama mtu huyo ni Mkiristo au Myahudi,
basi atakuwa anafanya kama anavyotakiwa (kutonidhulumu haki yangu). Ama wakati
huu wa leo, uaminifu umeondoka, na khiyaanah
imedhihiri na sitofanya biashara isipokuwa na fulani au fulani (tu)”.
Yaani alikuwa akifanya biashara na baadhi ya watu wachache tu alokuwa akiwaamini.
Hudhayfah (Radhiya Allaahu ‘Anhu) aliishi muda
baada ya kuuliwa kwa ‘Uthmaan bin ‘Affaan (Radhiya
Allaahu ‘Anhu).
[Imepokewa na Al-Bukhaariy
na Muslim]
Anasema Shaykh Yuusuf bin ‘Abdillaah Al-Waabil aliyeandika
kitabu cha Ashraatwus-Sa’ah kuwa: “Miongoni
mwa dalili za kupotea kwa amaanah ni kule kupewa ufalme, uongozi au uhakimu watu
wasiokuwa waadilifu wala waaminifu. Kwani viongozi
wanapotengenea, raia nao hutengenea. Ama huko juu
kukiharibika, basi chini nako kutaharibika pia. Na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam)
amekwishatujuulisha kuwa utafika wakati wa hadaa, mambo yatakapokwenda kinyume.
Wakati huo, muongo ndiye atakayesadikiwa na mkweli
atakadhibishwa, na muaminifu ataitwa haini na haini ndiye atakayeaminiwa”.
Kubebeshwa mzigo wa
uongozi watu wasioijali Dini yao, ni dalili ya watu kutojali maamrisho ya Dini
yao. Na dalili ya upungufu wa Ma’ulamaa na kuongezeka
kwa ujinga, na hizi pia ni katika dalili za kukaribia kwa Qiyaamah alizozitaja
Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam).
Mtume wa Mwenyezi Mungu
(Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) amesema: ((Katika
dalili za kukaribia kwa Qiyaamah ni kupotea kwa elimu na kuongezeka ujinga.))
[Imepokewa na Al-Bukhaariy]
Kushindana
Na Kujisifia Katika Kuipamba Misikiti
Imepokelewa kuwa Mtume wa
Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:
((Katika dalili za kukaribia kwa Qiyaamah ni watu kushindana na kujisifia katika kuipamba
misikiti.)) [Imepokewa na An-Nasaaiy]
Anasema Al-Bukhaariy: Amesema Anas (Radhiya
Allaahu ‘Anhu) kuwa: “Watu wataipamba (Misikiti) lakini
hawaendi kuswali ndani yake isipokuwa wachache”.
‘Umar bin Al-Khattwaab (Radhiya Allaahu ‘Anhu)
alikataza watu kuipamba sana Misikiti kwa sababu mapambo yanawababaisha watu
ndani ya Swalah zao. Alipokuwa akisimamia utengenezaji wa
Msikiti wa Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) alikuwa akiwaambia wajenzi:
“Wakingeni
watu na mvua na msitie rangi nyekundu wala manjano mkawababaisha watu”. [Imepokewa na Al-Bukhaariy]
“Mwenyezi Mungu Amrehemu ‘Umar
bin Khattwaab (Radhiya Allaahu ‘Anhu)”, anasema Shaykh Yuusuf Al-Waabil, “kwani
watu hawakutoshelezeka na kuwakinga watu na mvua wala hawakutoshelezeka na rangi
za manjano na nyekundu, bali Misikiti siku hizi inapambwa na kujazwa nakhshi
mfano wa nguo inavyonakshiwa”.
Mauaji
Kutoka kwa Abu Hurayrah
(Radhiya Allaahu ‘Anhu) amesema kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu
‘alayhi wa sallam) amesema: ((Qiyaamah hakitosimama
mpaka ‘Haraj’ ikithiri.)) Wakamuuliza: “Ni
nini hii ‘Haraj’ ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu?” Akasema:
((Mauaji, mauaji!.))
[Imepokewa na Muslim]
Na katika riwaya nyingine iliyosimuliwa na Abu Muusa (Radhiya Allaahu ‘Anhu) kuwa Mtume wa Mwenyezi
Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) amesema: ((Kabla
ya Qiyaamah kusimama kutatokea ‘Haraj’.)) Wakamuuliza: “Ni nini hii ‘Haraj’ ewe Mtume wa
Mwenyezi Mungu?” Akasema: ((Mauaji)). Wakamuuliza:
“Kuliko tunavyoua? Tunaua
(vitani) katika mwaka mmoja zaidi ya alfu sabini?” Akasema: ((Si kama kuuwa kwenu washirikina,
bali huko ni kuuana nyinyi wenyewe kwa wenyewe.)) Wakasema: “Tutakuwa na akili zetu siku hiyo?” Akasema: ((Zitaondolewa akili za wengi wa
watu wa zama hizo. Watakuwa na wafuasi wengi kama
vumbi, wengi wao watadhani kuwa wameshika chochote (katika haki), lakini
(ukweli ni kuwa) hawana chochote.)) [Imepokewa na
Imaam Ahmad na Ibn Maajah]
Halikadhalika, imesimuliwa kutoka kwa Abu Hurayrah kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu
‘alayhi wa sallam) amesema: ((Naapa kwa Yule ambaye
nafsi yangu imo mikononi mwake, haitotoweka dunia mpaka iwajie watu siku ambayo
ndani yake muuaji hatojua kwa ajili gani ameua na wala aliyeuliwa kwa ajili
gani ameuliwa.)) Akaulizwa: “Yatakuwaje
hayo?” Akasema: ((Al-Haraj! aliyeuwa na aliyeuliwa (wataingia) Motoni.))
Haya yote yashatokea kweli katika zama zilizopita na tunayaona yakitokea katika zama zetu hizi
pia. Hasa baada ya kuvumbuliwa kwa silaha
zinazoangamiza.
Na katika Hadiyth sahihi iliyomo katika Mustadrak ya Al-Haakim, Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:
((Ummah wangu ni Ummah utakaohurumiwa, hawatokuwa na
adhabu huko Akhera, kwani adhabu zao ni za dunia, mauaji na mashaka na
mitetemeko.))
Mtu
Atatamani Kufa
Imepokelewa kuwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu
‘Anhu) amesema kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla
Llaahu ‘alayhi wa sallam) amesema: ((Hakitosimama Qiyaamah
mpaka mtu atakapopita penye kaburi la mtu akasema: “Yareti mimi ndiye
ningelikuwa mahali pake”.)) [Imepokewa na Al-Bukhaariy]
Na kutoka kwa Abu Hurayrah
pia, kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) amesema: ((Naapa kwa yule ambaye nafsi yangu imo mikononi Mwake,
dunia haitotoweka mpaka mtu atakapopita penye kaburi akasimama na kusema:
‘Yareti ningelikuwa mimi ndani ya kaburi hili”. Si kwa
ajili ya Dini, bali kwa ajili ya mitihani.)) [Imepokewa na Al-Bukhaariy]
Amesema Ibni Mas’uud (Radhiya Allaahu ‘Anhu): “Utakupitikieni wakati, mtu akiyakuta mauti yanauzwa,
basi atayanunua”.
Wanasema Ma’ulamaa kuwa mambo kama
haya si lazima yatokee katika kila nchi. Lakini yanaweza kutokea katika zama mbali mbali kutokana na mitihani mizito mbali mbali. Mtu
anapokumbwa na mitihani hiyo atakapopita makaburini
atahisi kama kwamba yule aliyelala ndani mule ndiye aliyestarehe. Ama yeye
anajiona yumo katika adhabu, misukosuko mashaka na
mitihani mikubwa isiyomalizika.
Kupigana
Na Warumi (Wakiristo)
Kutoka kwa ‘Awf bin Maalik Al-Ashjaiy (Radhiya
Allaahu ‘Anhu) amesema kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa
sallam) amesema: ((Hesabu mambo sita, lazima yatatokea
kabla ya kusimama Qiyaamah, miongoni mwa mambo sita hayo akasema: Kisha vita
vitasimamishwa baina yenu na watu wa manjano (Wakiristo), kisha watakufanyieni
khiana, watakujieni chini ya bendera themanini, chini ya kila bendera (watu)
elfu kumi na mbili.)) [Imepokewa na Al-Bukhaariy]
Siku moja alikuja mtu kwa
‘Abdullaah bin Mas’uud (Radhiya Allaahu ‘Anhu) akamwambia: “Ewe ‘Abdullaah! Qiyaamah kitasimama (karibu sana)”. ‘Abdullaah bin Mas’uud (Radhiya
Allaahu ‘Anhu) aliyekuwa amekaa akiwa ameegemea, akakaa vizuri kisha akamwambia:
“Hakika ya Qiyaamah hakitosimama mpaka kwanza mirathi isigawiwe na ngawira isifurahiwe”.
Kisha akasema huku akiashiria upande wa Shaam (upande wa Mashariki): “Maadui watajikusanya
kuwapiga vita Waislam, na Waislam watajikusanya kwa ajili ya kupambana nao”. Nikamuuliza:
“Warumi? (Wakristo?)” Akasema: “Ndiyo, na katika vita
hivyo wengi watartaddi, na Waislamu watatayarisha jeshi litakalokuwa tayari
kufa lisilokubali kurudi nyuma bila ushindi, watapigana vita mpaka usiku
utakapoingia, kisha watarudi nyuma hawa na wale, hapana mshindi kati yao, kisha
jeshi litaangamia. Kisha Waislamu watatanguliza jeshi (lingine) litakalokuwa
tayari kufa, watapigana vita mpaka wakati wa jioni,
kisha watarudi nyuma hawa na wale, hapana mshindi kati yao, kisha litaangamia
jeshi. Itakapoingia siku ya nne, Waislamu waliobaki
watakuja kuwasaidia, na Mwenyezi Mungu Atawajaalia ushindi uwe upande wao,
watapigana vita visivyopata kuonekana namna yake, hata ndege akipita juu yao,
basi ataanguka akiwa amekufa”. [Imepokewa na Muslim]
Kuja
Kwa Qahtwaaniy
0 Comments