ads

SHAIRI: VUMILIA WARIDI



Nimefurahi moyoni, nikaishika kalamu
Maneno yalo laini, nayaandika kwa hamu
Huenda ukabaini, ujumbe wake salamu
Vumilia mitihani, vumilia mahamumu.

Vumilia mitihani, mwenzio ninakutaka
Japo mengi miongoni, mengine ukakwazika
Na usiwe taabani, huzuni ikakushika
Nakuahidi mwandani, punde utafurahika.

Yanini uhuzunike, sio tabia nzuri
Nitakuwa mi mpweke, ukiwa huko dhahiri
Usizidishe makeke, na usiwe ni msiri
Nakupenda mwanamke, moyo wangu umekiri.

Nikuambie waridi, mwenzio nitaabani
Muda nwingine yabidi, nami niwe mawazoni
Ni kipindi cha baridi, maradhi tele mwilini
Ila kwako sina budi, tabibu wangu mwilini.

Safari yetu ni ndefu, miaka imesogea
Ukweli ninakusifu, kwangu umesubiria
Wapo wengi maarufu, moyoni ukatulia
Nimeipenda harufu, waridi najivutia.

Waridi linatulia, mtini linavutia
Wengine walidhania, harufu itapotea
Mvua yalinyeshea, jua linajiwakia
Wengi macho watolea, waridi limetulia.

Mpenzi acha huzuni, punde utafurahia
Salamu hii ni ngeni, bila shaka yavutia
Nimekupenda moyoni, leo nimekupatia
Wewe ndo wangu mwandani, wewe ndie maridhia

MTUNZI: Mwinyi Abdallah
                  Mwinyiabdallah2012@gmail.com
                  0655895599

Post a Comment

0 Comments