ads

IPI HUKUMU KIDINI



Naanza tena kwa hamu, salamu pia muhimu
Naanza kwa majukumu, akili yanidhulumu
Ukimya wanilaumu, kuitolea hukumu
Baraza liloadhimu, salamu alaykumu.

Najua mmetulia, kuwapa langu moyoni
Akilini naumia, ndugu yenu ni swalini
Jibu sijalipatia, lanitesa akilini
Mpenzi nimechagua, ipi hukumu kidini.


Nadhani ipo sababu, kisa kuwaelezea
Alikuwa ni swahibu, mimi kwake nikatua
Nikajenga ukaribu, bila yeye kutambua
Mpenzi nimechagua, ipi hukumu kidini.

Nikaanza kwa utani, mara switi mara hani
Siku nyingi si kifani, mara ukaka pembeni
Nikamteka imani, kila jambo samahani
Mpenzi nimechagua, ipi hukumu kidini.

Simu nikazizidisha, usiku mwingi chumbani
Mara vocha zinakwisha, matusi tele moyoni
Usiku kwangu waisha, simu iko sikioni
Mpenzi nimechagua, ipi hukumu kidini.

Bila shaka mwatambua, ujana sio rafiki
Mihemko yanijia, nikaona ninadhiki
Imani nikaivua, nikataka yaso haki
Mpenzi nimechagua, ipi hukumu kidini.

Mtoto akaridhia, mengi tukajifanyia
Jaribio kuishia, matokeo yanijia
Sasa mimi najutia, mtoto nje ya ndoa
Mpenzi nimechagua, ipi hukumu kidini.

Nawauliza jamani, pia nakukatazeni
Yamenifika moyoni, ndo mana nakwambieni
Haifai jamiini, sijaijua kidini
Mpenzi nimechagua, ipi hukumu kidini

MTUNZI:       Mwinyi Abdallah
                        Mwinyiabdallah2012@gmail.com
0655895599

Post a Comment

0 Comments