ads

SHAIRI: SAMAKI BAHARINI





Toka mawio njiani, naelekea kusini
Upepo wa baharini, umenitoa njiani
Nimekwama kisiwani, nawangoja majirani
Nikatupa baharini, nyavu dema kwenda chini

Samaki nilokusudi, ni changu mwenye madoa
Kwa madema sina budi, changu ninawangojea
Nikazidisha juhudi, madema yakapotea
Namuomba maabudi, nyavu ipate tulia

Upepo kuongezeka, gharika ikatokea
Bahari ikachafuka, nyavu ikanipotea
Nyavu nayo kutoweka, changu wakatokezea
Je wali utalika, mpwa nishagaa gaa

Nyenzo nilizotumia, zote zimenipotea
Tatu nilizichukua, ndoana imebakia
Wapi nitaifungia, na changu kuniletea
Ndoana inachagua, chochote kujinasia

Ndoana nimeifunga, kuitosa baharini
Samaki nilomtunga, amechopoka majini
Kidau changu chatinga, sijui nifanye nini?
Kupiga mbizi napanga, majini nizame chini

Wapo wengi baharini, samaki walo wazuri
Kwa changu nipo kazini, madoa yake mazuri
Nishajitosa majini, majira ya adhuhuri
Kuchagua humu ndani, kila changu ni Hariri

Jua sasa limezama, usiku umeingia
Kidau kimetuama, mbele chashindwa sogea
Dua zangu kwa karima, njia imenipotea
Sasa najipa lawama, sina nilojipatia

Tatizo sijalijua, narejea kwanza pwani
Ili nipate tulia, nisizidi matatani
Wazee walinambia, japo najenga utani
Endapo nimekosea, akili niweke chini.

MTUNZI:                             Mwinyi Abdallah
                                         Mwinyiabdallah2012@gmail.com
                                         0655895599

Post a Comment

0 Comments