ads

SHAIRI: FITINA



Janga hili kubwa sana, hasara likienea
Pengine mushaliona, lakini hamujajua
Wengine wanahiana, si shaka munatambua
Janga hili la fitina, udugu utakimbia

Udugu utaondoka, fitini ikienea
Tena komeni haraka, mbele tupate sogea
Kila uchao mashaka, nyuma tunajirudia
Mfitini kwa hakika, huna salama sikia

Mtume amehusia, kuachana na fitina
Wengine mwajifanyia, ndo njia ya kupendana
Komeni kuendelea, kiama mutaachana
Kwa jeuri endelea, na mungu hana hiana

Akatazalo manani, ukweli si la faida
Musikae vikaoni, mukaziunda na mada
Masikini hayawani, munaizinga na shida
Kwake mola rahmani, huna chako cha ziada

Fitina nakusudia, ndie mchwa maluuni
Na kama hamujajua, ni bora nikwambieni
Fitina ikienea. Udugu wote kandoni
Ni bingwa wa kuongea, kwa mola huna thamani

Zipange fitina zako. Uongo kujipangia
Subiri malipo yako, mola kakuandikia
Na ngoja ujira wako, mtume ametwambia
Moto ndo halali yako, akhera ukiingia

Sisemi haya kwa juu, mola mtamtambua
Wengine munadharau, kwa mola mtajutia
Kama nawe ni mdau, uongo bora ondoa
Fitina ni ukakasi, fitina ni kubwa asi

MTUNZI:       Mwinyi Abdallah
                        Mwinyiabdallah2012@gmail.com
                        0655895599

Post a Comment

0 Comments