AISHAH BINT ABU BAKR BIN QUHAAFAH
"UMMUL MUUMINIYN"
Ummu ‘Abdullah ’Aishah bint Abu Bakr ni mtoto wa Sahiba na mwenza wa Mtume Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam Abu Bakr bin Quhaafah maarufu kama ‘Assidiyq’.
Mama yake aliitwa Umm Raumaan bint ‘Aamir alizaliwa baada ya Mtume Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam kupewa utume kwa miaka mine au mitano. Alihama Makkah kwenda Madina pamoja na dada yake Asmaa, mama pamoja na kaka yao.
Kuna kauli zinazotofautiana wakati wa kuolewa kwake na kauli yenye nguvu ni kwamba aliolewa akiwa na umri wa miaka sita au saba na kuhamia kwenye nyumba ya Mtume Salla ‘Allahu ‘Alayhi Wasallam akiwa na miaka tisa. Kabla ya kuolewa, Mtume Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam aliwahi kuoteshwa ndoto na kuletewa sura ya Bi ‘Aishah na Jibriyl ‘Alayhi Ssalaam huku akimwambia :
( هذه زوجتك في الدنيا والآخرة ) رواه الترمذي وأصله في الصحيحين
"Huyu ndie mke wako katika dunia na peponi”. Attirmidhiy na asili yake ni katika sahihi mbili.
Waislamu wanaichukulia ndoa ya Mtume Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam kwa bibi ‘Aishah kama ni ndoa ya aina yake kwani Mtume Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam hakuwahi kuoa mwanamke bikra kati ya wakeze na pia huu ulikuwa ni muungano wa watu wawili wenye sifa za aina yake.
Bi ‘Aishah alikuwa mahiri na mwenye akili nzuri ya kuhifadhi mambo. Kwa muda wote aliokaa na Mtume Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam aliweza kukumbuka takriban yote aliyoyaona au kuyasikia kutoka kwa Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam kwa ufasaha .
Mengi yalikuwa yakitokea wakati huo kwani Qur’aan iliendelea kuteremshwa na matukio kutokea. Katika kipindi hiki ndipo dini ya kiislamu ilipoanza kupangika na kueleweka kwani pombe iliharamishwa, Qiblah kilithibitishwa na waislamu wakaanza kuelekea Al Ka’abah kusali badala ya Baytul Maqdis, pia halali na haramu katika dini zikabainishwa. Pia aya za Hijaab zikateremshwa, muongozo wa jinsi ya kufunga ukabainishwa pamoja na utoaji wa Zakaah na kadhalika.
Bi ‘Aishah, licha ya kuwa na umri mdogo alipoolewa, ni miongoni mwa masahaba wachache waliopokea zaidi ya Hadithi elfu mbili kutoka kwa Mtume Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam. Alikuwa akikaa na akina mama kuwafundisha aliyoyasikia au kuyaona kutoka kwa Mtume Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam enzi za uhai wake na mpaka Mtume alipofariki aliendelea kuwa chanzo cha elimu kwa masahaba wanaume na wanawake mpaka Sahaba Abu Musa Al Ash’ariy aliwahi kusema:
ما أشكل علينا أصحاب محمد - صلى الله عليه وسلم - حديثٌ قط فسألنا عائشة ، إلا وجدنا عندها منه علماً " رواه الترمذي
“Tukipata hadithi ambayo tuna mashaka nayo sisi masahaba basi hurudi kwa Bi ‘Aishah kwenda kumuuliza na kila tukienda hujifunza elimu kutoka kwake” Attirmidhiy
Waislamu tuna deni kubwa kwa Bi ‘Aishah kwani kupitia kwake tumeweza kumjua jinsi Mtume Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam akiishi na vipi ilikuwa tabia yake na vipi ulikuwa murua wake. Kwa kupitia kwake tumeweza kujua Sunnah nyingi za Mtume Salla Allahu ‘Allayhi Wasallam na kupitia kwake kwa kuweza kuzihifadhi sunnah hizi na kuzisimulia kwa ufasaha na usahihi wa kauli na vitendo ndipo matendo mengi ya ‘Ibadah zetu na akhlaaq – tabia tumeweza kuzipata.
Na hakuna mwanamke mwengine katika uislamu aliyehifadhi hadithi nyingi zaidi ya Aishah na hakuna mwanamke mwengine katika uislamu alieweza kuifahamu dini kama inavyotakikana kutokana na kuwa kwenye chimbuko la dini yenyewe Al Habib Mustafa Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam .Kama anavyosema Azzuhriy:
: لو ُجمع علم نساء هذه الأمة ، فيهن أزواج النبي - صلى الله عليه وسلم - ، كان علم عائشة أكثر من علمهنّ " رواه الطبراني
Lau kama elimu ya akinamama wote wa umma huu ingelikusanywa sehemu moja wakiwemo wakeze Mtume Salla ‘Allahu ‘Alayhi Wasallam, basi elimu ya Bibi ‘Aishah ingeliwapita wote kwa wingi wake” Attabraaniy.
Bi ‘Aishah alibahatika kuwa kipenzi cha Mtume Salla ‘Allahu ‘Alayhi Wasallam kwani Mtume hakuwa akificha mapenzi yake na sahaba Amr ibnul ‘Aas aliwahi kumuuliza:
أي الناس أحب إليك يا رسول الله ؟ " ، قال له : عائشة ) متفق عليه ،
“Ni nani unayempenda sana Ewe mjumbe wa Allah?” Akasema: “’Aishah” Bukhari na Muslim
Ushahidi mwengine wa kuthibitisha mapenzi yake kwa bi ‘Aishah ni pale Mtume Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam alipougua maradhi yaliyopelekea kifo chake aliwaomba wakeze wamruhusu auguzwe chumbani kwa Bi ‘Aishah.
Katika moja ya mambo aliyosifika nayo ni wivu kwa Mtume Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam. Hii ni dalili tosha ya kuonesha mapenzi ya dhati aliyokuwa nayo. Na kuna kauli aliwahi kuitoa juu ya wivu wake kwa kusema:
وما لي لا يغار مثلي على مثلك ؟
Na kwa nini nisiwe na wivu kwa mfano wangu na wako? Muslim
Na kila Mtume Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam akioa mke basi hufanya haraka kwenda kumuona ili kuangalia kama ataweza kuiteka nafasi aliyekuwa nayo kwa Mtume Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam.
Na wivu wake mkubwa ulikuwa kwa Bi Khadijah, ingawa hakuwahi kukutana nae katika ukewenza, ila Mtume Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam alikuwwa akimtaja sana na kumsifia kama tulivyoona katika kisa chake.
Bi ‘Aishah pia hukumbukwa kuwa sababu ya kuteremshwa baadhi za aya katika Qur’aan. Aya ya kuruhusu kutayammam kwa wale waliokosa maji iliteremshwa baada ya tukio lililomkuta alipoazima chombo cha Asmaa kwa ajili ya kujisaidia na kilimpotea na hivyo kuchukua muda kurudi akikitafuta mpaka Mtume Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam akatuma masahaba kwenda kumtafuta na wakati wa sala kuwafikia wakiwa hawana maji ya kutawadhia.
Wakasali bila ya udhu na waliporudi kwa Mtume Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam wakamhadithia na hapo ikateremshwa aya ya kutayammam. Akasema Asyad bin Hudhayr kumwambia ‘Aishah:
جزاكِ الله خيراً ، فوالله ما نزل بك أمر قط إلا جعل الله لكِ منه مخرجاً ، وجعل للمسلمين فيه بركة " متفق عليه
“Allah akujaze kheri, Wallahi halijakufikia jambo lolote ila Allah hukujaalia njia ya kutokea na kuwajaalia baraka waislamu.
Bukhari na Muslim
Na pale alipojaribiwa katika mtihani mkubwa katika maisha yake pamoja na Mtume Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam katika kisa cha uzushi. Ambapo wanafiki walimzushia Bi ‘Aishah kwamba alifanya zinaa na Safwaan Ibnul Muattal baada ya kuwaona wakirudi pamoja wakati Bi ‘Aishah alipochelewa kurudi kujiunga na msafara na kukimbiwa.
Wanafiki waliitumia fursa hii kuenesha uzushi mpaka kumfikia Mtume Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam na jamii yote ya Madina kwa mwezi mzima ilizungumzia kisa hiki ambacho hakikuwa na ukweli wa aina yoyote. Hata hivyo ni Qur’aan ndiyo iliyokuja kumtoharisha Bi ‘Aishah na uvumi na uzushi. Annuur 11-13
إِنَّ الَّذِينَ جَاؤُوا بِالْإِفْكِ عُصْبَةٌ مِّنكُمْ لَا تَحْسَبُوهُ شَرًّا لَّكُم بَلْ هُوَ خَيْرٌ لَّكُمْ لِكُلِّ امْرِئٍ مِّنْهُم مَّا اكْتَسَبَ مِنَ الْإِثْمِ وَالَّذِي تَوَلَّى كِبْرَهُ مِنْهُمْ لَهُ عَذَابٌ عَظِيمٌ {11}لَوْلَا إِذْ سَمِعْتُمُوهُ ظَنَّ الْمُؤْمِنُونَ وَالْمُؤْمِنَاتُ بِأَنفُسِهِمْ خَيْرًا وَقَالُوا هَذَا إِفْكٌ مُّبِينٌ {12}
لَوْلَا جَاؤُوا عَلَيْهِ بِأَرْبَعَةِ شُهَدَاء فَإِذْ لَمْ يَأْتُوا بِالشُّهَدَاء فَأُوْلَئِكَ عِندَ اللَّهِ هُمُ الْكَاذِبُونَ
Hakika wale walio leta uwongo ni kundi miongoni mwenu. Msifikiri ni shari kwenu, bali hiyo ni kheri kwenu. Kila mtu katika wao atapata aliyoyachuma katika madhambi. Na yule aliyejitwika sehemu yake kubwa miongoni mwao, atapata adhabu kubwa Kwanini mlipo sikia khabari hii, wanaume Waumini na wanawake Waumini hawakuwadhania wenzao mema, na kusema: Huu ni uzushi dhahiri? Kwa nini hawakuleta mashahidi wane? Na ilivyo kuwa hawakuleta mashahidi wane basi hao mbele ya Allah ni waongo.
Baada ya tukio hili hakuna jambo baya lililosemwa juu ya Bi ‘Aishah kwani tayari Allah Subhaanahu Wata’ala ameshamlinda kutokana na hadhi yake na cheo chake kufikia Jibriyl kuweza kumfikishia Salaam
( يا عائشة هذا جبريل يقرأ عليك السلام ، فقالت : وعليه السلام ورحمة الله ) متفق عليه .
Anasema Mtume Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam; ‘ Ewe ‘Aishah huyu Jibriyl anakusalimia’. Akasema; ‘Wa’alayhi Ssalaam warahmatu llah’ Bukhari na Muslim
Hata hivyo bado kuna wanaojiita waislamu (mashia) ambao wamediriki kumdhania na kumtafutia ubaya Bi ‘Aishah na kumtaja kwa ubaya licha ya kutofanyika jambo hili enzi zake. Kwa kisingizio cha kujiepusha na ubaya wake!. Mama wa waumini, mke wa Mtume Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam katika dunia na peponi tujifunze kwa kujiepusha na mabaya yake!? Ni kioja cha kusikitisha. Annuur 15-19
إِذْ تَلَقَّوْنَهُ بِأَلْسِنَتِكُمْ وَتَقُولُونَ بِأَفْوَاهِكُم مَّا لَيْسَ لَكُم بِهِ عِلْمٌ وَتَحْسَبُونَهُ هَيِّنًا وَهُوَ عِندَ اللَّهِ عَظِيمٌ {15}وَلَوْلَا إِذْ سَمِعْتُمُوهُ قُلْتُم مَّا يَكُونُ لَنَا أَن نَّتَكَلَّمَ بِهَذَا سُبْحَانَكَ هَذَا بُهْتَانٌ عَظِيمٌ {16}يَعِظُكُمُ اللَّهُ أَن تَعُودُوا لِمِثْلِهِ أَبَدًا إِن كُنتُم مُّؤْمِنِينَ {17}وَيُبَيِّنُ اللَّهُ لَكُمُ الْآيَاتِ وَاللَّهُ عَلِيمٌ حَكِيمٌ {18}إِنَّ الَّذِينَ يُحِبُّونَ أَن تَشِيعَ الْفَاحِشَةُ فِي الَّذِينَ آمَنُوا لَهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ فِي الدُّنْيَا وَالْآخِرَةِ وَاللَّهُ يَعْلَمُ وَأَنتُمْ لَا تَعْلَمُونَ
Mlipo yapokea kwa ndimi zenu na mkasema kwa vinywa vyenu msiyo yajua, na mlifikiri ni jambo dogo, kumbe mbele ya Allah ni kubwaNa kwa nini mlipo yasikia msiseme: Haitufalii kuzungumza haya. Allah anakuonyeni msirejee tena kufanya kama haya kabisa, ikiwa nyinyi ni Waumini!Na Allah anakubainisheni Aya. Na Allah ni Mjuzi Mwenye hikimaKwa hakika wale wanao penda uenee uchafu kwa walio amini, watapata adhabu chungu katika dunia na Akhera. Na Allah anajua na nyinyi hamjui
Bi ‘Aishah alifariki katika mwaka wa 57 Hijriyah akiwa na miaka 63. Alizikwa Madina kwenye Baqi’i.( eneo la kuzikia ).
wabillah taufiq
0 Comments